WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku tabia ya baadhi ya viongozi katika maeneo mbalimbali nchini kuwakamata na kuwaweka ndani watumishi wakiwemo wauguzi bila ya kufuata taratibu.
Pia amewataka wauguzi nchini kufanya kazi kwa weledi, uaminifu pamoja na kufuata maadili ya taaluma yao kwa kuwa maisha ya wagonjwa yako chini yao.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Oktoba 04, 2017) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 45 wa Chama cha Wauguzi Tanzania, mkoani Lindi.
“Naagiza viongozi wote kufuata na kuzingatia sheria. Kama kuna makosa ya kitaaluma, Mabaraza husika yashughulikie jambo hilo na ni marufuku kuwaweka ndani watumishi kwa tuhuma za kitaaluma.”
Amesema kwamba katika sekta ya afya bila wauguzi ambao ni kundi kubwa kati ya Wanataaluma wa Afya, Serikali haitaweza kutekeleza ipasavyo mikakati mbalimbali iliyopangwa kwa ajili ya kuboresha sekta hiyo.
Katia hatua nyingine Waziri Mkuu amewaasa wauguzi wote nchini kuhakikisha wanazingatia kiapo cha maadili ya kazi yao na kwamba Serikali haitamvumilia yeyote atakae bainika kwenda kinyume.
“Nanyi Wauguzi mnao wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia kiapo na miiko ya taaluma yenu. Tunazo taarifa kuhusu baadhi ya Wauguzi kutoa lugha chafu kwa wagonjwa, kuomba rushwa na wengine kujihusisha na vitendo vya wizi wa dawa.”
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha afya za Watanzania wote zinaimarika ili kuendana na kasi ya utendaji kazi wa Serikali ya kuinua uchumi na kufikia wa kiwango cha kati, hivyo ni lazima watoe huduma bora kwa wananchi.
Pia amewaomba waunge mkono kwa nguvu zote jitihada za Serikali katika kuhakikisha miundombinu na vifaa vyote havihujumiwi na watu wachache ili viwe msaada mkubwa hususani kwa akina mama wajawazito ili wajifungue salama.
Akizungumzia kuhusu upungufu wa wauguzi nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo Wauguzi na Wakunga na kuwapanga katika maeneo yenye upungufu zaidi.
Awali, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Khamis Kigwangalla alisema baadhi ya viongozi katika maeneo mbalimbali wamekuwa wakiwakamata na kuwachukulia hatua watumishi wa Sekta ya Afya bila ya kufuata taratibu, jambo ambalo si sahihi.
Mkutano huo umehudhuriwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Kigwangalla, Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania Bw. Paul Magesa, Mbunge wa Lindi Mjini Bw. Hassan Kaunje, Mbunge wa Kuteuliwa Mama Salma Kikwete(MB) Viti maalum.
Wengine ni Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Gustav Moyo, Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Bw. Stewart Mbelwa.
Wengine ni Mbunge wa Viti Maalumu, Hamida Abdallah, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Uuguzi Bw. Ndementria Vermund, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt. Obadia Nyongolena wawakilishi wa wauguzi kutoka mikoa yote nchini.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.