Monday, March 29, 2021

“Serikali kuendelea kudhibiti Dawa za Kulevya na UKIMWI nchini” Mhagama

 



Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, imeihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, kuwa imeweka mikakati ya Kudhibiti UKIMWI na Dawa za kulevya ili kuimarisha ustawi wa wananchi nchini.


Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama,tarehe  29 Machi 2021,  Jijini Dodoma, wakati akiwasilisha kwa kamati hiyo, taarifa ya Utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2020/2021 na makadirio ya  Bajeti ya mwaka 2021/2022  ya  Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya.


“Kazi hii ya kuwaokoa vijana na watanzania kwenye UKIMWI na dawa za kulevya tumeshafanya vizuri. Tumewasaidia waraibu 10,565 ambao wanapatiwa matibabu katika kliniki za Methadone nchini. Tumeandaa mkakati wa kuhakikisha kuwa waraibu hao hawarejei tena katika matumizi ya dawa za kulevya na tunafanya hivyo kupitia Idara ya Kazi na Ajira.” Amesisitiza Mhe. Mhagama.


Mhe. Mhagama amefafanua kuwa, Serikali imetengeneza mtandao wa Asasi ambapo hadi sasa kuna takribani Asasi 52 nchi nzima ambazo zinashirikiana na Serikali Katika shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya. Aidha, ameongeza kuwa tayari mwongozo wa namna Kamati za UKIMWI za Halmashauri zitakavyoratibu shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya na  Asasi zilizopo kwenye Halmashauri husika umeshaandaliwa.


Amesisitiza kuwa, serikali inaendelea kushirikiana na nchi nyingine kwenye kudhibiti na kupambana na Dawa za kulenya kwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa Katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, amesema Operesheni za Kupambana na biashara ya Dawa za Kulevya zimefanyika kwa umakini, ambapo Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Februari 2021 wamekamatwa  jumla ya watuhumiwa 5,374 wakiwemo wanaume 4,917 na wanawake 457.

 

Kadhalika, amesema Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetoa mafunzo kwa waratibu wa UKIMWI kwa Halmashauri 185 juu ya ukusanyaji, utunzaji na matumizi ya takwimu sizizo za kitabibu TOMSHA. Pia ameeleza kuwa   ufuatiliaji na usimamizi na Ukaguzi wa takwimu za kila robo mwaka umefanyika katika Mikoa yote 26.


“Hadi Desemba mwaka jana, utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kimataifa wa Kudhibiti na Kupambana na UKIMWI wa 90-90-90, ulionesha mafanikio kwenye  WAVIU milioni 1.4, sawa na asilimia 83 ya WAVIU wote walikuwa wanatambua hali zao za  VVU. Tulifanikiwa WAVIU milioni 1.36 sawa na asilimia 98 walikuwa kwenye tiba na matunzo ya ARV na jambo la faraja ni kuwa asilimia 92 ya waliokuwa kwenye tiba ya ARV walikuwa na kiwango cha chini cha VVU mwilini.” Amesema Mhe. Mhagama


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, Mhe. Fatma Tawfiq amebainisha kuwa kamati yake imeridhika na jinsi serikali ilivyozingatia ushauri  wa kamati hiyo uliolenga kuimarisha jitihada za kudhibiti dawa za kulevya na UKIMWI nchini. Amefafanua kuwa matatizo ya dawa za kulevya na UKIMWI ni mtambuka na yanaathiri sekta mbalimbali hivyo serikali haina budi kuendelea kushirikana na wadau katika kuhakikisha wanaimarisha ustawi wa wananchi.


Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Ngeriananga, Katibu Mkuu (Bunge na Waziri Mkuu), Tixon Nzunda, Katibu Mkuu (Sera na Uratibu), Dorothy Mwaluko, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya.   James Kaji pamoja na Wakurugenzi na Wataalam wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

 

Dira ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ni “Kujenga jamii ya Watanzania isiyotumia dawa za kulevya na kutoshiriki katika biashara ya dawa hizo”. Aidha, Dira ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania ni: “Kuwa Taasisi yenye hadhi inayoongoza Tanzania katika kuelekea kizazi kisicho na maambukizi ya VVU na UKIMWI”.

MWISHO.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, Mhe. Fatma Tawfiq akieleza umuhimu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kushirikiana na wadau katika kuimarisha ustawi wa watanzania wakati kamati hiyo walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini Dodoma, tarehe 29 Machi 2021.


Makatibu wakuu na wakuu wa Taasisi za Ofisi ya Waziri Mkuu, wakifuatilia kikao cha Ofisi hiyo na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini Dodoma, tarehe 29 Machi 2021.


Baadhi ya Wakurugenzi na wataalamu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia kikao cha Ofisi hiyo na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini Dodoma, tarehe 29 Machi 2021.


Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko, akieleza mikakati waliyoipanga katika kudhibiti UKIMWI nchini wakati wa kikao cha Ofisi ya Waziri Mkuu na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini Dodoma, tarehe 29 Machi 2021.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiwaongoza Manaibu Mawaziri, Makatibu wakuu, Wakuu wa Taasisi, Wakurugenzi na Wataalamu wa Ofisi hiyo , wakati wa kikao cha Ofisi hiyo na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini Dodoma tarehe 29 Machi 2021.



EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.