Friday, January 6, 2023

WAZIRI SIMBACHWENE AHIMIZA MAPAMBANO DHIDI YA UDHALILISHAJI WANAWAKE NA WATOTO


 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene ametoa wito kwa Walezi na jamii kwa ujumla kupiga vita dhidi ya udhalilishaji kwa Wanawake na Watoto mambo ambayo yanapoteza heshima na haiba kwa nchi yetu.

 “tushirikiane katika kutokomeza udhalilishaji kupinga, kuwafichua na kuwafikisha katika vyombo vya Sheria wale wote wanaofanya unyama huu kwa wanawake na Watoto, lakini pia hatunabudi kurejesha utamaduni wetu wa malezi ya pamoja ili kulidhibiti janga hili kwa jamii na Taifa kwa ujumla.”

wito huo ameutoa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha afya Shehia ya Uzi Mkoa wa Kusini Unguja katika sherehe ya kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Katika shughuli yetu kuu ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi   wetu huu, ambayo tayari tumeshaifanya kwa ukamilifu wake, hivyo iliyobaki kwetu ni kuhakikisha mradi huu   unakamilika kwa hatua zilizobakia ili kukidhi  malengo tuliyoyakusudia. 

tunaendelea kushuhudia mapinduzi makubwa ya kiuchumi yanayoendelea kufanyika nchi nzima na hii inathibitisha kauli ya mwaka huu isemayo “Mapinduzi yetu ndio Amani yetu tuyalinde kwa Maendeleo yetu”.

Aidha  serikali zetu zote mbili ya SMT na SMZ zimeendelea kusogeza huduma mbalimbali kwa wananchi wake na tunashuhudia ujenzi wa Miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo huu wa ujenzi wa Kituo cha Afya katika Shehia zetu za Uzi na Ng’ambwa. Mradi ambao unafadhiliwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF ambao ni miongoni mwa matunda ya Mapinduzi yetu yaliyofanyika Januari 12 mwaka 1964.

“ujenzi huu wa Kituo cha Afya umekuja baada ya kuona upo uhitaji mkubwa wa jengo hili kwa wanajamii wa Shehia zetu za Uzi na Ng’ambwa, hali ambayo itarahisisha upatikanaji wa huduma bora ya afya kwa wananchi hususani mama na watoto,”alisema Waziri.

Waziri amesisitiza ushirikiano wa hali na mali katika ufuatiliaji, usimamizi na utekelezaji wa mradi ili uweze kukamilika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu. Pia, amewaomba viongozi  wa  Mkoa, Wilaya, Baraza la Mji Kati na Shehia zote kuwa karibu katika kusimamia utekelezaji wa  mradi huo muhimu kwa jamii na Taifa kwa ujumla na kuendelea  kutoa msaada pale unapohitajika  ili kufanikisha ukamilishaji wa  mradi kwa wakati.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe Rashid Hadid Rashid amewapongeza TASAF kwa jinsi wanavyoshirikiana na serikali katika kutekeleza Miradi ya maendeleo.

“Katika kipindi kifupi cha miaka miwili wameweza kujenga ukumbi wa mitihani, Kizimkazi Dimbani na katika Maswala ya Kilimo cha Mwani, wazee wetu wanashughulika na kilimo hicho na walikuwa wanapata tabu kuchukua Mwani baharini kuja juu TASAF imewajengea ngazi  ili iwe rahisi kufika juu.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji - Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) Bwn. Ladisius Joseph Mwamanga amesema TASAF inajenga uwezo wananchi kwa kukuza rasilimali watu  katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Napenda kuwapongeza wananchi kwa ushirikiano mkubwa ambao wameuonesha katika ujenzi wa kituo cha afya uzi, mradi umesimamiwa kwa ukaribu na wananchi wenyewe wa Shehia ya Uzi na Ng’ambwa.”

Awali katika risala ya wananchi iliyosomwa Bi. Lemi Khalifa amesema utekelezaji wa mradi ulianza mwezi wa nane 2022 kwa kusimamiwa na kamati kuu mbili; kamati ya Shehia na kamati ya usimamizi ngazi ya jamii CMC.

“Mradi ulitengewa kiasi cha million 184,8 21,428 kati ya hizo shilingi million 134,270.261 zimetumika na ujenzi unaendelea.”


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.