Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia masual aya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga
amezindua rasmi Mtandao wa Uwezeshaji wa Watu Wenye Ulemavu Mahali pa Kazi
nchini (National Business Disability Network – NBDN).
Mhe. Nderiananga amefanya uzinduzi
huo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete ambapo alikipongeza Chama cha Waajiri
Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Shirika Lisilo la Kiserikali la Sightsavers
International kwa kuona umuhimu wa kuwa na mtandao huo.
Alisema kuanzishwa kwa mtandao huo
utahakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata fursa sawa na kushiriki
kikamilifu katika soko la ajira akisema ni jambo la msingi kwa ustawi wa jamii
na kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa haki
za watu wenye ulemavu zinaheshimiwa na kuthaminiwa,” Alisema Naibu Waziri huyo.
Aliongeza kwamba Serikali imeendelea
kutekeleza Sera na Sheria mbalimbali zinazolinda haki za watu wenye ulemavu,
zikiwemo Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Watu Wenye Ulemavu na Sheria ya Watu Wenye
Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010.
Vile vile alibainisha kuwa watu
wenye ulemavu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mahali pa kazi, ikiwa ni
pamoja na unyanyapaa, ukosefu wa miundombinu rafiki, na uelewa mdogo wa waajiri
kuhusu uwezo wa watu wenye ulemavu katika kuchangia maendeleo ya taasisi na
taifa.
“Napenda kuwasihi waajiri wote wa
sekta binafsi nchini kuhakikisha kuwa wanazingatia masuala ya ujumuishaji kwa
kutoa nafasi kwa watu wenye ulemavu, si kwa misingi ya hisani, bali kwa
kutambua mchango wao katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Tunapaswa kuondoa
vikwazo vyote vinavyowazuia watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika soko
la ajira,”Alisisitiza.
Aidha Naibu Waziri huyo alifafanua
kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau
wote ili kuhakikisha kuwa ajenda ya ujumuishaji wa watu wenye ulemavu
inatekelezwa kwa ufanisi.
“Kwa pamoja, tunaweza kuleta
mabadiliko chanya na kujenga jamii jumuishi inayotoa fursa sawa kwa wote. Hata
hivyo, kupitia mtandao wa NBDN, nina imani kuwa changamoto hizi zitapungua kwa
kiasi kikubwa kwa kuwa utatoa mwongozo na kusaidia waajiri kutekeleza sera za
ujumuishaji kwa vitendo,”Alihimiza Mhe. Nderiananga.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.