Ofisi ya Waziri Mkuu imewezesha watu wenye ulemavu nchini kushiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kupitia Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA).
Ushiriki huo umewawezesha kuonesha bidhaa na huduma wanazotoa pamoja na kufanya biashara katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Akitembelea banda la SHIVYAWATA pamoja na banda la Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe. Ummy Nderiananga, alisema ameridhishwa na kiwango cha ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maonesho ya mwaka huu, akibainisha kuwa ushiriki huo umeongeza fursa za kiuchumi na kuwajengea kujiamini tofauti na miaka iliyopita.
Mhe. Nderiananga alisema Serikali imegharimia ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maonesho hayo bila wao kubeba gharama yoyote, hatua iliyowapa nafasi ya kutangaza bidhaa zao na kufanya biashara katika mazingira yenye usawa na heshima na kuhaidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha ushiriki huo katika miaka ijayo ili watu wengi zaidi wenye ulemavu wanufaike na fursa hizo.
Aidha, aliipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) pamoja na Taasisi nyingine zilizowezesha ushiriki huo, huku akizitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kutenga na kutoa mikopo ya asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kukuza shughuli zao za kiuchumi.
"Ni wakati sasa kwa watu wenye ulemavu kuendelea kuonesha uwezo wao katika uzalishaji na biashara. Kupitia maonesho haya tumejionea matokeo chanya ya uwezeshaji wa kiuchumi unaotokana na mikopo na fursa zinazotolewa na Serikali". alisema Mhe. Nderiananga.
Kwa upande wake, mwakilishi wa washiriki hao, Bi. Pili Bilahi, aliishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwawezesha kushiriki katika maonesho hayo bila kulipia gharama yeyote.
Pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi yanayowapa watu wenye ulemavu fursa za kiuchumi, ikiwemo kupitia mikopo ya asilimia mbili inayotolewa na halmashauri.
Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanaendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere chini ya kaulimbiu isemayo, "Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba ni Fahari ya Tanzania," yakilenga kukuza biashara, uwekezaji na ubunifu nchini.


EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.