Waziri Afya
Mheshimiwa Jenista Mhagama amezindua Usambazaji wa Ripoti ya Utafiti wa
Viashiria na Matokeo ya UKIMWI 2022-2023 Mkoani Ruvuma.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika
Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma alieleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika
juhudi za kudhibiti maambukizi ya UKIMWI nchini Tanzania ambapo imeelezwa kuwa
kiwango cha Maambukizi Mapya kimepungua huku akipongeza juhudu zinazofanywa na
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Nchini
"Kwa mujibu
wa ripoti hiyo, kiwango cha maambukizi ya UKIMWI nchini kimepungua kwa kiasi
kikubwa kutoka asilimia 7 mwaka 2022 hadi asilimia 4.4 mwaka 2023. Aidha,
juhudi za kupunguza maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto zimezaa matunda, ambapo
kiwango cha maambukizi kimepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia
8.1 mwaka 2023," alisema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama
alieleza kuwa mafanikio haya yametokana na juhudi za Serikali kwa kushirikiana
na wadau wa maendeleo, sekta binafsi, na jamii katika kuimarisha programu za
utoaji elimu, upimaji wa hiari, na matumizi ya dawa za kufubaza makali ya
virusi vya UKIMWI (ARVs).
Alisisitiza
umuhimu wa kuendelea na juhudi hizi ili kufikia malengo ya kumaliza maambukizi
mapya ya UKIMWI, hasa kwa watoto, ifikapo mwaka 2030. Vilevile, aliwahimiza
wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na maambukizi na kufuata ushauri
wa kitaalamu.
Aidha alitoa
wito kwa jamii kuunga mkono mikakati ya kitaifa ya kupambana na UKIMWI ili
kuhakikisha maendeleo ya afya ya jamii na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na
Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga, amesema Watanzania wamepiga hatua kubwa
katika mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU)ambapo asilimia
98 ya Watanzania wanaohitaji dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo (ARVs) sasa
wanatumia dawa hizo, hatua ambayo imevuka malengo yaliyowekwa kitaifa na
kimataifa.
Mhe. Ummy
alibainisha kuwa mafanikio haya ni matokeo ya jitihada za serikali chini ya
Mhe. Dkt . Samia Suluhu Hassan, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo
utoaji wa elimu ya afya, upimaji wa hiari, na utoaji wa dawa kwa urahisi katika
vituo vya afya.
Pia ametumia
nafasi hiyo kuhimiza wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na
kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuendelea kutumia dawa kwa walioambukizwa ili
kuboresha maisha yao na kupunguza maambukizi mapya.
Serikali
inaendelea kuweka mikakati imara kuhakikisha kila Mtanzania anayehitaji huduma
za matibabu anazipata kwa wakati.
Maadhimisho ya
Wiki ya UKIMWI Duniani yanaadhimishwa Kitaifa mkoani Ruvuma yenye kauli Mbiu
isemayo "Chagua Njia Sahihi, Tokomeza UKIMWI"
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.