Friday, December 7, 2018

WAZIRI MKUU AWATOA HOFU WAKULIMA WA KOROSHO


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewatoa hofu wananchi hususan wakulima wa korosho nchini baada ya kuwahakikishia kuwa korosho zao zote zitanunuliwa.
Amesema Serikali kupitia Bodi ya Mazo Mchanganyiko itanunua korosho zote na hakuna korosho za wakulima nchini ambazo zitabaki bila ya kununuliwa.
Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Desemba 7, 2018) alipozungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha korosho cha Terra akiwa njiani kwenda Dodoma.
Waziri Mkuu amesema bodi hiyo inaendelea kufanya thamini na kujiridhisha kama kweli korosho hizo zimezalishwa nchini na kuangalia viwango vya ubora.
Amesema baada ya kujiridhisha kuhusu viwango vya ubora na mkulima aliyepeleka ndiye mwenyewe ndipo taratibu za malipo hufanyika.
Waziri Mkuu amesema Serikali iliamua kununua korosho baada ya wafanyabiashara kutaka kuzinunua kwa bei ya chini ambayo haikuwa na tija.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha mkulima ananufaika na ndipo Rais Dkt. John Magufuli alisitisha ununuzi baada ya kuona wakulima wanataka kudhulumiwa.”
Waziri Mkuu amesema kuwa hadi sasa tayari tani 181,000 zimeshakusanywa, hivyo amewataka wakulima wa zao hilo nchini waendelee kuiamini Serikali yao.
Kadhalika, Waziri Mkuu ameupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuunga mkono jitihada za Serikali kukuza uchumi kwa kupitia sekta viwanda.
Awali, Meneja Utawala wa kiwanda cha Terra, Peter Ngwale alisema uwezo wao ni kubangua tani 6,000 kwa mwaka, ambapo tayari wamebangua tano 3,000.
Pia aliiomba Serikali iwasaidie katika suala la ubora wa korosho kwa kuwa kiwango cha ubora kinachoandikwa kinakuwa tofauti na uhalisia wa korosho  yenyewe.

 (mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.