Monday, July 18, 2022

Katibu Mkuu Dkt. Jingu ahimiza ufanisi ujenzi wa Mji wa Serikali


 Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu azitaka Wizara zote kuhakikisha zinasimamia ufanisi na weledi katika ujenzi Awamu ya Pili wa majengo ya Ofisi zao katika Mji wa Serikali Mtumba.

Ameyasema hayo mapema alipokutana na Wakurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara zote katika Ukumbi wa mikutano wa ofisi yake Jijini Dodoma kwa lengo la kujadili maendeleo ya ujenzi wa Ofisi za Wizara hizo zinzojengwa Mtumba Jijini Dodoma.

Dkt. Jingu alisema,kila wizara inajukumu la kuhakikisha majengo yanajengwa kwa viwango vinavyoendana na thamani ya fedha huku akiwataka kuendelea kufanya kazi kwa uzalendo kama ilivyoelekezwa.

“Viongozi wetu na wananchi kwa ujumla wana matarajio makubwa kuona mji wa Serikali unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa hatutarajii kuwa na delays,”alisema Dkt. Jingu

Aidha alizitaka kila Wizara kuendelea kuzingatia ubora katika kulifanikisha zoezi hilo huku wakiwasimamia wakandarasi na kuhakikisha kila vifaa vinavyonunuliwa vinakaguliwa na timu husika kabla ya matumizi.

Aliwasihii viongozi hao kuongeza rasilimali watu, vifaa na wataalamu ili kuweza kukamilisha ujenzi wa majengo hayo.

“kazi ya ujenzi izingatie viwango vilivyopo, katika hili tumeunda timu mbalimbali za kupitia na kukagua viwango ambapo tumewapa kazi BICO ya kufanya Quality assurance kuona mihimili ya majengo na mifumo mbalimbli ikiwemo ya maji, umeme na TEHAMA inakidhi vigezo hivyo naomba tuwape ushirikiano ili watimize kazi zao,”Alisisitiza

Hata hivyo Dkt. Jingu aliwasisitiza kuendelea kutoa taarifa za maendeleo ya ujenzi huo kila ifikapo tarehe 30 ya mwisho wa mwezi na kuwasilishwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu ili kujua na kuwa na uhakikika wa kazi inavyoendelea.

Katika hatua nyingine aliwasihi kuendelea kutunza miti iliyopandwa katika maeneo ya ofisi zao kwa kuzingati umuhimu wake wa kuboresha mazingira na kuupamba mji huo.

“Kila Wizara ihakikishe inatunza miti iliyopandwa na kuzingatia mikataba ya upandaji wa miti katika Mji wa Serikali,”alisisitiza Dkt. Jingu


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.