Uwekezaji wa Serikali ya
Tanzania katika kuimarisha mifumo ya kukabiliana na majanga kupitia Kituo cha
Ufuatiliaji wa Majanga na Tahadhari ya Mapema (Situation Room) umeanza kuzaa
matunda, baada ya nchi mbalimbali za Afrika kuonesha kuvutiwa na namna kituo
hicho kinavyofanya kazi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi
wa mafunzo ya siku tatu kwa wataalamu kutoka Ghana, Togo na Burkina Faso
yanayofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa
Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Hosea
Ndagala, alisema kituo hicho kimeongeza uwezo wa nchi kuchakata taarifa za
viashiria vya majanga na kutoa taarifa za viashiria vya majanga na kutoa
tahadhari mapema kwa wananchi.
“Uendeshaji wa kituo hiki
unahusisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali wanaoshirikiana
kuchakata taarifa kwa pamoja, jambo linalosaidia kutoa tahadhari kwa wakati,”
alisema Brigedia Jenerali Ndagala.
Mkurugenzi Msaidizi wa kituo
hicho, Bi. Jane Kikunya, alisema wageni kutoka nchi hizo tatu wameonesha
kuvutiwa na mfumo wa ufuatiliaji wa majanga unaohusisha hadi ngazi za vijiji,
na wamepanga kuiga mfumo huo katika nchi zao ili kuimarisha usimamizi wa maafa.
Katika mafunzo hayo, washiriki
walielezwa namna kituo hicho kinavyokusanya taarifa kutoka sekta mbalimbali
kama hali ya hewa, maji, kilimo, na kijamii, kisha kuzichambua na kutoa taarifa
rasmi kwa vyombo husika na kwa wananchi.
Miongoni mwa wageni, Simboou
Akleso kutoka Togo alisema: “Tumekuja
Tanzania kubadilishana uzoefu kwa sababu mnafanya vizuri. Tumeshuhudia kwa
macho namna taarifa zinavyokusanywa, kuchakatwa na kuwasilishwa kwa wananchi.”
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.