Wednesday, April 1, 2020

SERIKALI YAWEZESHA UPATIKANAJI AJIRA MILIONI 12.6

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uboreshaji wa huduma za jamii unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano umechangia kuzalisha ajira milioni 12.6 kwenye sekta mbalimbali nchini.

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili mosi, 2019) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2020/2021.

“Mafanikio haya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uboreshaji wa huduma za jamii yameenda sambamba na uzalishaji wa ajira zipatazo milioni 12.6 zikiwemo ajira za moja kwa moja milioni 11.7 kwenye sekta mbalimbali nchini,” amesema.

Akitoa mfano Waziri Mkuu amesema sekta za afya, elimu na utawala zimetoa ajira za kudumu kwa kuajiri watumishi 28,403 katika mamlaka za Serikali za Mitaa; ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) pamoja na kuboresha viwanja vya ndege umetoa jumla ya ajira 2,970 huku ujenzi wa viwanda nchini ukichangia ajira 41,900.

“Mradi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa umewezesha kuzalishwa ajira zipatazo 13,177 za kitaalam na zisizo za kitalaam. Kati ya hizo, ajira za kitaalam kwa wazawa ni asilimia 46.5. Pia, kupitia mradi huu kumekuwa na utoaji wa zabuni zenye thamani ya shilingi bilioni 664.7 kwa wazabuni na wakandarasi wa ndani 640,” ameongeza.

“Mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere kupitia maporomoko ya mto Rufiji umezalisha jumla ya ajira 3,897 ikiwemo ajira za wazawa 3,422.”

Amesema jumla ya mafundi 845,348 walipata ajira za mikataba na muda kwenye ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo Hospitali za Wilaya, vituo vya afya, zahanati, madarasa, nyumba na majengo maeneo mapya ya utawala, miradi ya barabara chini ya TARURA kwa kutumia Force Account.

Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa katika usimamizi madhubuti wa sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji wa viongozi na watumishi wa umma. “Usimamizi huo, umewezesha viongozi na watendaji wa umma kuwajibika ipasavyo kwa wananchi ambao ndiyo waajiri wao. Sambamba na hilo, nidhamu Serikalini imeongezeka kutokana na Serikali kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wazembe, wadanganyifu na wasio waadilifu.”

Waziri Mkuu amesema mafanikio yote hayo yanachangiwa na uongozi mahiri wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. “Tunapotaja mafanikio haya tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani uongozi wake mahiri na wenye uthubutu ndiyo msingi mkuu wa mafanikio yaliyopatikana.”

“Dhana na falsafa aliyojenga ya Hapa Kazi Tu imesaidia kubadili mtazamo wa Watanzania wengi ambapo sasa tunashuhudia uwajibikaji wa kiwango cha juu wa mtu mmoja mmoja, katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na uzalishaji iwe shambani, ofisini, kiwandani, sokoni na kwingineko badala ya tabia ya awali ya baadhi ya wananchi wachache kupoteza muda mwingi katika shughuli zisizokuwa na tija kwa Taifa.”

(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.