Na Mwandishi
wetu-Dodoma
Serikali
imewaonya baadhi ya watu au makundi ya watu wenye nia isiyo njema kwa
zoezi la sensa ambao wamekuwa wakitoa matangazo ya ajira za Sensa kwa nia
ya kuwatapeli wananchi wanaohitaji kushiriki katika zoezi hilo.
Hayo yalisemwa Mei,
05, 2022 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene wakati akizungumza
na waandishi wa habari kuhusu kuanza kwa mchakato wa Ajira za Makarani na
Wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022 Nchi
nzima.
Pia Mhe. Simbachawene
alisema kwamba mchakato wa ajira za makarani na wasimamizi kuanzia Mei 05 hadi
Mei 19,2022 ambao utahusisha ngazi zote za kiutawala kuhakikisha
wanapatikana makarani na wasimamizi wenye sifa stahiki.
“Kumekuwepo na watu au
makundi ya watu wenye nia isiyo njema kwa zoezi la sensa ambao wamekuwa
wakijaribu kutoa matangazo ya ajira za Sensa kwa nia ya kuwatapeli wananchi
wanaohitaji kushiriki katika zoezi hili na pengine kwa nia ya kuvuruga mchakato
mzima,”alisema Mhe. Simbachawene.
Vilevile Mhe.
Simbachawene aliwahimiza watanzania wote wenye sifa ambao wangependa kuomba
nafasi za ajira hizo kufuata utaratibu uliowekwa kwa ukamilifu ili kuomba
nafasi hizo.
“Kazi za kufanya
pamoja na sifa za mwombaji zimebainishwa katika Tangazo la Ajira za Muda za
Makarani na Wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.Hakutakuwa na
maombi yatakayofanyiwa kazi zaidi ya yale yatakayofuata utaratibu uliowekwa
mtandaoni,”alifafanua Mhe. Simbachawene.
Kuhusu namna ya
kufanya maombi hayo alibainisha kwamba waombaji watatakiwa kutuma maombi yao
kupitia mtandao (online) ambao hautahusisha malipo yoyote kwa mwombaji wa
ajira.
” Mfumo wa kuomba ajira
hizi kupitia mtandao unapatikana kupitia tovuti zifuatazo;www.pmo.go.tz, www.tamisemi.go.tz, www.nbs.go.tz kwa Tanzania Bara na www.ompr.go.tz, https://www.tamisemim.go.tz au www.ocgs.go.tz kwa wale wanaoomba Tanzania Zanzibar,”Alieleza.
Aidha alihitimisha
kuwa mchakato wa kuchambua maombi ya kazi pamoja na usaili utasimamiwa na
Kamati maalum itakayoundwa katika ngazi ya kila Wilaya na usaili utafanyika
katika ngazi ya kata kwa nafasi za makarani na wasimamizi wa maudhui na katika
ngazi ya Wilaya kwa Wasimamizi wa TEHAMA,”alihitimisha Mhe. Simbachawene.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.