Friday, August 17, 2018

WATENDAJI WA HALMASHAURI HAMUENDI KWA WANANCHI-MAJALIWA


*Asema wingi wa mabango kwenye mikutano ya viongozi ni ishara tosha

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwepo kwa mabango mengi kwenye mikutano ya hadhara  ya viongozi wakuu kunadhihirisha wazi kwamba watendaji wa  Halmashauri hawawatembelei  wananchi katika maeneo yao na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

“Watendaji hamuendi kuwatembelea wananchi na kusikiliza matatizo yao, haiwezekana wawe wanawasubiri viongozi wa juu na kuwasilisha kero zao, sasa jipangeni haya mabango yote mtakuja kuyajibu kwa sababu hoja zote ni za ngazi ya halmashauri,” alisema.

Aliyasema hayo jana jioni (Ijumaa, Agosti 17, 2018) wakati akizungumza na wananchi wa jimbo la Nzega Mjini kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Parking, ambapo aliwataka viongozi wa halmashauri hiyo kutenga siku maalumu kwa ajili ya kwenda vijijini kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeelekeza nguvu kubwa katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, hivyo itasimamia kuhakikisha kila mtumishi anawajibika kwa kiwango kinachostahili.

Alisema Serikali inataka kuona wananchi wakihudumiwa, Makatibu Tawala wa Wilaya wanatakiwa kujiridhisha kwenye halmashauri zao kama watumishi wa umma wanafanyakazi ipasavyo  na iwapo hawaridhishwi wanatakiwa kutoa taarifa kwenye ngazi husika.

“Serikali hii haimlindi mfanyakazi ambaye ni mbadhilifu, mwizi na ambaye hafanyi kazi kwa weledi au anayebagua wananchi eti kwa uwezo wake wa kifedha au rangi au dini yake au chama chake. Hivi vitu havipo katika Serikali kila mwananchi aliyeko Nzega anatakiwa kuhudumiwa,”alisisitiza

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya wafuatilie na kujua kiasi cha fedha kinachopelekwa na Serikali katika halmashauri zao kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kujiridhisha kama zinatumika kama ilivyokusudiwa.
“Ni lazima viongozi hao wajue fedha za miradi zilizopatikana katika halmashauri zao ili waweze kwenda kukagua utekelezwaji wa miradi husika na kujiridhisha kama inakidhi viwango na inalingana na kiasi cha fedha kilichotumika,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu alitoa siku 30 kwa  uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Nzega uwe umekamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara katika shule ya sekondari ya Magengati. Miaka minne iliyopita wananchi walijitolea kwa kujenga maboma na kuiachia halmashauri imalizie hatua zilizofuata.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa jimbo la Nzega Vijijini katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Usagali, ambapo alisema ni lazima ujenzi wa vyumba hivyo vya maabara ukamilike. “Haiwezekani miaka minne vyumba hivyo viwe havijakamilika,”.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.