Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga
amegawa futari kwa watu wenye ulemavu 500 kutoka Wilaya Saba za Mkoa wa Kusini
Unguja.
Akizungumza katika ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed
Shein, Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar Mhe. Nderiananga
aliwaomba waumini wa dini ya kiislamu na watanzania wote kuutumia mwezi
Mtukufu wa Ramadhan kwa kufanya ukarimu kwa wanyonge, wasiyojiweza
na watu wenye ulemavu.
Mhe. Nderiananga amegawa futari hiyo kwa
kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia watu wenye
ulemavu la Tanzania Foundation for Excellence in Disabilities (TFED)
iliyoambatana na dua maalum ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi katika utekelezaji wa majukumu yao ili Taifa
liwe na amani, umoja na mshikamano.
“Nimshukuru sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani
viongozi wetu hawa wamekuwa watu wema wametujali na kututhamini wakati wote.
Sisi watu wenye ulemavu Watoto wa Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi tumeona
ushirikishwaji mkubwa katika serikali na sekta binafsi,” Mhe. Nderiananga.
Pia alimpongeza Dkt. Samia kwa kuendelea kutoa
fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwani ni nia yake
njema kwa watanzania wote kuwa na maendeleo huanzia ngazi ya familia hadi Taifa
kwa ujumla.
Vilevile alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali
Mwinyi kwa kazi kubwa aliyoifanya katika utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo
kama ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami.
“Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali
Mwinyi amefanya kazi kubwa sana hapa Zanzibar barabara zimejengwa kila
mahali watu wanaendelea na shughuli zao. Sekta ya afya Dkt. Mwinyi
amewashangaza wengi kwa ujenzi wa hospitali za Wilaya zenye vifaa tiba vya kisasa,
sekta ya maji na elimu ambapo tunashuhudia ujenzi wa shule katika maeneo
yetu,”Alipongeza.
Aidha aliwasisitiza wazazi na walezi
kutowaficha watoto wenye ulemavu ndani na badala yake wawapeleke shule
kwani Serikali iko tayari kwa ajili ya kuwahudumia kuhakikisha wanatimiza ndoto
zao na kuwa nguvu kazi ya Taifa.
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani inayotarajiwa kuadhimishwa Machi 08 mwaka huu ameiomba jamii kuendelea
kuiamini nafasi ya mwanamke katika uongozi akisema Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mfano wa kuigwa hivyo wanawake
hawana budi kujitokeza kugombea katika nafasi mbalimbali pindi wakati
utakapowadia wa uchaguzi unatakaofanyika mwezi Oktoba 2025.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.