WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waishio Canada wadumishe mshikamano wao na wawe na uzalendo kwa Taifa lao.
Ametoa wito huo jana (Jumanne, Oktoba 31, 2017)
wakati akizungumza na Watanzania waishio Toronto, Canada.
Waziri Mkuu ambaye yuko Canada kwa ziara ya
kikazi, alisema kila Mtanzania anapaswa ahubiri utaifa wake. “Tembea huku
ukiringia nchi yako, wakati wote ringia nchi yako, unapotakiwa kuisemea nchi
yako, isemee vizuri kama ambavyo wengine wanasemea vizuri nchi zao licha ya
matatizo waliyonayo.”
Aliwataka wakumbuke kuweka akiba na wanapopata
fursa watume fedha zao nyumbani ili zisaidie kuleta maendeleo. “Ukipata kitu kidogo,
rusha nyumbani; ukipata mtu anayeweza kuleta tija, mlete nyumbani, nasi
tutawapokea wewe na yeye,” alisisitiza.
“Tunawasisitiza muitangaze nchi yetu kwa mataifa
mengine ili nao waone Tanzania ni mahali pa fursa, na akitaka kuwekeza ajue
kuwa anawekeza mahali ambapo ni salama,” alisema.
Alisema Serikali inasisitiza wananchi waishio nje
ya nchi, wawe wazalendo na washirikiane kuhakikisha wanazitumia vizuri fursa za
kimaendeleo kwa manufaa ya nchi yao.
Awali, Balozi wa Tanzania nchini Canada, Mhe. Jack Nzoka, alitumia fursa hiyo
kuwasihi Watanzania waishio nchini humo wazingatie sheria za nchi hiyo.
“Wote sisi tunawatambua kama mabalozi katika nafasi
zenu hapa Canada. Tunawashauri muwe raia wema, na muishi kwa kufuata sheria na
taratibu za nchi hii na msisahau mlipotoka, kwani hakuna mahali pazuri kama
nyumbani,” alisisitiza.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.