Tuesday, October 24, 2017

WATUMISHI WA OFISI YA WAZIRI MKUU WAJENGEWA UWEZO KUKABILI MAAFA

Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wameshiriki Warsha ya kujengewa uwezo kuhusu kugharamia maafa na matumizi ya Bima za majanga ili kutumia fursa zilizopo za kukabili maafa pindi yanapotokea kwa kushirikisha wadau mbalimbali  ikiwemo Taasisi zilizopo chini ya Umoja wa Afrika .

Akizungumza wakati wa Warsha hiyo iliyofanyika Oktoba 24, 2017 Mjini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Bunge, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Bw. Issa Nchasi alisema kuwa warsha hiyo inalenga kutoa uelewa kuhusu utaratibu utaotumiwa na African Risk Capacity (ARC) ambayo ni Taasisi chini ya Umoja wa Afrika.

“Serikali imekuwa ikifanya kazi ya kuboresha mazingira ili kujenga uwezo wa kukabili madhara yatokanayo na maafa nchini” Alisisitiza Nchasi

Akifafanua amesema kuwa, warsha hiyo itasaidia watumishi wa Idara ya Uratibu wa Maafa kuwa na uwezo katika Menejimenti ya Maafa hali itayorahisisha Kujikinga, kukabili na kurejesha hali.

Washa hiyo ya siku moja imelenga kuwajengea uelewa Watumishi wa Ofisi hiyo kuhusu utaratibu unaotumiwa na Taasisi yaAfrica Risk Capacity katika kuhudumia na kugharamia maafa na Bima za majanga.

Kuwawezesha Serikali kutambua maeneo ya ushirikianao katika huduma na kugharimia maafa na Bima za majanga.

Kwa upande wake Mkuu wa Huduma kwa Serikali kwa nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kutoka Shirika la “Africa Risk Capacity” bi. Lucy Nyirenda amesema kuwa mpango huo uko chini ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) na takribani nchi 9 zimeshajiunga katika mfumo wa Bima za majanga.

“Takribani nchi 32 zimeshajengwewa uwezo kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya majanga ili kuimarusha uwezo wa kuyakabili pale yanapotokea kwa kushirikiana na wadau.” Alisisitiza Lucy

Akifafanua Lucy amesema kuwa, ni vyema nchi za Afrika zikaungana ili kuweza kuzuia majanga katika Bara la Afrika kwa kushirikishana mbinu mbalimbali zikiwemo fursa zinazoweza kusaidia kukabiliana na majanga hayo .

Warsha hiyo ya siku moja iliyoandaliwa na Taasisi ya Africa Risk Capacity (ARC ) iliyopo chini ya Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu  imewashirikisha  Watumishi kutoka  Wizara za kisekta na Idara zinazojitegemea Takribani 42.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.