Tuesday, October 13, 2026

OFISI YA WAZIRI MKUU YATOA WITO KWA SEKTA BINAFSI KUWA TAYARI KUKABILIANA NA EL NIÑO.

Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa imetoa wito kwa wakuu wa taasisi binafsi nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika juhudi za kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali baada ya kutokea kwa majanga, hususan athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zilizotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni na Mawasiliano ya Dharura kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kanali Selestine Masalamado wakati akizungumza katika Jukwaa la Majadiliano la Wakuu wa Taasisi Binafsi Tanzania (CEOrt) jijini Dar es Salaam, ambapo amesisitiza umuhimu wa sekta binafsi kuwa sehemu ya maandalizi na utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na maafa nchini.

Kanali Masalamando ameeleza kuwa Serikali imechukua hatua za kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo, kwa kuimarisha uratibu wa shughuli za menejimenti ya maafa, ufuatiliaji wa taarifa za tahadhari na mawasiliano ya dharura, pamoja na kuhamasisha ushirikiano wa wadau katika kupunguza vihatarishi na kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kutokea.

Amesisitiza kuwa, maandalizi dhidi ya maafa yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, mashirika na wananchi ili kuhakikisha taarifa za tahadhari zinawafikia watu kwa wakati na hatua stahiki zinachukuliwa kulinda maisha, mali na shughuli za kiuchumi.

Aidha, amewaalika wakuu wa taasisi binafsi na wadau wengine kuchangia kwa hali na mali katika juhudi za kukabiliana na athari za El Niño, akieleza kuwa ushiriki wa sekta binafsi kupitia rasilimali fedha, vifaa, utaalamu na huduma mbalimbali unaweza kusaidia kuimarisha maandalizi, utoaji wa msaada wa dharura na urejeshaji wa hali katika maeneo yatakayoweza kuathirika.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuzingatia mahitaji ya makundi yote ya wananchi, wakiwemo watu wenye ulemavu, watoto, wazee na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi, ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika maandalizi na utekelezaji wa hatua za kukabiliana na maafa.




EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.