Tuesday, May 19, 2020

WAZIRI KAIRUKI AHIMIZA WAWEKEZAJI KUONGEZA UZALISHAJI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki amehimiza wawekezaji katika sekta mbalimbali kuongeza uzalishaji zaidi hususani katika kipindi hiki ambacho mahitaji ya bidhaa mbalimbali yanazidi kukua katika soko la ndani. Ameyasema hayo leo tarehe 18 Mei 2020 alipotembelea Kiwanda cha OK Plast Ltd kilichopo Vingunguti, Dar Es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine amepata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazoendelea kiwandani hapo na kusikiliza changamoto zao.

Kiwanda hicho cha OK Plast Ltd ni moja ya viwanda vichache vinavyochakata skrepaza shaba na kuzalisha bidhaa za mwisho kama vile nyaya za aina mbalimbali za umeme pamoja na malighafi za viwanda vingine kama vile ingoti za betri, kathodi na rodi za shaba.

Wakati akimpatia maelezo ya uwekezaji wa kiwanda hicho, Meneja wa Kiwanda Bw. Fadl Ghaddar ameeleza kuwa hadi sasa wameshawekeza takribani Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kuendeleza mradi huo ambapo amebainisha kuwa tangu waliposajili mradi huo Mwaka 2005 umekuwa ukijiendesha kwa mafanikio ikiwemo kuweza kuzalisha bidhaa zenye uhakika wa soko la hapa nchini huku wakiendelea kupokea oda za bidhaa kutoka nchi jirani hususani kutoka Kenya.

Meneja huyo aliongeza kuwa hadi sasa wamefanikiwa kuajiri jumla ya wafanyakazi 600 ambapo kati yao 595 ni Watanzania na 5 tu ndiyo raia wa kigeni. Aidha, alifafanua kuwa wanajivunia kuweza kuendelea kutoa mafunzo ya ujuzi wa kushughulikia aina mbalimbali za metali kwa waajiriwa wao na hata wale wanaoamua kuacha kazi huondoka wakiwa na ujuzi wa kuweza kuanzisha karakana zao na kujitegemea. Kiwanda hicho kinalipa Kodi taribani Shilingi bilioni 2 kwa mwaka, alieleza. 

Hata hivyo, Bw. Ghaddar alibainisha kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni uhaba wa malighafi ya skrepa ya shaba jambo ambalo limepelekea Kiwanda kuzalisha chini ya uwezo wake ambapo kwa sasa huzalisha takriban tani 150 za bidhaa mbalimbali za shaba kwa mwezi huku uwezo wa kiwanda kuzalisha ukiwa tani zaidiya 500 kwa mwezi. Alieleza kuwa changamoto hiyo inatokana na ukweli kwamba licha ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya BICO ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuonesha kuwa kuna upatikanaji wa kutosha wa skrepa ya shaba hapa nchini kutosheleza mahitaji ya viwanda vya kuchakata malighafi hiyo, kuendelea kuuzwa nje ya nchi kwa skrepa kumesababisha uhaba wa malighafi hiyo kwa viwanda vinavyoihitaji hapa nchini. Hivyo, alishauri na kutoa ombi kwa Serikali kupitia kwa Waziri wa Uwekezaji kuliangalia suala hilo ili kulinda viwanda vya ndani kwa kuvihakikishia upatikanaji wa malighafi ya kutosha ili kuepuka kutumia fedha za kigeni kuagiza malighafi hiyo nje ya nchi.

Kwa upande wake Waziri Kairuki aliupongeza uongozi wa Kiwanda hicho kwa kuhakikisha uzalishaji kiwandani hapo unaendelea kama kawaida licha ya changamoto ambazo wanakabiliana nazo. Alipongeza pia hatua ya Kiwanda hicho kuitikia wito wa Serikali kwa wawekezaji wa kuajiri Watanzania kwa kazi ambazo zinaweza kufanywa na wazawa pamoja na kuweka program nzuri kwa wataalamu wa kigeni kutoa mafunzo ya ujuzi mbalimbali kwa wafanyakazi wa kitanzania. Alitumia pia fursa hiyo kuwapongeza kwa kulipa kodi za Serikali kwa mujibu wa Sheria na kuwataka wawekezaji wengine pia kuiga mfano huo ikiwa ni sehemu ya wajibu wao kwa Serikali.

Aidha alitoa wito kwa wawekezaji waliojisajili Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)  kuendelea kuwasilisha taarifa za maendeleo ya miradi yao kila baada ya miezi 6 kama ilivyoainishwa kwenye kanuni za usajili TIC ili Kituo kiweze kufahamu na kufuatilia kwa karibu changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kwa wakati.

Waziri Kairuki anatarajia kuendelea na ziara ya kutembelea miradi ya uwekezaji katika sekta mbalimbali katika Mikoa ya Dodoma na Singida kwa lengo la kusikiliza chanmagamoto zao  na kuhamasisha uzalishaji hususani wa bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa hapa nchini badala ya kuagizwa kutoka nje ya Nchi.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.