Wednesday, May 6, 2020

WADAU WACHANGIA SH. MILIONI 150 KUKABILIANA NA CORONA



WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amepokea msaada wa hundi tatu zenye thamani ya sh. milioni 150 zilizotolewa na kampuni tatu zinazozalisha nguzo za umeme nchini kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (COVID- 19).

Waziri amepokea michango hiyo kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo tarehe 4 Mei, 2020 katika Ofisi ya Waziri Mkuu Mlimwa, Jijini Dodoma. Michango hiyo imetolewa na kampuni Mufindi Woodpoles Plant and Timber Ltd, Qwihaya General Enterprises Co Ltd na Poles (T) Ltd ambapo kila kampuni imetoa sh. milioni 50.

Akizungumza wakati wa kupokea michango hiyo Waziri Mhagama aliwapongeza viongozi wa kampuni hizo kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha inapambana na janga la ugonjwa wa COVID-19.

“Nawashukuru sana kwa niaba ya Serikali na hii inaonesha uzalendo, utayari na kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa ni sehemu ya mapambano hayo kwa vitendo,”alieleza Waziri Mhagama.

Pia, Waziri Mhagama alitumia fursa hiyo kuwasihi wakandarasi wengine pamoja na Watanzania kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kujitolea kwa hali na mali ili kuwezesha katika kukabiliana na janga hilo.

“Tunatoa wito kwa Watanzania wote kuona umuhimu na kuguswa na janga hili kwa kuchangia kwa kadiri inavyofaa ili kuendeleza uzalendo kwa hali ya kujali na kuonesha utayari ili kudumisha hali ya utamaduni uliopo tangu awali wa umoja na mshikamano ,”alisema Waziri Mhagama.

Aliwahakikishia wadau hao kuwa, michango hiyo itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwaeleza kuwa imefika katika eneo salama.

Awali, Waziri wa Nishati Dkt. Medadi Kalemani aliwapongeza viongozi wa kampuni hizo kwa michanga waliyoitoa kwa Serikali ambayo inakwenda kuongeza nguvu katika kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19.

“Niwapongeze wakandarasi hawa kwa kuonesha nia ya kushiriki katika mapambano haya na wito wangu kila anayeguswa na janga hili ni faraja kubwa mnayoitoa kwa Serikalini katika kuhudumia na kusaidia katika kipindi hiki. Pia nawaomba wakandarasi wengine waige, ”alisema Dkt. Kalemani.  



EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.