Saturday, August 18, 2018

WAZIRI MKUU AWAWASHIA MOTO MADIWANI MANISPAA YA TABORA


*Awataka wajiondoe kufanya biashara na halmashauri hiyo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora wajiondoe katika kufanyabiashara na halmashauri hiyo kwa kuwa wanakiuka maadili ya utumishi wa umma.

Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Agosti 18 ,2018) wakati akizungumza na watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Manispaa ya Tabora na Hospitali ya Rufaa ya Kitete katika ukumbi wa Isike Mwanakiyungi.

“Madiwani mjiondoe kuwa wasimamizi wa kampuni zinazozofayakazi na halmashauri yenu na wakuu wa idara nanyi muwe makini mfanye kazi na kampuni huru ili muweze kuchukua hatua pale linapotokea tatizo,”.

“Nyie Madiwani ndio mnaopaswa kuisimamia halmashauri, sasa kama watu mliopewa dhamana mkiingia katika kufanya shughuli nyingine mnawakwaza wakuu wa idara na kuharibu mambo. Fanyeni kazi yenu ya kuisimamia halmashauri kwa mujibu wa dhamana mliyopewa,”.

Waziri Mkuu amesema Madiwani wawe wanafanya tathmini ya ushauri unaotolewa na wakuu wa idara na wasijihusishe na biashara ndani ya halmashauri zao na badala yake waziachie kampuni zifanye kazi zenyewe na Serikali bila ya kuzisimamia.

Waziri Mkuu alitolea mfano wa mradi wa ununuzi maroli mawili na makontena 20 ya kukusanyia taka mitaani ya Manispaa hiyo na kampuni inayomilikiwa na diwani ilipewa zabuni ya kununua vifaa hivyo, ambapo ilikabidhi roli moja likiwa bovu na kukataliwa. “ Yeye akaenda kulipaka rangi na kuwaletea, walilikataa tena,”.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Bw. Msalika Makungu aifanyie uchunguzi ofisi ya Mwekahazina  wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora baada ya kuwepo kwa utafunaji wa fedha za umma kwa visingizio mbalimbali.

Amesema zaidi ya sh. milioni 12.4 zimelipwa na Mwekahazina wa Halmashairi ya Manispaa hiyo, Bw. Abbas Mwanzori kwa ajili ya malipo ya wahasibu waliofanya kazi muda wa ziada na watumishi, huku kukiwa hakuna fomu zilizojazwa na watumishi hao.

“Hatuwezi kwenda mbele tukiwa na watu wa namna hii. Halmashauri haiwezi kuendelea mtu anatumia vibaya ofisi kwa manufaa yake binafsi. Na kati ya fedha hizo sh. milioni 8.4 mlizitoa kwa kutumia ‘password’ ya Halima (Mhasibu) bila ya kumjulisha na alipogundua akahoji mkamuhamishia sokoni, Naagiza arudishwe mara moja,”.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wajikite katika kufanya kazi vizuri na watambue dhamana waliyopewa na Serikali ambayo ni kuwatumikia wananchi wa Tabora na si vinginevyo. “Tunahitaji kuona mabadiliko ya maendeleo kwenye maeneo yenu ya kazi,”.

Waziri Mkuu amewaambia watumishi hao kuwa ili waweze kupata mafanikio ya kiutendaji lazima wawe na mpangokazi utakamuwezesha kila mmoja wao kutimiza wajibu wake. Mipango hiyo iwe shirikishi kwa kila mtumishi ndani ya idara husika.

Pia amewaagiza Wakuu wa Wilaya wasimamie utendaji wa pamoja katika idara zilizo ndani ya halmashauri zao na wahakikishe watendaji hao wanawatembelea wananchi katika maeneo  yao ili wanapokutana kwenye Mabaraza ya Madiwani wafanye tathmini ya kina juu ya mafanikio na changamoto zinazowakabili wananchi.

Kadhalika Waziri Mkuu alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora ya Kitete na kukagua maendeleo ya chuo cha Afya kinachojengwa hospitalini hapo pamoja na kutembelea wodi ya akinamama waliojifungua.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.