Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization - WMO) Bi. Celeste
Saulo ameahidi kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mfumo wa Tahadhari ya
mapema (early warning systems) kwa ajili ya kuchukua hatua za haraka kuzuia na
kukabiliana na maafa pindi yanapotokea.
Ameyasema hayo wakati wa kikao
cha pembezoni mwa Jukwaa la Nane la Dunia la Kupunguza Madhara ya Maafa na
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, na Uratibu, Dkt.
Jim Yonazi pamoja na ujumbe alioongozana nao kwa lengo la kuzungumza mikakati
na mipango ya kuendeleza ushirikiano mapema 05 Juni 2025 mjini Geneva Uswizi.
Bi. Celeste Saulo amesema wapo
tayari kuwezesha maeneo mbalimbali ikiwemo ya kuongeza ueleza kupitia mafunzo
kwa wataalam kwenye masuala ya Matumizi ya Taarifa za hali ya hewa pamoja na masuala muhimu kama
elimu na kuona namna wanavyoweza kuunga nguvu za Pamoja katika matumizi ya
vifaa vya kisasa vya utabiri wa hali ya hewa na matumizi ya taarifa
zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya hewa kwa lengo la kuendelea kuwa na
tahadhari za mapema.
“Tunaendelea kushirikiana na
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kuwa tuna ushirikiano wa muda mrefu.Aidha,
tunazingatia umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa maafa kwa kuzingatia hatua
zinazochukuliwa na Tanzania ya kujenga uwezo pamoja na kushirikiana na nchi
zingine na kuandaa miradi ambayo inazingatia vipaumbele vyenye maslahi kwa
wote,” alisisitiza Bi. Saulo
Kwa hatua hiyo Bi. Saulo
ameipongeza Tanzania kwa namna imeendelea kuwa ya mfano katika kuratibu,
masuala ya menejimenti ya maafa na kuhakikisha wanakuwa na mifumo ya tahadhari
za mapema inayowasaidia katika kupeana taarifa za mapema zinazosaidia kuzuia
madhara yanayoweza kutokea wakati wa maafa.
Aidha alifafanua kuwa mifumo
ya tahadhari za mapema ni muhimu kwani inasaidia kuandaa mifumo jumuishi ya
kupeana taarifa za tahadhari za mapema; kupata taarifa mapema zinazosaidia
kupunguza madhara ya majanga, kuwezesha upatikanaji wa taarifa za awali
zitakazosaidia kuimarisha mfumo wa maisha ya jamii ambayo iko katika hatari ya
kuathirika na majanga na kupunguza madhara katika kujiandaa kwa ajili ya maafa
yanayoweza kutokea.
Katika mazungumzo hayo, Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, na Uratibu, Dkt. Jim
Yonazi amesisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania kuendeleza ushirikiano na
Mamlaka ya Hali ya Hewa Duniani katika kuimarisha masuala ya usimamizi wa maafa
inayolenga kuwawezesha kuwa na jamii stahimilivu na majanga na kuifanya Dunia
kuwa sehemu salama ya kuishi.
Akiongelea namna Tanzania
inavyoendelea kuratibu masuala ya Menejimenti ya maafa kwa kuzingatia sheria,
kanuni na taratibu zilizopo ili kuendela kulinda jamii isipatwe na madhara
yatokanayo na maafa huku akiainishsa mafanikio makubwa ikiwemo la uwepo wa Kituo
cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema (National
Emergency Operation and Communication Center Situation Room) katika Kituo cha
Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura nchini Tanzania chenye tija kwa
Taifa kwani kimerahisisha utekelezaji na utendaji wa haraka katika masuala ya
maafa.
Viongozi hao wamejadili
umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya maendeleo jumuishi ili kuhakikisha
juhudi za pamoja katika kukabiliana na maafa kwa kushirikiana na wadau wengine
ili kuinufaisha jamii nzima.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.