Wednesday, March 21, 2018

KATIBU MKUU OFISI YA WAZIRI MKUU AONGOZA KIKAO CHA BARAZA LA WAFANYAKAZI.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge na Waziri Mkuu Bi. Maimuna Tarishi ameongoza Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo na kuwaasa wajumbe wa baraza kutoa maoni yatakayosaidia kufanikisha mchakato wa maandalizi ya Bajeti ya mwaka 2018/2019.

Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Kikao hicho Tarishi amesema kuwa Watumishi wote katika Ofisi hiyo wanao wajibu wakushiriki kikamilifu katika mchakato wa maandalizi ya bajeti ili kufanikisha azma ya Serikali kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Bila kujali nafasi zenu ni lazima mtambue kuwa mnao wajibu sawa katika kutoa maoni yatakayosaidia katika mchakato wa maandalizi ya bajeti” alisisitiza Bi.  Tarishi.

Akifafanua Tarishi amesema kuwa Ofisi yake imekuwa ikizingatia maoni ya wajumbe wa baraza hilo katika maandalizi ya bajeti hivyo ni wakati mwingine tena kwa watumishi hao kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika kikao cha baraza hilo kwa kutoa mchango utakaosaidia katika utendaji wa Ofisi hasa katika kipindi hiki cha maandalizi ya bajeti.

Aliongeza kuwa Baraza hilo linafanyika ikiwa ni utekelzaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanayotaka Ofisi zote za Serikali kuwapa  nafasi watumishi wake kutoa maoni yao kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo bajeti kupitia kwenye baraza la Wafanyakazi hali inayochochea maendeleo na tija katika utoaji wa huduma.

Naye Katibu wa TUGHE mkoa wa Dodoma Bw. John Mchenya alieleza kuwa Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wanapaswa kuwa kielelezo katika uwajibikaji na utekelezaji wa majukumu yao ili kuwa mfano wa kuigwa hususan katika kukilinda na kuhakikisha uhai wa chama cha Wafanyakazi kwa kutenda haki kwa mujibu wa sheria zilizopo.

“Ni vyema kila mmoja wenu akawa wakili mzuri katika utendaji kuzingatia Ofisi hii ndiyo mtendaji Mkuu wa Shughuli za Serikali bila kuacha kuzingazita uwepo wa TUGHE kwa kuwa ipo kwa mujibu wa Sheria namba 6 inayoeleza masuala ya ajira na usajiri wa vyama vya Wafanyakazi”.Alisema Bw.Mchenya

Kwa upande wake mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo Bw.Yona Mwakilembe  amesema kuwa  maoni ya watumishi katika Ofisi hiyo yamekuwa yakizingatiwa kwa ukamilifu  hali inayoongeza morali kwa watumishi wa Ofisi hiyo.

“Tangu nimehamia hapa nimeshuhudia kwa kiwango kikubwa kwamba maoni tunayotoa kupitia baraza la wafanyakazi yanazingatiwa hivyo ni jambo la kujivunia na tunapongeza kwa hatua hii” Alisisitiza

Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu linafanyika mjini Dodoma leo Machi 21, 2018 ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa uliowekwa na Serikali kupitia Wizara,  Mikoa,  Wilaya, Idara, Wakala, Taasisi na Mashirika ya Umma kuwapa nafasi watumishi kutoa maoni yao kupitia baraza la wafanyakazi ili kuongeza tija na uwajibikaji katika Taasisi husika.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.