Friday, August 28, 2020

NAIBU KATIBU MKUU TAMISEMI AKUNWA NA MAFUNZO KAZINI YA OFISI YA WAZIRI MKUU

 

Ofisi ya Waziri Mkuu imefanya mafunzo ya kujenga uwezo wa kutekeleza majukumu waliyokasimiwa kwa maafisa 36 kutoka idara na vitengo vya ofisi hiyo. Mafunzo hayo ya wiki moja yamefanyika kuanzia tarehe 24 hadi 28 Agosti 2020, Jijini Dodoma, ambapo Wakala wa Serikali ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) waliendesha mafunzo hayo kwa ufadhili wa Shirika la Chakula Duniani. 


Lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kujenga uwezo kwa maafisa wake katika maeneo ya Uchambuzi wa Sera, Ufuatiliaji na Tathmini ya Sera na Uandishi wa taarifa. Mafunzo hayo pia yamewezesha maafisa hao kuongeza umahiri wa utekelezaji majukumu waliyokasimiwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara 52, ambapo jukumu la msingi la Ofisi hiyo ni kuratibu na kusimamia shughuli za Serikali katika sekta zote na Bungeni pamoja na majukumu mengine yaliyoainishwa kwenye Tangazo la Serikali Na. 144 Aprili 2016, lililofanyiwa mabadiliko tarehe 7 Oktoba 2017.


Akiongea wakati akifunga rasmi mafunzo hayo, leo tarehe 28 Agosti  jijini Dodoma,  Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Gerald Mweli hakusita kueleza furaha yake juu ya utaratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendesha mafunzo kwa watumishi yanayolenga kujenga uwezo wa kutekeleza majukumu waliyokasimiwa.


“Nimevutiwa sana na mbinu zilizotumika katika ufundishaji wa mafunzo haya. Nimeambiwa katika kuhakikisha mnapata mbinu na umahiri kwenye Tathmini na Ufuatiliaji wa Sera, mmepitia Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa masuala ya Lishe. Naelewa Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo mratibu wa mpango huu na sisi TAMISEMI tunatekeleza. Nakusudia na mimi Kufanya mafunzo kama haya kwa watumishi wa wizara yangu” amesisitiza Mweli.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko amelishukuru Shirika la Chakula Duniani kwa ufadhili wa mafunzo hayo, ambapo   matokeo ya mafunzo hayo  ni Ofisi hiyo kuwa na mfumo bora wa uratibu wa shughuli za serikali kutokana na mamlaka iliyonayo kikatiba ya kuratibu shughuli zote za Serikali pamoja na masuala mtambuka ikiwemo masuala ya lishe.


“Mafunzo haya yatakuwa ni mwendelezo kwa   maafisa wote na menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, lengo ni kuongeza umahiri kwa uchambuzi bora wa sera, ufuatiliaji na tathmini ya sera pamoja na kuwa na  mfumo bora wa mawasiliano ya utekelezaji wa majukumu kwa idara zote ndani ya Ofisi, pia na mfumo bora wa uratibu wa shughuli za serikali” amesisitiza Mwaluko.


Awali akiongea kabla ya kufungwa kwa mafunzo hayo, Kaimu mkurugenzi mkuu wa Wakala ya Mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA), Dickson Mwanyika amefafanua kuwa mafunzo hayo yaliyoendeshwa kwa utaratibu wa mijadala washiriki walipata fursa ya kufahamu mbinu za kimkakati za uchambuzi wa Sera na kanuni za uratibu wa Sera, njia za kufanya ufutiliaji na tathmini, vigezo vya kuzingatia katika kufanya tathmini na ufuatiliaji pamoja na  namna ya kuandika taarifa na muundo wa taarifa.


Wakiongea kwa nyakati tofauti kwenye mafunzo hayo, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, Frank Mwega na Elilanga Kaaya  wamebainisha kuwa mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa kwa washiriki katika kuwajengea uwezo. Aidha, wameshauri uendelevu wa mafunzo ya namna hiyo yenye kuwajengea uwezo watumishi kwenye maeneo ya utendaji.

MWISHO.


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko akisisitiza kuwa Ofisi hiyo itaendelea kutoa mafunzo ya kujenga uwezo kwa maafisa wa ofisi hiyo, lengo ikiwa ni kutekeleza majukumu waliyokasimiwa kwa ufanisi na weledi. Mafunzo hayo ya siku tano, yameendeshwa na Wakala ya Mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA) na kufungwa leo jijini Dodoma tarehe 28 Agosti, 2020.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko, akimshukuru Afisa Lishe kutoka Shirika la Chakula Duniani, Neema Shosho, kwa ufadhali wa mafunzo ya kujenga uwezo kwa maafisa wa ofisi hiyo, lengo ikiwa ni kutekeleza majukumu waliyokasimiwa. Mafunzo hayo ya siku tano, yameendeshwa na Wakala ya Mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA) na kufungwa leo jijini Dodoma tarehe 28 Agosti, 2020.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Gerald Mweli akisisitiza umuhimu wa ubora wa Uratibu wa shughuli za serikali wakati akifunga rasmi mafunzo ya kujenga uwezo kwa maafisa wa ofisi hiyo leo jijini Dodoma tarehe 28 Agosti  2020, kushoto kwake ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko na kulia ni  Kaimu mkurugenzi mkuu  wa Wakala ya Mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA) Dickson Mwanyika,  


Baadhi Maafisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Gerald Mweli wakati akifunga rasmi mafunzo ya kujenga uwezo kwa maafisa wa ofisi hiyo leo jijini Dodoma tarehe 28 Agosti  2020, Mafunzo hayo ya siku tano, yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na kuendeshwa na Wakala ya Mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA).

Mchumi Mwandamizi Ofisi ya Waziri Mkuu. Frank Mwenga, akieleza umuhimu wa  mafunzo ya kujenga uwezo kwa maafisa wa ofisi hiyo wakati wa kufunga mafunzo hayo  leo jijini Dodoma tarehe 28 Agosti  2020, Mafunzo hayo ya siku tano, yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na kuendeshwa na Wakala ya Mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA).

Mchumi Ofisi ya Waziri Mkuu. Elilanga Kaaya, akieleza umuhimu wa  mafunzo ya kujenga uwezo kwa maafisa wa ofisi hiyo wakati wa kufunga mafunzo hayo  leo jijini Dodoma tarehe 28 Agosti  2020, Mafunzo hayo ya siku tano, yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na kuendeshwa na Wakala ya Mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA).

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu Gerald Mweli,   akimkabidhi cheti Afisa Habari Mwandamizi Ofisi ya Waziri Mkuu Isabela Katondo,  baada ya kuhitimu mafunzo ya Uchambuzi wa Takwimu, Ufuatiliaji  na Tathmini ya Sera na Uandishi wa Taarifa, leo jijini Dodoma tarehe 28 Agosti  2020, Mafunzo hayo ya siku tano, yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na kuendeshwa na Wakala ya Mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA).

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu Gerald Mweli,   akimkabidhi cheti Afisa Utumishi Ofisi ya Waziri Mkuu Herman Chando, baada ya kuhitimu mafunzo ya Uchambuzi wa Takwimu, Ufuatiliaji  na Tathmini ya Sera na Uandishi wa Taarifa, leo jijini Dodoma tarehe 28 Agosti  2020, Mafunzo hayo ya siku tano, yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na kuendeshwa na Wakala ya Mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA).

Washiriki wa mafunzo ya Uchambuzi wa Takwimu, Ufuatiliaji  na Tathmini ya Sera na Uandishi wa Taarifa wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu,  Gerald Mweli (mwenye tai),  kulia kwake ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko, leo jijini Dodoma tarehe 28 Agosti  2020, Mafunzo hayo ya siku tano, yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na kuendeshwa na Wakala ya Mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA).



EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.