Wednesday, April 1, 2020

MAJALIWA: ATAKAYETHIBITIKA NA CORONA APELEKWE ENEO MAALUMU BILA KUJALI CHEO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesisitiza kuwa mtu yeyote akithibitika kuwa na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) apelekwe eneo maalum bila kujali cheo chake na atalala palipoandaliwa.


Amewataka Watanzania wazingatie masharti ya afya kwa kufuata ushauri unaotolewa na Serikali kwa sababu hivi sasa nchi yetu na dunia kwa ujumla inapitia katika kipindi kigumu pia,waendelee kupuuza taarifa za uzushi zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Aprili 1, 2020) akiwasilisha Bungeni hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2020/2021, Bungeni jijini Dodoma.

AmesemaMachi 11, 2020Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko wa Homa Kali ya Mapafu ijulikanayo kama COVID-19inayosababishwa na virusi vya CORONA kuwa ni janga la Kimataifa. Aidha, tarehe 16 Machi, 2020 Serikali ilitangaza kuwepo kwa mgonjwa wa kwanza nchini, ni muhimu wananchi kuchukua tahadhari

 

Waziri Mkuu amesema tangu kugundulika kwa ugonjwa huo, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukaguzi, upimaji na ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini.

 

Amesema la hatua hizo ni kuwabaini wasafiri wanaoonesha dalili za ugonjwa wa COVID-19 au wenye viashiria hatari, hata hivyo mashirika mengi yamesitisha ndege zao kwa kukosa abiria. “Abiria wote waingiao nchini hupelekwa Isolation house.”

 

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na virusi vya corona, Serikali ilitoa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na yafuatayo kusitisha Mbio za Mwenge wa Uhuru na fedha zilizotengwa kwa ajili ya jukumu hilo zitumike kusaidia hatua za kukabiliana na janga hilo.

 

“Mbali na kusitidsha mbio za mwenge Serikali imesitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu ikiwemo ligi kuu ya Tanzania Bara, ligi daraja la kwanza, ligi daraja la pili na aina nyingine za michezo.”


Amesema Serikali pia imesitisha shughuli zote za elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari, vyuo vya kati hadi vyuo vikuu pamoja na semina, warsha, makongamano na mikutano yote ya ndani na ya hadhara yenye kuhusisha mjumuiko wa watu wengi.

Amesema suala lingine ni kuwatenga abiria waingiao nchini kwenye maeneo maalum kwa siku 14 ili kufuatilia hali zao mpaka tutakapojiridhisha kuwa hana ugonjwa ili kuhakikisha maambukizi ya virusi hivyo hayasambai kwa jamii.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali inawasisitiza Watanzania kufuata kanuni za kudhibiti maambukizi ikiwemo kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni, kukinga unapokohoa na kupiga chafya, kutopeana mikono, kukaa au kusimama kwa umbali na jirani yako.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuwaasa Watanzania wenye safari zisizo za lazima kwenye nchi zenye maambukizi ya virusi vya Corona, kusitisha safari hizo, na hatua zingine zitafuata.

Amesema Serikali inaendelea na usimamizi wa karibu sambamba na kufanya tathmini na kuchukua hatua kadhaa. “Tumeunda Kamati za kitaifa tatu zinazosimamia ugonjwa huu, niendelee kusisitiza kuwa sote tuzingatie maelekezo yaliyotolewa na Serikali toka tulipoanza kampeni ya kupambana na ugonjwa huu.”

Wakati huo huo, Wazirti Mkuuamesema Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba liidhinishe jumla ya sh. 312,802,520,000; kati ya fedha hizo, sh. 88,429,156,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 224,373,364,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Vilevile Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh. 121,786,257,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, sh. 113,567,647,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 8,218,610,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

(MWISHO)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.