Saturday, April 22, 2017

WAZIRI MHAGAMA: MAANDALIZI YA SHEREHE ZA MIAKA 53 YA MUUNGANO YAKAMILIKA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akieleza mafanikio ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa maandalizi ya maadhimisho ya sherehe za Muungano Mjini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Jenista Mhagama ameeleza kukamilika kwa maandalizi ya kuadhimisha sherehe za miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitakazofanyika Viwanja vya Jamhuri Mjini Dodoma, siku ya jumatano Aprili 26, 2017.

Ameyasema hayo leo wakati akizungumza waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Aprili 22, 2017 katika Ofisi yake Dodoma.

“Nipende kuwaeleza Watanzania wote kuwa hadi sasa maandalizi ya kuifikia siku ya Maadhimisho ya Sherehe za Muungano tayari yamekamilika kwa kuangalia mambo yote yaliyopangwa katika ratiba ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli.”Alisema Waziri Mhagama.

Amesema sherehe hizo zitakuwa na  upekee wa aina yake ukizingatia kuwa  ni mara ya kwanza tangu Serikali ilipotimiza adhma yake ya kuhamia Dodoma.

Akitaja upekee huo, Waziri Mhagama amesema sherehe hizo zitapambwa na Gwaride la heshima lililoandaliwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Maonesho ya Kikosi cha Makomando, Onesho la Mbwa na Farasi waliofunzwa, onesho la Ukakamavu la Uzalendo la Wanafunzi kutoka shule za Sekondari za Dodoma, burudani za vikundi vya ngoma kutoka Kaskazini Pemba pamoja na Bendi ya mziki wa kizazi kipya kutoka Dodoma, Yamoto Bend na Mwenge Jazz.
“Ikumbukwe hii itakuwa mara ya kwanza kuiadhimisha sherehe hii ya Miaka 53 ya Muungano wetu kwa kuzingatia Serikali sasa imeshahamia Dodoma na tayari Watendaji wake wapo huku hivyo tuitumie fursa hii kuwaalika Wananchi wote kuudhuria kwa wingi ili kuifanikisha na kuonesha Umoja wetu.”Alisistiza Waziri.

Kwa upande wake,   Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba  ametoa wito kwa Watanzania wote wajitokeze  kwa wingi kwenda  kuangalia mafanikio yaliyotokana na uwepo wa Muungano huo.

“Muungano huu umetupa mafanikio mengi ikiwemo; kuijengea nchi heshima, kuwepo kwa Katiba, kuimarika kwa Taasisi za kimuungano, ongezeko la masuala ya kimuungano kutoka 11 hadi 22, ongezeko la usalama, Kuwepo Mfumo dhabiti wa kushughulikia changamoto za Muungano na ongezeko la ushirikiano kwa masuala yasiyo ya Kimuungano.”Alieleza waziri Makamba.

Naye  Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana alipongeza jitihada za Ofisi ya Waziri Mkuu hususan Kitengo cha Maadhimisho kwa kushirikiana na Ofisi yake kwa kuratibu na kuhakikisha maandalizi yote yamekalika kwa wakati uliopangwa.

“Niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu kwa jitihada zake kuiratibu siku hii muhimu kwa Taifa letu, na nitoe wito kwa Wakazi wa Dodoma na walioko nje ya Mji kuonesha mfano kuja kwa wingi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.”Alisisitiza Mhe.Rugimbana.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.