Tanzania imeendelea kutambuliwa kwa mchango wake katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, tathmini, utendaji na uwajibikaji kwa umma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha utawala na utendaji wa Serikali barani Afrika.
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, kupitia Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini, imewasilisha tuzo maalumu kwa Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Jim Yonazi, iliyotolewa kwa Tanzania kutokana na mchango wake katika kuboresha utawala barani Afrika kupitia ushiriki wake katika mtandao wa TWENDE MBELE.
Tuzo hiyo imewasilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini, Bi. Sakina Mwinyimkuu, ikitokana na matokeo ya kikao kazi cha TWENDE MBELE kilichofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Utambuzi huo unaonesha mchango wa Tanzania katika kuendeleza mifumo ya ufuatiliaji na tathmini inayosaidia kuboresha utendaji wa Serikali, kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mipango na programu za maendeleo.
Katika hatua nyingine, Bi. Mwinyimkuu amemkabidhi Dkt. Yonazi tuzo ya uongozi bora katika kuendeleza ufuatiliaji, tathmini na ujifunzaji nchini Tanzania.
Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa Kongamano la Tano la Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL) 2026, lililofanyika jijini Arusha.
Tuzo hizo ni sehemu ya utambuzi wa mchango wa Tanzania na uongozi katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, tathmini na ujifunzaji, ambayo ni muhimu katika kupima matokeo ya utekelezaji wa mipango ya Serikali, kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.