Saturday, August 8, 2020

WAZIRI MKUU ATOA WIKI MOJA KWA WIZARA YA ELIMU

 

*Ni kuhusu ucheleweshwaji wa michango ya wanafunzi NHIF

 

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa muda wa wiki moja kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kukutana na Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini ili kubaini vyuo ambavyo vimeshindwa kuwasilisha michango ya wanafunzi katika Mfuko wa Taifa Bima ya Afya (NHIF) licha ya wanafunzi kulipa fedha hizo.

 

“Katibu Mkuu Wizara ya Elimu kashughulikie jambo hili tujue mifumo wanayotumia, pia nataka kujua ni wanafunzi wangapi ambao wamelipa na hawajapewa vitambulisho na kwa nini na nani amesababisha haya na hatua alizochukuliwa. Taarifa hiyo nataka niipate tarehe 16 mwezi huu, wiki moja inakutosha.”

 

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Agosti 9, 2020) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza kwa mwaka 2019/2020 wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi ya Elimu ya Juu Tanzania(TAHLISO) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

 

Ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi hao yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa TAHLISO, Bw. Peter Niboye ambaye alisema kwamba kumekuwepo na ucheleweshaji wa vitambulisho vya bima ya afya unaotokana na baadhi ya vyuo kuchelewa kufikisha fedha NHIF.

 

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuziagiza Menejimenti zote za vyuo vikuu nchini ziendelee kushirikiana kwa karibu na Serikali za Wanafunzi kwenye vyuo vyao ili waweze kushughulikia changamoto za wanafunzi kwa wakati.

 

Akizungumzia kuhusu wabunifu pamoja na wanafunzi bora, Waziri Mkuu amesema “Naiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia isimamie utambuzi wa masuala mbalimbali ya kitaaluma iwe ni kwenye teknolojia, afya na hawa wabunifu watambuliwe na waendelezwe. Tuwe na benki ya wabunifu waliobuni kazi ambazo zinaweza kusaidia jamii.”

 

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa taarifa ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia inaeleza kuwa tangu kufunguliwa kwa vyuo nchini tarehe 01 Juni, 2020 wanafunzi wote walioripoti wapo salama na wanaendelea vema na masomo yao.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAHLISO, Bw. Niboye  amesema wanajivunia kufanya kazi kwa karibu na Bodi ya Mikopo na Mfuko wa Bima ya Afya na imechangia kutokuwepo kwa migomo ya wanafunzi.

Akitoa tamko la jumuia hiyo katika kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu, amesema TAHLISO inamuunga mkono mlezi wao na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika uchaguzi huo na watahakikisha  anashinda kwa kishindo.

Mwenyekiti huyo amesema TAHLISO imefanya uamuzi huo baada ya kuridhishwa na utendajikazi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama ya elimu, umeme, maji, miundombinu na afya.

 

OWM


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.