Sunday, March 11, 2018

WAKULIMA 2000 WAONGEZA KIPATO KWA UJENZI WA DARAJA LA MIVARF

Muonekano wa Daraja la Masware lililopo katika kijiji cha Masware Kata ya Kiru Wilayani Babati, daraja hilo limejengwa na Mradi wa Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za kifedha Vijijini (MIVARF).
Baadhi ya waendesha pikipiki ambao ni wakazi wa kijiji cha Masware Kata ya Kiru Wilayani Babati wakipita  katika Daraja la Masware lililojengwa na Mradi wa Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za kifedha Vijijini (MIVARF).

Baadhi ya watembea kwa miguu ambao ni wakazi wa kijiji cha Masware Kata ya Kiru Wilayani Babati wakipita  katika Daraja la Masware lililojengwa na Mradi wa Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za kifedha Vijijini (MIVARF).

Na Mwandishi wetu
Wakulima 2000 kutoka  vijiji sita vya, Kata ya Kiru Wilayani Babati wameongeza kipato kutokana na ujenzi wa daraja lililojengwa na Mradi wa Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za kifedha Vijijini (MIVARF),  ikiwa ni sehemu ya malengo ya mradi huo katika kuongeza kipato nchini hususan  maeneo ya vijijini.
Wakulima hao wa Kata ya Kiru, inayojumuisha kaya 306, walishindwa kuongeza kipato kwa takribani  miaka 38,  tangu mwaka 1978, baada ya Daraja walilokuwa wanatumia kusombwa na Mafuriko hadi mwaka 2016, Serikali kupitia Mradi wa MIVARF ilipojenga  Daraja hilo ambalo limeanza kutumika sasa na  kuchochea shughuli zao za  kiuchumi .
Akiongea  na timu ya  wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na  Mradi  wa MIVARF mara baada ya kutembelea Kijiji cha Masware lilipojengwa Daraja hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Babati Hamis Malinga amesema, Serikali kupitia Mradi wa MIVARF imeweza kuchochea uwekezaji katika kata hiyo
Kiwanda cha Sukari cha Manyara kimeweza kuongeza uzalishaji kutoka tani 15 hadi 30 kwa siku kutokana na ujenzi wa daraja la kijiji cha Masware ambalo limesaidia kuboresha biashara baina ya vijiji na kuongeza kipato kwa wananchi. Aidha, Usafirishaji wa mazao na bidhaa ulikuwa wa gharama kubwa sana lakini kwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kupitia mradi huu tumeweza kuona maendeleo makubwa katika Vijiji hivi”, alisema Mkurugenzi Malinga.
Kwa upande wa wakulima wa kijiji  cha Masware wamesema ujenzi wa Daraja hilo umeongeza kipato chao kwani wanaweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi pamoja na vijana wamepata ajira kupitia usafiri wa pikipiki maarufu kama “bodaboda”  unaotumiwa kusafirisha abiria
“Tangu ujenzi wa daraja hili tumeweza kupeleka mazaoyetu katika soko tunalotaka ambapo awali haikuwa rahisi, wakulima walikuwa wanalanguliwa gunia moja la mahindi lilikuwa likiuzwa kuanzia shilingi elfu 20,000 hadi 30,000 lakini kwa ujenzi wa daraja hili wananchi wanaweza kuuza mahindi kuanzia elfu 50,000 hadi 60,000 kwa gunia moja” amesema Aboubakar  Mohamed.
Naye Mkulima wa Kijiji hicho Zena Mpinga ameeleza  kuwa, “kabla ya ujenzi wa daraja hilo wanawake na wamama wajawazito walikuwa wakisafiri kwa shida na kwa gharama kubwa sana ambapo ukisafiri kwa kutumia pikipiki maarufu kama “bodaboda” ilikuwa ni shilingi elfu 10,000 kutokana na ukosefu wa kivuko imara na bora na kulazimu kuzunguka na pikipiki kijiji jirani ila kwa sasa usafiri wa bodaboda ni shilingi elfu 2000 hadi 3000 tu inakufikisha na kuweza kukamilisha mahitaji yako kwa wakati.
Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF), inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na kutekelezwa katika Halmashauri 76 za Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwa  imegharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (IFAD) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (ADB) kwa kushirikiana na  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.