Friday, April 9, 2021

Waziri Mhagama atoa maagizo 22 kwa Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu

 



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, ametoa maagizo kwa menejimenti ya ofisi hiyo ili kuboresha  utendaji katika ofisi hiyo kutokana na mabadiliko ya kiuongozi yaliyofanywa  hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.


Kwa sasa majukumu ya ofisi hiyo ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu yatakuwa yanasimamiwa na Katibu Mkuu mmoja na Manaibu Makatibu Wakuu wawili, awali majukumu hayo yalikuwa yanasimamiwa na  Makatibu Wakuu wa tatu kwa kila mmoja akisimamia majukumu yake.


Kabla ya kutoa maelekezo hayo kwenye kikao kazi na menejimenti ya ofisi hiyo kilichojumuisha wakuu wa idara, vitengo na taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo leo tarehe 9 Aprili, 2021 Jijini Dodoma, Waziri Mhagama amebainisha kutoridhishwa na baadhi ya watendaji kutoshiriki kikamilifu kwenye kikao cha Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala kama ilivyotakiwa na mkaguzi huyo.


“Kila tunachofanya ni kwa ajili ya taswira ya Mhe. Waziri Mkuu na  ofisi ya  Waziri Mkuu,  nasikitika miongoni mwetu tukishindwa kutekeleza wajibu wetu tutatia doa ofisi ya Waziri Mkuu. Katibu mkuu fikiria utaratibu wa kudhibiti uzembe lazima kila mmoja awajibike. Tumepanga katika mambo ya msingi hatutasita kufuatilia utendaji ili kila mmoja atekeleze wajibu wake.”Amesema Mhe. Mhagama.


Akitoa maagizo katika kikao hicho amewataka watumishi kutanguliza taifa kwa kila jambo pia na kuwa wazalendo katika kutekeleza majukumu yao. Aidha amewataka kutumia ubobezi wa  taaluma walizo nazo ili kuleta matokeo yenye tija kwenye ofisi hiyo. Amewasistiza kuwa wabunifu katika  utendaji wa shughuli zao kwa kuizingatia kasi ya serikali ya  awamu ya sita.


Aidha, Mhe. Mhagama ameagiza kufanyika kwa  vikao vya kila robo muhula ili kujipima na kutathimini namna ya utendaji wa shughuli za idara na taasisi za ofisi hiyo, amesisitiza vikao hivyo vitaweza kuchangia kuleta mabadiliko ya haraka ya kiutendaji katika idara zote na kupata matokeo yaliyo kusudiwa.


Pia, Mhe.Mhagama amezitaka Idara na Taasisi zilizo chini ya  ofisi hiyo kuendeleza dhana ya mshikamano katika utekelezaji wa shughuli za ofisi hiyo. Amefafanua kuwa mafanikio ya moja ya idara ya ofisi hiyo  ni mafanikio ya ofisi nzima hivyo amewataka watumishi wote kushirikiana.


Mhe.Mhagama ameagiza kuhakikisha Mabaraza ya wafanyakazi katika ofisi hiyo yaendelee kufanyika.Aidha,  amesisitiza kuhakikisha katika idara,wizara  na tasisi za serikali  pamoja na  kwenye sekta binafsi mabaraza hayo yanafanyika ili  waweze kuimarisha mauhusiano kati ya waajiri na wafanyakazi.


Aidha Waziri  ameagiza kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Aprili, mfumo wa kielektroniki wa vibali vya kazi na ukaazi kwa wageni  uwe umezinduliwa na kufanya kazi ili kudhibiti mianya ya rushwa. Mfumo huo utasaidia kupunguza urasimu wa utoaji vibali kwa wawekezaji.


“Tayari tumesha wafukuza baadhi ya maafisa kazi wanye tabia ya kupokea rushwa kwenye vibali, tunataka mfumo huo kusaidia kuondoa tatizo la  rushwa kwenye vibali, tunazo taarifa sisi tukisha pitisha utoaji vibali hivyo vinachukua zaidi ya wiki mbili havijatolewa ili kumfikia muhusika. Nataka mfumo huo uanze kufanya kazi.” Amesisitiza Mhe. Mhagama.


Pia, Mhe. Mhagama meagiza andaliwe kikao na maafisa rasilimali watu kutoka kwenye makampuni makubwa ya uwekezaji nchini,  ili waelezwe utaratibu sahihi wa utoaji vibali. Amefafanua kwamba baadhi ya mawakala wanao wasaidia makampuni hayo katika kupata vibali hivyo wamekuwa wakikiuka taratibu na tayari wamewachukulia hatua. Aidha ameagiza kuhakikisha kuwa mikataba ya ajira inatolewa na wajiri nchini pamoja na kuzingatia  masuala ya mishahara.


Mhe.Waziri ameagiza  kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi,  ufanyike utekelezaji wa  Mpango kazi wa  kushughulikia kero  na malalmiko za wafanyakazi, waajiri na  ya wadau wengine katika sekta ya kazi na ajira.Aidha,  ameagiza kufanyika ukaguzi kwenye makampuni na migodi, miradi ya kimkakati na makampuni, amesema kuwa ukaguzi huo utasaidia uwekezaji kuwa wa tija  kwa watanzania kwa kuwa  na uwiano wa ajira pamoja na mishahara. 


“Natambua tupo kipindi cha mpito cha kubadili mifuko ya hifadhi ya jamii nataka ndani ya wiki moja Katibu Mkuu hakikisha vikao vya kimkakati tulivyo viweka kwa kushirikiana vyama vya waajiri, vyama vya wafanyakazi na sisi serikali vinaanza kufanyika ili zoezi hilo liweze kukamilika kama lilivyo agizwa. ” Amesisitiza Mhe.Mhagama.


Masuala mengine ambayo ameagiza Mhe.Mhagama ni kufuatilia mradi wa kukuza ujuzi, mafunzo ya uwanagenzi, mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi kwa wahitimu, suala la migogoro kwa wafanyakazi kupitia tume ya usuluishi na uwamuzi, masuala ya mawakala kukagua mahali pa kazi. Pia ameitaka Kitengo cha Huduma za Ajira kushirikiana na Uhamiaji na Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa kuibua ajira zenye staha nje ya nchi na kuangalia masuala ya mikataba ya  ajira hizo.


Aidha,   ameelekeza utekelezaji wa maagizo yake kwenye miradi ya Mbigili na Mkulazi iliyopo chini ya NSSF. Ameagiza  aandaliwe kikao kazi  na timu ya NSSF kwajili ya miradi hiyo pia ameelekeza kukutana na maafisa matekelezo wa mikoa wa NSSF. Amesisitiza  na kuagiza ni muhimu shughuli zote zinazotekelzwa kwenye ofisi hiyo zizingatie kuhusisha masuala ya wenye ulemavu pia na ameataka wahakikishi hata sekta nyingine kufanya hivyo.


Kwa upande wake katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajiara na Wenye Ulemavu) Tixon Nzunda, amemhakikishia Waziri Mhagama kutekeleza Maagizo yote  kwa kuzingatia misingi ya weledi, Uadilifu, bidii ya kazi ili kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa kwa wakati.


Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi, Naibu Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Ngeriananga, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bw. Tixon Nzunda pamoja na Manaibu Makatibu Wakuu ; Profesa Jamal Adam Katundu na Kaspar Kaspar Mmuya.

MWISHO.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Bw. Tixon Nzunda akizungumza wakati wa kikao hicho, kuushoto kwake ni Profesa Jamal Adam Katundu na Kaspar Kaspar Mmuya.

Baadhi ya Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) wakifuatilia kikao cha Waziri wa Nchina Menejimenti hiyo alipokutana nao kwa lengo la kuboresha utendaji wa ofisi hiyo.
Kamishna Msaidizi Idara ya Kazi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Mwalwisi akichangia jambo wakati wa kikao hicho.
Baadhi ya Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) wakifuatilia kikao cha Waziri wa Nchina Menejimenti hiyo alipokutana nao kwa lengo la kuboresha utendaji wa ofisi hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akitoa ,maagizo kwa Menejimenti ya ofisi hiyo alipokutana nao kwa lengo la kuboresha utendaji wa shughuli za ofisi hiyo. Kulia kwake ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Nderiananga  na kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Bw. Tixon Nzunda (wa kwanza kulia), Naibu Katibu Mkuu Profesa Jamal Katundu (katikati) na Naibu Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Bw. Kaspar Mmuya (mwenye tai) wakifuatilia kikao hicho.
Baadhi ya Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) wakifuatilia kikao cha Waziri wa Nchina Menejimenti hiyo alipokutana nao kwa lengo la kuboresha utendaji wa ofisi hiyo.








EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.