Sunday, September 17, 2017

MARUFUKU VIONGOZI WA SERIKALI KUJIHUSISHA NA BIASHARA YA KOROSHO-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Viongozi wa Serikali wasiokuwa na mashamba ya mikorosho kutojihusisha na biashara ya uuzaji wa zao hilo.

“Kama huna shamba, huwezi kuwa na korosho, unauza umepata wapi. Jukumu lenu ni kufuatilia, kukemea na kuchukua hatua stahiki penye udhaifu na si vinginevyo.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Septemba 17, 2017), wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa korosho uliofanyika mkoani Tanga.

Amesema kama viongozi hao wanahitaji kuuza korosho watumie muda huu ambao Serikali inahamasisha watu wafungue mashamba mapya nao watumie fursa hiyo na kulima.

Amesema ni vema kila mdau akahahakikisha anatimiza wajibu wake ipasavyo kama ni mkulima alime kwa kuzingatia stadi za kilimo na mnunuzi azingatie taratibu zilizopo.

Waziri Mkuu amesema Bodi ya Korosho inatakiwa kuhakikisha inaimarisha zao hilo na kuishauri vizuri Serikali kuhusu namna bora ya kuliendeleza.

Amesema Serikali inaamini kuwa iwapo kila mdau wa zao la korosho atatimiza wajibu wake kikamilifu katika kuliendeleza zao hilo kila upande utanufaika kikamilifu.

Hivyo, ni vizuri kila mdau ajitathmini kama anatimiza wajibu wake kikamilifu, huku akiwaagiza viongozi wa Ushirika waendeshe Ushirika kwa uadilifu mkubwa.

Waziri Mkuu amesema Serikali haitakuwa tayari kusikia mkulima yeyote akilalamika kuhusu malipo iwe kwa kupunjwa, kuchelewa ama kutolipwa.

Amesema katika msimu huu wa biashara ya korosho Serikali haitarajii kusikia mambo ambayo yalikwaza ufanisi katika misimu iliyopita kama wakulima kukatwa unyaufu kwa namna yoyote.

“Sheria ya unyaufu ni miezi sita kutoka korosho inapoanza kuvunwa hadi kuuzwa na korosho haifiki miezi sita, hivyo wakulima hawahusiki unyaufu kwa namna yoyote ile na tusisikie tena.”

Amesema hali hiyo ikitokea hawatasita kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika. “Nawaagiza viongozi wa ngazi zote kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa jambo hili.”

Pia amepiga marufuku Bodi ya Maghala kutoza ushuru wa kuhifadhi mazao kwani hilo si jukumu lao bali ni la mpangaji wa ghala na wao washughulikie utoaji wa leseni tu.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa maghala ya kuhifadhia korosho kutowazuia Viongozi wa Serikali kuyakagua kabla na wakati wa biashara.

Amesema viongozi hao wanatakiwa wasizuiwe kuyakagua maghala hayo hata baada ya minada ili kujiridhisha na mwenendo sahihi wa uhifadhi wa mazao.

Pia ameagiza kukamatwa na kutaifishwa kwa korosho zote zitakazonunuliwa kwa njia ya kangomba. Korosho zitaendelea kuuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi gharani.

Awali, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage amesema korosho ya Tanzania inaongoza kwa ubora duniani, hivyo wazalishaji wahakikisha sifa na ubora wa zao hilo katika soko la dunia haushuki.

Amesema Serikali inaendelea kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika viwanda vya kubangulia korosho ili kuiongezea thamani kabla ya kuisafirisha nje ya nchi.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Mwijage, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Bw. January Makamba.

Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Bi. Anna Abdallah, Wakurugenzi wa Bodi ya Korosho, Wakuu wa mikoa na wilaya zinayolima korosho, Wabunge wanaotoka katika mikoa inayolima korosho, wanunuzi, wasafirishaji na wenye viwanda vya ubanguaji.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.