Monday, November 1, 2021

Waziri Mhagama azindua rasmi Nembo ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru Jijini Dodoma

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (wa pili kutoka kulia) akiangalia nembo na kauli mbiu ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara kuelekea maadhimisho ya Sherehe za Uhuru Kitaifa Disemba 9, 2021. Wa tatu kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar (Sera na Uratibu) Mhe. Dkt. Khalid Salum, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Ashatu Kijaji. Kulia ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa. Kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa ratiba na shughuli za maadhimisho ya Sherehe za Uhuru Kitaifa zinazotarajiwa kufanyika Disemba 9, 2021.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar (Sera na Uratibu) Mhe. Dkt. Khalid Salum akieleza jambo wakati wa mkutano huo. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama.


Na: Mwandishi Wetu - DODOMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amezindua rasmi nembo maalum ya Maadhimisho ya sherehe za Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara ambazo Kitaifa zitakazofanyika Disemba 09, 2021 katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza hii leo Novemba 01, 2021 na waandishi wa habari Jijini Dodoma Mhe. Mhagama alieleza kuwa sherehe hizo zitafanyika kati uwanja huo mahali ambapo Tanzania Bara wakati huo Tanganyika ilipata uhuru wake mwaka 1961 kutoka wa Waingereza.

“Kwa heshima ya mafanikio ya kihistoria ya nchi yetu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ipo katika maandalizi ya sherehe hizo zitakazo tanguliwa na shughuli mbalimbali ambazo zitahusisha Wizara na Taasisi zote za Serikali kueleza hatua ambazo kila sekta imepiga tangu nchi ilipopata uhuru, ilipo sasa na inapoelekea” alieleza Waziri Mhagama

Waziri Mhagama alifafanua kuwa, shughuli za maadhimisho hayo zimeanza rasmi hii leo Novemba 1, 2021 ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu itatoa taarifa kwa wananchi kuhusu taswira nzima za maadhimisho hayo.

“Leo tunapoanza ratiba ya maadhimisho ya Sherehe za Uhuru kitaifa, tutazindua rasmi nembo na kauli mbiu ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara. Nembo hiyo itakuwa na picha ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekabidhiwa Uhuru wan chi yetu miaka 60 iliyopita kama heshima na kuthamini mchango wake katika historia ya Taifa letu,” alisema Mhagama

Aliongeza kuwa, Maadhimisho hayo yatahusisha mashindano ya Insha kwa  Wanafunzi wa  Shule za Msingi na Sekondari, Michezo, Sanaa, Ngoma za jadi, Makongamano ya Kikanda na Kitaifa, Mdahalo wa Kitaifa, Maonesho ya Maalum ya Vijana kuonesha Ubunifu na ujuzi katika sekta mbalimbali pamoja na Maonesho ya Biashara ya Kitaifa yatakayotanguliwa na Mkutano wa Uwekezaji yatakayofanyika  katika Mikoa yote ya Tanzania Bara Zanzibar  kuanzia Novemba 01, 2021 hadi tarehe 30 Novemba, 2021,” alisema Mhe. Mhagama

Aidha Mheshimiwa Mhagama alibainisha kuwa makongamano yatakayofanyika yataelezea mchango wa waasisi wa Taifa katika kupigania Uhuru wa Tanzania na kusaidia ukombozi wa nchi mbalimbali barani Afrika.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar (Sera na Uratibu) Dkt. Khalid Salum alipongeza hatua ya ushirikishwaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika hatua zote za maandalizi ya sherehe hiyo.

“Uhuru wa Tanganyika wa Disemba 09, 2021 ni baba wa Muungano wetu, lakini Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 nayo pia ni baba wa Muungano wetu. Uhuru na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ndiyo yaliyotufanya tuwe wamoja hadi hii leo,” alipongeza Mhe. Dkt. Mohamed.




EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.