Sunday, October 1, 2017

VIONGOZI WA DINI WAWAPINGE WANAOTAKA KUVURUGA AMANI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba Viongozi wa Jumuiya na Taasisi zote za kidini nchini wahakikishe wanawapiga vita watu wote wanaopanga na kutaka kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini kwa sababu watakwamisha maenendeleo.

Amesema Serikali inaelewa kwamba dini ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya maendeleo ya ustaarabu wa mwanadamu kwani inatoa elimu ya maadili mema yenye kuwafanya waumini waepukane na maovu mbalimbali.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumapili Oktoba 01, 2017) wakati akifungua mkutano Mkuu wa mwaka wa 48 wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya uliofanyika katika eneo la Kitonga kata ya Msongola wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Amesema kila Mtanzania anatakiwa ahakikishe anadhibiti matukio yote yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kwa kutoa taarifa katika mamlaka husika.”Tanzania ni nchi salama na yenye utulivu, hivyo ni lazima wote tushirikiane kuitunza.”

 “Napenda niwahakikishieni kuwa Serikali inaunga mkono juhudi za Jumuiya za kidini katika kupiga vita maovu ya kila aina; mathalan utumiaji wa dawa za kulevya, wizi, rushwa, uzinzi ambao husababisha madhara mengi ukiwemo ugonjwa wa UKIMWI.”

Amesema iwapo dini zetu zitatumika vizuri tutaweza kwa haraka sana kutekeleza agizo la Rais Dkt. John Magufuli  la 'Hapa kazi tu' kwani kila mtu ataepuka uzembe na kuwajibika ipasavyo.

Waziri Mkuu amesema ana imani kwamba jumuiya hiyo kama zilivyo taasisi zingine za kidini itaendeleza kazi kubwa ya kupambana na maovu katika jamii yetu kwa kuwapatia waumini wao na wananchi kwa ujumla elimu na maarifa ya kuboresha tabia zao na maadili yao kiroho.

Amesema amani na utulivu uliopo nchini unatokana na mambo mengi ikiwemo na wananchi kupata ustawi, kuweza kufanya shughuli zao vizuri na kuwa na imani na Serikali yao, ambayo imejiwekea mikakati ya kuhakikisha wananchi hususan wanyonge wanapata faraja ndani ya nchi yao.

Waziri Mkuu amesema mambo yameweza kupatikana baada ya Serikali kupambana na rushwa na ufisadi pamoja na kuimarisha maadili ya watumishi wa umma, ambayo vimekuwa ni vyanzo vya kupotea kwa amani na utulivu katika baadhi ya nchi.
“Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kupambana na ufisadi, kupitia mikataba mibovu na kuimarisha maadili ili kujenga imani kwa wananchi, kuondoa migongano na tofauti ya kipato, kuwa na matumizi mazuri ya rasilimali za umma, kuleta tija kwa kuongeza thamani ya huduma na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.”
Awali, Amir na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya Tanzania, Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry  amesema Jumuiya hiyo imekuwa ikifanya mikutano kila mwaka kwa lengo la kukumbushana misingi sahihi ya dini tukufu ya kiislam pamoja na kukuza undugu wao.
Sheikh Chaudhry amesema mkutano wa mwaka huu umejumisha watu zaidi ya 4,000 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wageni kutoka nchi za Uingereza, Canada, Rwanda, Uganda, Ujerumani, Kenya, Burundi, Malawi na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Amesema Jumuiya hiyo mbali na masuala ya kidini pia inatoa huduma mbalimbali za kijamii kama elimu, maji na afya kwenye mikoa tofauti tofauti nchini.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.