Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Mhe.
Ummy H. Nderiananga (Mb), amesisitiza umuhimu wa kuharakisha urasimishaji wa
tasnia ya ukalimani wa Lugha ya Alama ya Tanzania, ili kuhakikisha watu wenye
ulemavu wa kusikia wanapata huduma kwa usawa.
Akifungua
kikao cha mashauriano kilichoandaliwa na Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA),
na kuhudhuriwa na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu
Tanzania (SHIVYAWATA), Wabunge pamoja na wadau mbalimbali, Jijini Dodoma, Mhe.
Nderiananga amesema hatua hiyo itasaidia kuweka viwango vya taaluma, kuboresha
mafunzo, na kutambua rasmi wakalimani wa Lugha ya Alama nchini.
Aidha,
Mhe. Nderiananga amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau
mbalimbali katika kuandaa miongozo na kanuni zitakazosaidia kusimamia taaluma
hiyo, huku akihimiza jamii kuongeza uelewa wa matumizi ya Lugha ya Alama, ili
kuondoa vikwazo vya mawasiliano.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa CHAVITA, Bi. Selina Mlemba amesema, urasimishaji wa
tasnia ya ukalimani wa Lugha ya Alama ni hatua muhimu katika kuhakikisha haki
za watu wenye ulemavu wa kusikia zinalindwa na kutekelezwa kwa vitendo.
Aidha
Bi. Mlemba ameongeza kuwa CHAVITA itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na
wadau wengine ili kuhakikisha kunakuwepo na miongozo, mafunzo, pamoja na mfumo
rasmi wa usajili wa wakalimani wa Lugha ya Alama nchini, sambamba na hilo
amesisitiza kuwa hatua hiyo itachangia kuongeza ubora wa huduma katika sekta
mbalimbali na kuwezesha ushiriki kamili wa watu wenye ulemavu wa kusikia katika
maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Washiriki
wa kikao hicho wameitaka Serikali kuipa kipaumbele tasnia hiyo, wakisisitiza
umuhimu wa ajira kwa wakalimani wa Lugha ya Alama katika sekta zote, pamoja na
kuimarisha mafunzo na utambuzi wa taaluma hiyo ili kuboresha huduma kwa watu
wenye ulemavu wa kusikia.

EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.