KAMPUNI YA
EVERWELL CABLE AND ENGINEERING CO. LTD YACHANGIA
SH. MILIONI 100 KUKABILIANA NA CORONA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana, na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista
Mhagama (Mb), amepokea msaada wa hundi yenye thamani ya sh. milioni 100 iliyotolewa
na kampuni ya Everwell Cable and Engineering Co. Ltd, inayojishughulisha na
uzalishaji wa nyaya za kusafirisha umeme kwenye miradi mbalimbali ya umeme hapa
nchini, kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu
inayosababishwa na virusi vya Corona (COVID- 19).
Waziri amepokea mchango huo kwa niaba
ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo tarehe 13 Mei, 2020 katika Ofisi ya
Waziri Mkuu Mlimwa, Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kupokea mchango
huo Waziri Mhagama ameipongeza kampuni hiyo kwa kuunga mkono jitihada za
Serikali katika kuhakikisha inapambana na janga la ugonjwa wa COVID-19.
“Kwa niaba ya serikali nawashukuru
sana kwa kuwa sehemu ya watanzania katika kipindi hiki cha mapambano ya janga
la COVID-19. Tunawashukuru sana kwa kuendelea kuwa sehemu ya shida na raha za
Taifa hili,” ameeleza Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama amewahakikishia
watanzania kuwa michango hiyo inasimamiwa vyema na serikali kwa kuitumia
michango hiyo katika kushughulikia majukumu yaliyopangwa ya kupambana na janga
la ugonjwa wa COVID-19.
Awali, Waziri wa Nishati Dkt. Medadi
Kalemani ameipongeza kampuni hiyo kwa mchango wao kwa Serikali kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19.
“Kampuni hii ni moja ya wawekezaji
waliojenga Kiwanda hapa nchini, lakini pamoja na shughuli za uwekezaji wameguswa katika
kipindi hiki wakati serikali inapambana na janga hili la ugonjwa wa COVID-19, tunawashukuru
sana kwa mchango wenu kwa watanzania ”amesema Dkt. Kalemani.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.