Saturday, September 2, 2017

WAZIRI MKUU AMUAGIZA RC MORO KUFUATILIA UTENDAJI WA KAMPUNI YA ZHONG FENQ

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt Steven Kebwe na kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa kwenda katika kijiji cha Maseyu kufuatilia utendaji wa kampuni ya Zhong Fenq kama inafuata sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Septemba 2, 2017), wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa kiwanda cha Philp Morris kinachotengeneza sigara aina ya Marlboro akiwa  katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya viwanda mkoani Morogoro.

Agizo hilo limefuatia malalamiko ya mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki Mheshimiwa Omary Mgumba kuwa wawekezaji hao kutoka China wanaendesha shughuli za uchimbaji wa mabo katika kijiji cha Maseyu wilayani Morogoro bila ya kuwa na kibali.

Mheshimiwa mgumba amesema tangu mwaka 2011 wawekezaji hao wameendesha shughuli zao bila  kulipa kodi za Serikali na tozo za Halmashauri, hivyo kuikosesha Serikali mapato.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kijiji cha Maseyu kuna Wachina wa kampini ya Zhong Fenq wanachimba mabo na hawana kibali na hakuna kodi yoyote wanayolipa Serikalini tangu mwaka 2010 walipoanza uzalishaji.”

Mbunge huyo ambaye machimbo hayo yako jimboni kwake aliongeza kwamba licha ya uongozi wa mkoa kwenda katika eneo hilo na kuizuia kampuni kuendelea na uchimbaji hadi itakapopata vibali walikaidi na kuendelea na shughuli.

Waziri Mkuu amesema hakuna muwekezaji anayeruhusiwa kufanya kazi bila ya kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi. Hivyo ameagiza kesho Mkuu wa Mkoa afuatilie Wachina hao na kuona namna gani wamezingatia sheria za nchi.

Amesema iwapo watabaini kwamba wawekezaji hao  hawajafuata sheria, kanuni na taratibu hatua zichukuliwe dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa katika eneo hilo chini ya ulinzi na kuwasiliana na ubalozi wa China  Nchini.

Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa watu wote wenye nia ya kutaka kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini Tanzania kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na taratibu za uwekezaji.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema ni faraja kuona kiwanda cha Philp Morris kikiwa kimekamilika tayari kwa kuanza uzalishaji wa sigara aina ya Marlboro hivyo kuwezesha wakulima wa tumbaku nchini kuwa na soko la uhakika.

Amesema miaka ya nyuma uzalishaji wa tumbaku ulipungua nchini kutokana na wakulima kukata taama baada ya kukosa soko la uhakika pamoja na kuchoshwa na ubadhilifu wa mali za ushirika uliokuwa ukifanywa na viongozi wa vyama vya ushirika wa tumbaku.

Pia Waziri Mkuu alitembelea ujenzi wa kiwanda cha sukari kilichopo katika Gereza la Mbigiri wilayani Kilosa na kukagua shamba la miwa lenye ukubwa wa hekta 4,800 ambapo hekta 320 zimelimwa na kati yake hekta 125 tayari zimepandwa miwa na imeshaota.

Kiwanda hicho kinajengwa kwa ushirikiano wa Jeshi la Magereza na mifuko ya hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF kupitia mradi wa Mkulazi ambao unatarajia kuzalisha tani 250,000 za sukari kwa mwaka kati yake tani 50,000 zitazalishwa katika kiwanda cha Mbigiri na tani 200,000 katika kiwanda cha Ngerengere.

Amesema uwepo wa viwanda nchini utawezesha watanzania kulima kilimo chenye tija kwa kuwa watauza mazao yao viwandani na mmoja atashiriki kulima zao ambalo ataliuza katika kiwanda cha jirani.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.