Friday, April 7, 2017

MAPITIO NA MWELEKEO WA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU 2017/2018-SEHEMU YA PILI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe . Kassim Majaliwa akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano kuhusu mapitio na mwelekeo wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.


Kilimo


31.           Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa mwaka 2015/2016 ikijumuisha mazao ya nafaka na yasiyo ya nafaka ulifikia tani 16,172,841 ikilinganishwa na mahitaji ya kitaifa ya tani 13,159,326. Hivyo, katika kipindi hicho nchi ilikuwa na ziada ya tani 3,013,515 za chakula. Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017, hali ya upatikanaji wa mvua katika Mikoa inayopata mvua za vuli haikuwa ya kuridhisha na hivyo kusababisha ukame na upungufu wa mavuno katika baadhi ya maeneo. Tathmini ya awali imebainisha kwamba Halmashauri 55 zimeathirika na ukame.

32.              Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na hali hiyo, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kununua mazao ya chakula kutoka katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba. Aidha, wafanyabiashara waliokuwa wamehifadhi nafaka katika maghala, walitakiwa kuzisambaza katika masoko ya ndani. Vilevile, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya walielekezwa kuwahamasisha na kuwaelekeza wakulima kupanda mbegu bora za mazao ya kilimo yanayostahimili ukame na yanayokomaa kwa muda mfupi kwa kipindi hiki cha mvua za masika. Ili kutoa msukumo katika kazi hiyo, kiasi cha tani 1,969 za mbegu bora za mazao yanayostahimili ukame zilinunuliwa na Serikali na kusambazwa katika Halmashauri zilizobainika kuathirika na ukame. Pia, wakulima wanaendelea kuhamasishwa kuzitumia vizuri mvua zinazonyesha katika msimu huu wa masika kwa kupanda mazao hayo yanayostahimili ukame na kukomaa mapema.

33.              Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo katika uchumi wetu, Serikali imeweka dhamira ya kuongeza uzalishaji, tija na kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara. Katika mwaka 2016/2017, Serikali ilifanikisha kupatikana kwa tani 277,935 za mbolea na tani 23,333 za mbegu bora. Aidha, hadi Februari 2017, Serikali ilitoa tani 30,773 za mbolea ya ruzuku ya kukuzia na kupandia kupitia vituo vya mauzo ya mbolea vya Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC).

34.       Mheshimiwa Spika, moja ya ahadi ya Serikali kwa wakulima wetu ni kupunguza kodi, tozo na ada mbalimbali zinazochangia kupunguza faida kwa mkulima. Katika mwaka 2016/2017, Serikali ilifuta baadhi ya tozo za mazao ambazo ni kero kwa wakulima katika mazao ya pamba, chai na kahawa. Tozo zilizofutwa kwenye zao la pamba ni mchango wa Mwenge wa Shilingi 450,000 unaotolewa na kila kiwanda cha kuchambua Pamba na ada ya vikao vya Halmashauri za Wilaya ambayo ni shilingi 250,000. Kwa zao la chai, kodi ya moto na uokoaji imeondolewa na katika zao la kahawa, ada ya leseni ya kusindika kahawa ya Dola za Marekani 250 nayo pia imefutwa.

35.      Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeboresha Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani kwa kuanzisha utaratibu wa wazi wa ununuzi wa mazao kupitia minada. Mathalani, katika msimu wa 2016/2017 kwenye zao la korosho, utaratibu huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa bei ya korosho kwa kilo kutoka shilingi 1,200 hadi shilingi 3,800, bei ambayo haijawahi kufikiwa katika historia ya zao la korosho nchini. Aidha, Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani na utaratibu wa minada umeongeza ushindani na kuvutia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi hususan nchi ya Vietnam na nchi nyingine kuja wenyewe kununua korosho badala ya kutegemea soko la India pekee. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea na uchambuzi wa kina wa kodi, tozo na ada zilizobaki katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuziondoa au kuzipunguza ili kumwezesha mkulima, mvuvi na mfugaji anufaike zaidi na jasho lake na kuongeza mapato ya Halmashauri zetu. Kwa sasa, tunashughulikia zao la tumbaku kwa kupitia tozo zake na pia kubaini ubadhirifu unaoendelea kwenye ushirika huo.

Mifugo


36.              Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza uzalishaji wa mitamba na uhimilishaji wa mifugo ili kuhamasisha ufugaji wa kisasa na wenye tija. Mitamba 546 imezalishwa kutoka mashamba ya Serikali na mitamba 88 kutoka NARCO na kusambazwa kwa wafugaji wadogo. Aidha, Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji – NAIC Usa River, Arusha kimeimarishwa na kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za ng’ombe hadi kufikia dozi 10,494 ikilinganishwa na dozi 8,000 zilizozalishwa na kusambazwa katika mwaka 2015/2016. Pia, ng’ombe waliohimilishwa wameongezeka kutoka 221,390 mwaka 2015/2016 hadi ng’ombe 457,557 mwaka 2016/2017.

37.         Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kuimarisha kituo chetu cha kuzalisha mitamba cha Kitulo wilayani Makete ili kukiongezea uwezo wake. Aidha, Serikali inatoa nafasi kwa mashamba binafsi kuzalisha mitamba zaidi kama mashamba ya ASAS kule Iringa ili wafugaji wadogo wanufaike.  Serikali pia itaendelea na zoezi la kutenga, kupima na kumilikisha wafugaji maeneo ya ufugaji na kujenga miundombinu ya mifugo kwa kuongeza idadi ya malambo na mabwawa katika mikoa. Hatua hizo zitasaidia kupunguza uzururaji wa mifugo na migogoro baina ya wafugaji na wakulima na hifadhi za misitu.

Madini


38.       Mheshimiwa Spika, Sekta ya madini ni muhimu kwa uchumi wetu. Serikali imetenga maeneo zaidi kwa ajili ya wachimbaji wadogo, kuweka utaratibu mzuri zaidi wa kutoa ruzuku pamoja na kuimarisha shughuli za ugani. Katika kipindi cha mwezi Julai 2016 hadi Februari 2017, Serikali imetenga maeneo 11 yenye ukubwa wa hekta 38,567 kwa ajili ya wachimbaji madini wadogo. Maeneo hayo ni Msasa na Matabe mkoani Geita, Biharamulo na Kyerwa mkoani Kagera, Itigi mkoani Singida, D-Reef, Ibindi na Kapanda Mkoani Katavi, Ngapa mkoani Ruvuma, Kitowelo na Namungo mkoani Lindi pamoja na Nzega mkoani Tabora.

39.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali za madini na kuimarisha ukaguzi wa shughuli za uzalishaji na biashara ya madini kwa migodi mikubwa, ya kati na midogo. Aidha, Serikali itaendeleza wachimbaji wadogo na wa kati wa madini pamoja na kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani wa madini hayo.

Huduma za Kiuchumi

Ardhi

40.           Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2016/2017, Serikali iliahidi kuanza ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi. Ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kazi ya ujenzi wa mfumo huo awamu ya kwanza ilizinduliwa rasmi Agosti, 2016 na Mkandarasi tayari ameanza kazi. Sambamba na zoezi hilo, Serikali inakamilisha ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Taarifa za Ardhi. Kukamilika kwa mradi huo kutaboresha utendaji kazi, kuharakisha huduma za utoaji hati miliki, kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za ardhi ambapo nyaraka zote za ardhi zitakuwa katika mfumo unganishi wa kielektroniki.

41.    Mheshimiwa Spika, Serikali pia iliidhinisha ramani za upimaji zenye jumla ya viwanja 78,771 na mashamba 239. Aidha, Serikali imekamilisha upigaji wa picha za anga za Jiji la Dar es Salaam na inaendelea kutatua  migogoro ya matumizi ya ardhi  baina ya wakulima, wafugaji na hifadhi katika maeneo mbalimbali nchini.

42.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kujenga Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi na kuboresha usimamizi wa sekta ya ardhi kwa kufanya mapitio ya Sera na Sheria za Ardhi na  kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sera, sheria, kanuni na miongozo ya ardhi ili kudhibiti viashiria vya migogoro ya matumizi ya ardhi nchini. Ninatoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinashughulikia migogoro ya ardhi mapema na kuweka mazingira wezeshi ya upimaji wa ardhi katika Halmashauri zao.

Umeme


43.      Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua thabiti za kuongeza uzalishaji, kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na kuongeza kasi ya usambazaji umeme. Katika mwaka 2016, umeme uliozalishwa na kuingizwa katika Gridi ya Taifa uliongezeka na kufikia Gigawatt hours (GWh) 7,092 ikilinganishwa na Gigawatt hours (GWh) 6,227 zilizozalishwa mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 13.9. Vilevile, Serikali imepanua na kuboresha njia za usafirishaji umeme kwa kukamilisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovolti 400 na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme kutoka Iringa – Dodoma – Singida – Shinyanga.

44.      Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Katika kipindi cha mwaka 2016/2017, Wakala ulikamilisha ujenzi wa vituo sita (6) vya kuongeza nguvu ya umeme kutoka msongo wa kilovolti 11 hadi kilovolti 33 katika miji ya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Ngara, Mbinga na Tunduru; ujenzi wa njia za kusambaza umeme zenye urefu wa kilometa 17,740 za msongo wa kilovolti 33; ujenzi wa vituo vidogo vya kupoza na kusambaza umeme 4,100; na ujenzi wa njia ndogo ya usambazaji umeme wenye urefu wa kilometa 10,970.

45.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaongeza uzalishaji, kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme nchini. Aidha, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mradi mkubwa wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Kabaale (Uganda) hadi Tanga (Tanzania). Serikali pia, itawezesha uwekaji wa mtandao wa usambazaji wa gesi asilia kwenye viwanda na matumizi ya majumbani pamoja na uendelezaji wa mradi wa kusindika gesi asilia (Liquefied Natural Gas - LNG) mkoani Lindi.

Barabara


46.  Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Julai 2016 hadi Februari 2017, Serikali imejenga na kukarabati jumla ya  kilometa 430 za barabara kuu sawa na asilimia 62 ya lengo la kilometa 692.  Aidha, ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya TAZARA unaendelea vizuri pamoja na maandalizi ya kuitisha zabuni za ujenzi wa Daraja Jipya la Selander na ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam – Chalinze kwa kiwango cha Expressway. Vilevile, ujenzi wa barabara za juu (Interchange) kwenye makutano ya Barabara ya Ubungo ulizinduliwa rasmi tarehe 20 Machi, 2017. Hizi ni hatua muhimu za kukabiliana na changamoto ya muda mrefu ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015.

Vivuko na Usafiri Majini


47.    Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, Serikali ilipanga kujenga kivuko kipya cha Pangani (MV Pangani) na kukarabati kile cha Magogoni – Kigamboni. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba hadi kufikia Februari, 2017 ujenzi na ukarabati wa vivuko hivyo ulikuwa umekamilika. Aidha, ununuzi wa boti ndogo za abiria kwa ajili ya vivuko vya Kilambo – Namoto (Mtwara), Mkongo – Utete (Pwani), Pangani – Bweni (Tanga) na Msemo – Msangamkuu (Mtwara) utakamilika katika mwaka huu wa fedha. Kwa upande wa huduma za usafiri kwenye maziwa, Serikali inaendelea na ujenzi wa meli moja katika Ziwa Victoria, meli mbili katika Ziwa Nyasa zitakazofanya safari kati ya Kyela na Mbambabay pamoja na ukarabati wa meli za MV Victoria na Butiama (Ziwa Victoria) na MV Liemba (Ziwa Tanganyika).

 

Bandari


48.       Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Uboreshaji wa Bandari nchini kwa kufanya upanuzi na kuimarisha miundombinu ya Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Mifumo ya Ulinzi katika bandari hizo imeimarishwa na mashine za kisasa za kukagua mizigo zimefungwa. Kutokana na jitihada hizo, tumeanza kuona mwelekeo mzuri wa kuimarika ufanisi wa kiutendaji hususan katika Bandari ya Dar es Salaam. Tutaendelea kufanya maboresho zaidi ili Bandari ya Dar es Salaam iwe chaguo namba moja katika usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi yetu.   

Reli


49.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali iliendelea kutekeleza miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya Reli ya Kati ili kuongeza uwezo wa reli hiyo kutoa huduma za uchukuzi nchini na nchi jirani zinazotumia bandari zetu. Awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli mpya ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa kiwango cha standard gauge imeanza kutekelezwa kwa kusaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha reli ya Dar es Salaam - Morogoro (kilometa 205). Taratibu za kuwapata makandarasi wa ujenzi wa reli kutoka Morogoro – Makutupora (kilometa 336), Makutupora- Tabora (kilometa 294), Tabora- Isaka (kilometa 133) na Isaka- Mwanza (kilometa 254) zinaendelea.

Usafiri wa anga


50.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali imetekeleza kwa dhati azma ya kuimarisha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL). Katika kipindi hicho, ndege mbili (2) aina ya Dash 8 – Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja zilinunuliwa na kuanza kutoa huduma mwezi Oktoba, 2016. Aidha, mwishoni mwa mwaka 2016, Serikali iliingia mkataba wa ununuzi wa ndege nyingine nne (4). Kati ya hizo, ndege moja ya aina ya Dash 8 - Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 76 inatarajiwa kuwasili mwezi Julai, 2017. Ndege nyingine mbili (2) aina ya CS300 zenye uwezo wa kubeba abiria 127 kila moja zinatarajiwa kuwasili mwezi Juni, 2018 na ndege kubwa moja ya masafa marefu aina ya Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 inatarajiwa kuwasili mwezi Julai, 2018.

51.   Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa ununuzi wa ndege hizi kutaisaidia ATCL kuongeza safari za ndani na nje ya nchi na hivyo kuchangia katika jitihada za kuongeza watalii wanaokuja nchini kutembelea vivutio vyetu na kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini. Aidha, ATCL imeanzisha safari za kuja Dodoma na hivyo kuongeza uhakika wa usafiri wakati huu ambapo Serikali inahamia Dodoma. Wigo wa upanuzi kwa viwanja vyote nchini unaendelea na sasa hivi tunakamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege.

Mawasiliano


52.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, baadhi ya kazi zilizofanyika kwenye sekta ya mawasiliano ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; kutekeleza Mradi wa Anuani za Makazi na Postikadi; na kuanzisha huduma ya kituo cha Jamii Centre kitakachorahisisha utoaji wa huduma muhimu katika kituo kimoja. Huduma hizo ni kulipa pensheni, ankara na huduma za kibenki. Aidha, Sekta ya Mawasiliano inatekeleza Programu ya Miundombinu ya Kikanda ambayo inahusisha Mradi wa Shule Mtandao (e-school), Mradi wa Video Conference ambao unahusisha ununuzi, usimikaji na ufungaji wa vifaa vya TEHAMA katika Mikoa 26 na Taasisi za Serikali.

53.      Mheshimiwa Spika, Serikali pia inatekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mawasiliano Vijijini kwa kushirikiana na Kampuni   ya   Viettel   ya   Vietnam.   Mradi huu unatekelezwa kwa kipindi  cha  miaka  mitatu 2015-2017. Viettel wamekwishafikisha miundombinu ya mtandao wa intaneti kwenye shule 417, Ofisi za Halmashauri za Wilaya 123, Hospitali za Wilaya 74, Vituo vya Polisi vya Wilaya 131 na Ofisi za Posta 68.  

54.   Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa kituo cha kuhifadhi taarifa na mifumo ya Serikali (Government Data Centre). Lengo ni kuongeza na kuimarisha usalama wa mifumo na taarifa unaoenda sambamba na uhakika wa upatikanaji wa taarifa za Serikali katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku. Pamoja na ujenzi wa vituo hivyo, matumizi ya TEHAMA yameongezeka na hivyo kuziwezesha taasisi za Serikali kutoa mchango mkubwa kwenye uboreshaji na utoaji wa huduma, kuongeza mapato na kuokoa gharama mbalimbali.

Sekta ya Huduma za Jamii

Elimu


55.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujenga uwezo wa walimu wa shule za msingi kwa kuwapa mafunzo hasa katika ufundishaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK). Jumla ya walimu 22,995 wa shule za msingi na walimu 519 wanaofundisha elimu maalum kwa wanafunzi wasioona na wenye ulemavu wa kusikia wamepewa mafunzo hayo. Lengo ni kuhakikisha kila mwanafunzi anayemaliza darasa la saba anajua kusoma na kuandika.

56.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali iliendelea na mpango wa kutoa Elimumsingi bila malipo. Tangu utekelezaji wa mpango huo uanze, Serikali imekuwa ikipeleka wastani wa Shilingi bilioni 18.77 kila mwezi, ambapo shule za msingi 16,088 na shule za sekondari 3,602 zimenufaika na mpango huo. Mpango huo umeleta manufaa kwa Watanzania wengi wa kipato cha chini na cha kati na umeongeza uandikishaji wa wanafunzi kwenye shule za Msingi na Sekondari. Kufuatia ongezeko hilo, tulijikuta tukilazimika kupambana na upungufu wa madawati, jambo ambalo liliifanya Serikali ianzishe kampeni maalum ya kumtoa sakafuni mtoto wa Kitanzania. Hivi sasa madawati sio tatizo tena kwenye shule nyingi nchini. Nitumie fursa hii kutoa pongezi kwa Watanzania wote walioshirikiana na Serikali katika kutatua changamoto ya upungufu wa madawati.  Natoa pongezi kwa taasisi binafsi, watu binafsi na Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao yote.

57.     Mheshimiwa Spika, uchumi wa viwanda kwa kiasi kikubwa unahitaji rasilimaliwatu yenye weledi hasa katika masomo ya hisabati na sayansi. Kama zilivyo nchi nyingine Barani Afrika, Tanzania inakabiliwa na changamoto ya wanafunzi kutopenda kusoma masomo ya hisabati na sayansi na hivyo kuchangia katika ufaulu duni kwenye masomo hayo. Ni dhahiri kuwa watoto wetu wasipoweka bidii katika masomo ya hisabati na sayansi viwanda vyetu vitalazimika kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi jambo litakalowafanya Watanzania kuwa watazamaji.

58.   Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imefanya juhudi za kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi katika ngazi zote za shule. Aidha, Serikali inaendelea na Mpango wa Ujenzi wa Maabara katika shule za sekondari na vyuo vikuu pamoja na ununuzi wa vifaa. Katika mwaka 2016/2017, Serikali imenunua vifaa vya maabara kwa ajili ya shule 1,625 za sekondari zilizokamilisha ujenzi wa maabara na usambazaji wa vifaa umeanza mwezi Machi, 2017 katika Mkoa wa Dar es Salaam na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Aprili, 2017 kwa nchi nzima. Aidha, Serikali inatoa mafunzo kwa walimu 5,920 wanaosoma Stashahada maalum ya Sayansi, Hisabati na TEHAMA.

59.    Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kuimarisha ufundishaji wa masomo ya TEHAMA kwa shule za Sekondari. Serikali inaendelea na mpango wake wa kujenga maabara za kompyuta ili wanafunzi wawe na uelewa wa TEHAMA. Utekelezaji wake utafanyika hatua kwa hatua.
 
60.      Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa vibali vya ajira kwa walimu wa Hisabati na Sayansi 4,129. Natoa wito kwa wazazi wenzangu kuhamasisha watoto wetu kupenda masomo ya Hisabati na Sayansi. Naagiza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na TAMISEMI na wadau wengine waandae Mkakati Maalum wa kuhamasisha na kuwavutia wanafunzi kusoma masomo ya Hisabati na Sayansi. Mkakati huo pia uwezeshe upatikanaji wa walimu watakaofundisha masomo ya Hisabati na Sayansi katika shule za msingi na sekondari kwa kipindi kifupi bila kuathiri ubora wa ufundishaji.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.