Serikali y
a Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kuweka mifumo, sera na mikakati madhubuti ya kuzuia, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali ya pindi baada ya maafa yanapotokea, ili kuimarisha usalama na ustawi wa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa jijini
Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala
ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi, wakati wa hafla ya kufunga mafunzo
ya wakufunzi kuhusu usimamizi wa hatari zitokanazo na maafa Mafunzo hayo yaliandaliwa
na Jumuiya ya Nchi Zilizopo kwenye Mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) kwa
ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Uturuki (TİKA), Shirika la Msalaba
Mwekundu la Uturuki, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki ya Tanzania.
Dkt. Yonazi amesema kuwa
mafunzo hayo yamekusudia kuimarisha uwezo wa kitaifa na wa kikanda katika
kudhibiti maafa na kuwalinda wananchi. Alibainisha kuwa mafunzo hayo yanaonesha
umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kupunguza hatari za maafa (DRR),
sambamba na kujenga jamii imara na endelevu.
“Kuwajengea uwezo viongozi wa
jamii ni jambo la msingi, kwani wao ndiyo wahusika wa kwanza kutoa mwitikio
wakati wa majanga, kusaidia kuratibu misaada na kuhakikisha usalama na ustawi
wa jamii,” amesisitiza Dkt. Yonazi.
Aidha, amewapongeza wadau wote
waliowezesha mafunzo hayo kufanyika kwa mafanikio, akiwemo TİKA, Sekretarieti
ya IORA, Msalaba Mwekundu wa Uturuki, pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa mchango wao mkubwa na ushirikiano thabiti.
“Ni faraja kubwa kwa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mafunzo haya muhimu kwa maendeleo ya
ukanda huu. Nawatakia kila la heri na natumai mmefurahia uwepo wenu hapa Dar es
Salaam na Tanzania kwa ujumla. Tunawakaribisha tena na tena,” amesema.
Kwa upande wake, Balozi wa
Uturuki nchini Tanzania, Mheshimiwa Bekir Gezer, alieleza kuwa Serikali ya
Uturuki itaendelea kushirikiana na Tanzania, hasa katika masuala yahusuyo
maafa. Amesisitiza kuwa nchi yao iko tayari kusaidia kwa kutoa vifaa muhimu vya
kukabiliana na maafa.
Naye, Bi. Filiz Sahinci,
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la TİKA nchini Tanzania, amesema shirika
hilo limejikita kusaidia juhudi za kukabiliana na maafa kwa kubadilishana
uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika kutatua changamoto zinazotokana na
maafa.
Mafunzo hayo yamehusisha
wakufunzi kutoka Mataifa Kumi na Moja zilizopo kwenye Mwambao wa Bahari ya
Hindi na yameweka msingi muhimu wa kuimarisha utayari wa jamii dhidi ya majanga
na magonjwa ya kuambukiza, hususan katika mazingira ya baada ya maafa.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.