Serikali inategemea Bodi ya Mpya ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI italeta fikra mpya, mbinu mpya, na weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha Mfuko huo unakuwa chombo madhubuti cha kuhakikisha Tanzania inafikia malengo yake ya kutokomeza UKIMWI ifikapo Mwaka 2030.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. William Lukuvi (MB) wakati akizinduza Bodi ya Tatu ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust Fund - ATF) jijini Dodoma.
Waziri Lukuvi ameeleza kuwa, Bodi hiyo inapaswa kutambua kuwa dunia ipo katika hatua mpya na muhimu ya kimkakati katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ambapo Tanzania kama sehemu ya jumuiya ya kimataifa imesaini na inatekeleza ahadi na makubaliano mbalimbali ya kimataifa na kikanda.
“Tumejidhatiti kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs 2030), hasa lengo la tatu linalohusu kuhakikisha afya njema na ustawi kwa wote, vilevile, tunaitekeleza kwa dhati Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063, pamoja na Azimio la Kisiasa la Umoja wa Mataifa la mwaka 2021 kuhusu UKIMWI” amefafanua Waziri Lukuvi.
Aidha, Mhe Lukuvi ameitaka Bodi hiyo kutambua kwamba kwa sasa dunia inashuhudia mabadiliko makubwa katika namna ya kufadhili mapambano dhidi ya UKIMWI.
“Wahisani wakuu wa Kimataifa kama PEPFAR na Global Fund wameshaanza kupunguza kwa awamu michango yao huku wakisisitiza umuhimu wa nchi kuchukua umiliki wa ndani na kuhakikisha uendelevu wa kifedha kwa juhudi zake. Mwelekeo huu unatutaka sisi kama Taifa kuongeza uwezo wetu wa ndani wa kifedha ili kuhakikisha mwitikio wa VVU na UKIMWI unaendelea kwa nguvu, kasi, na mafanikio makubwa”.
“Katika muktadha huu, Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI (ATF) ni nyenzo muhimu sana katika kuhakikisha Taifa linakuwa na uhakika wa kifedha na usalama wa afya ya wananchi wake” amebainisha Waziri Lukuvi.
Vilevile ameeleza kuwa, Mfuko huo ni alama ya dhamira ya kweli ya Serikali kuhakikisha kuwa huduma za VVU na UKIMWI zinadumu, hata katika mazingira ambapo michango ya wahisani inapungua.
“Kupitia Mfuko huu, tunasisitiza umiliki wa kitaifa ambapo Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia, taasisi za dini, vijana, watu wanaoishi na VVU na jamii kwa ujumla wanashiriki kikamilifu katika juhudi hizi. Mfuko huu pia unaleta msukumo mkubwa wa uwajibikaji wa kisera na kifedha kwa kuhakikisha matumizi ya fedha yanazingatia uwazi na matokeo yanayoonekana” ameongeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw. Sabasaba Mushingi amemshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuamini na kumchagua yeye kuwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wake na hivyo kuahidi kuisimamia na kuingoza bodi hiyo ili kuweza kutimiza malengo ya majukumu waliyopewa.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.