Friday, April 7, 2017

MAPITIO NA MWELEKEO WA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU 2017/2018-SEHEMU YA KWANZA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe . Kassim Majaliwa akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano kuhusu mapitio na mwelekeo wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

UTANGULIZI

1.   Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2016/2017 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018. Aidha, ninaliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

2.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Bunge lako Tukufu limeondokewa na Wabunge wenzetu, Mheshimiwa Hafidh Ally Tahir aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani - CCM na Mheshimiwa Dkt. Elly Marko Macha, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum - CHADEMA. Pia, Taifa lilimpoteza Mheshimiwa Samwel John Sitta aliyekuwa Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, nchi yetu imekumbwa na majanga na maafa yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Ninaomba Mwenyezi Mungu awajalie nafuu ya haraka wale wote waliopata majeraha, na kuwapumzisha kwa amani wale waliopoteza maisha, Amina! Ninatoa pole kwa familia za wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki. Pia ninatoa pole kwa Mheshimiwa Aida Khenani aliyepata ajali ya kugongwa na pikipiki wakati akitoka Bungeni. Tunamuombea apone haraka na aweze kurejea Bungeni ili kuendelea na majukumu yake.

PONGEZI NA SHUKRANI


3.   Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wao. Sisi tunaowasaidia tunajivunia uongozi wao mahiri, uzalendo uliotukuka na dhamira njema waliyonayo kwa Watanzania.

4.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Bunge lako Tukufu limepokea na kuwaapisha Wabunge wapya watano, ambao ni Mheshimiwa Abdallah Majura Bulembo (Mb.), Mheshimiwa Anne Killango Malecela (Mb.), Mheshimiwa Juma Ali Juma (Mb.), Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb.) na Mheshimiwa Salma Rashidi Kikwete (Mb.). Ninawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wapya kwa heshima waliyoipata ya kujumuika nasi kwenye Bunge hili. Kama ilivyo ada, tutatoa ushirikiano unaotarajiwa kwa Waheshimiwa Wabunge hawa ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi na tija. Kipekee, ninampongeza Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.  

Pia ninatumia nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote walioteuliwa kuingia kwenye Bunge la Afrika Mashariki, Makatibu Wakuu wapya walioteuliwa na Mheshimiwa Rais yaani Profesa Kitila Alexander Mkumbo, Dk. Leonard Akwilapo, Maimuna Tarishi na Dk. Ave Maria Semakafu. Nawapongeza sana wote walioteuliwa kushika nyadhifa hizo.

5.   Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ninawashukuru kipekee sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini kwa kutoa mchango mkubwa wakati wa maandalizi ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia, niwapongeze Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kuongoza kwa umahiri mkubwa Kamati zao wakati wa kupitia makadirio ya sekta zote. Maoni na ushauri wao umesaidia sana kuboresha Makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mafungu yote.

6.   Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Idara, Mashirika na Taasisi zote za Serikali kwa ushirikiano wanaoendelea kunipa katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, ninawashukuru Wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, kwa kukamilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/2018.

7.   Mheshimiwa Spika, kipekee, ninamshukuru Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama (Mb.), Mbunge wa Peramiho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu); Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde (Mb.), Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana) kwa ushirikiano  wao mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Abdallah Possi aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa aliyofanya wakati akiitumikia nafasi hiyo. Ninamtakia kazi njema kwenye jukumu lake  jipya la kuiwakilisha Tanzania nchini Ujerumani. Vilevile, ninawashukuru wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Uongozi wa Makatibu Wakuu, Dkt. Hamisi H. Mwinyimvua; Bwana Eric F. Shitindi na aliyekuwa Katibu Mkuu Bwana Uledi A. Mussa kwa ushauri wao wa kitaalam kwangu na kwa Waheshimiwa Mawaziri.

8.   Mheshimiwa Spika, ninazishukuru pia nchi marafiki, Taasisi na Mifuko ya Fedha Duniani, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Madhehebu ya Dini na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kujenga uchumi wa nchi yetu.  Misaada na mikopo iliyopatikana kwa wakati imechangia kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

9.   Mheshimiwa Spika, ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati wananchi wa Jimbo la Ruangwa kwa kuendelea kuniunga mkono na kuielewa vizuri dhamana ya Kitaifa niliyonayo ya kusimamia utendaji wa Serikali katika sekta zote na kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Mwisho ninaishukuru familia yangu hususan mwenza wangu mpendwa, Mary na watoto wetu kwa upendo, dua na kuendelea kunitia moyo ili nitekeleze kwa ufanisi zaidi majukumu yangu ya Kitaifa.  Asanteni sana!MWELEKEO WA BAJETI


10.    Mheshimiwa Spika, ni mwaka mmoja sasa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani. Katika kipindi hicho, yapo mambo mengi yaliyofanyika kwa mafanikio makubwa ambayo yataanishwa kwa kina katika bajeti za Sekta pindi Mawaziri husika watakapoziwasilisha. Baadhi ya mafanikio hayo ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya Elimu Bila Malipo; kuongezeka kwa uzalishaji na kasi ya usambazaji wa umeme vijijini; kuimarika uwajibikaji na nidhamu katika Utumishi wa Umma; kuongeza ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma; kuboresha huduma za kiuchumi na za kijamii; na kutekeleza Awamu ya Kwanza ya Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma. Nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wa Serikali, Watumishi wa Umma na Watanzania wote kwa ujumla kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake, kwani bila ushirikiano wao, tusingeweza kupata mafanikio hayo.

11.    Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuandaliwa kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano; ahadi za Mheshimiwa Rais alizotoa wakati wa Kampeni, pamoja na maelekezo yake wakati anazindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015. Bajeti hii itaendelea kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika mwaka uliopita na kushughulikia utatuzi wa vikwazo vya kukuza uchumi kwa haraka na baadhi ya changamoto zilizojitokeza. Aidha, Serikali itajikita zaidi katika maeneo yatakayochangia kuimarisha uchumi wa viwanda na kuboresha huduma za jamii. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla, kuendelea kushirikiana na Serikali katika kufikia azma hiyo ili dhamira yetu ya kuboresha maisha ya Watanzania iweze kutimia. Ni vyema tukakumbuka kwamba tuna mwaka mmoja tu wa utekelezaji wa yale tuliyopanga kufanya ndani ya kipindi cha miaka mitano. Tutatumia bajeti ya mwaka ujao wa fedha kukabili changamoto zilizojitokeza. Ahadi ya Serikali ni kuendelea kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na bila ubaguzi wowote, huku tukitanguliza mbele maslahi ya Taifa.

SERIKALI KUHAMIA DODOMA


12.     Mheshimiwa Spika, tarehe 23 Julai 2016, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi, alitangaza uamuzi wa kuhamishia rasmi Shughuli za Serikali Kuu Dodoma. Kufuatia uamuzi huo, mipango ya kuhamia Dodoma kwa awamu ilianza baada ya mahitaji halisi yatakayoiwezesha Serikali kuhamia Dodoma kubainishwa, ikiwa ni pamoja na ofisi na nyumba za makazi kwa viongozi na watumishi wa umma. Awamu ya kwanza ilipangwa kuhama ifikapo mwisho wa mwezi Februari, 2017.

13.      Mheshimiwa Spika, ninafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tayari watumishi 2,069 wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo na watumishi wengine wamekwishahamia Dodoma kama ilivyopangwa. Vilevile, Wizara zote zimepata majengo ya Ofisi yatakayotumika katika kipindi cha mpito.

14.           Mheshimiwa Spika, ili Mji wa Dodoma uweze kuendelezwa kwa mpangilio mzuri, Serikali inaupitia upya Mpango Kabambe wa Mji wa Dodoma. Mapitio hayo yatasaidia sana kuepuka makosa yaliyofanyika katika miji mingi hususan ujenzi holela unaochangia katika uchafuzi wa mazingira na kuharibu mandhari ya miji. Ni wazi kwamba, ujenzi wa Mji wa Dodoma hautafanywa na Serikali pekee, bali tutaendelea kuhamasisha Sekta binafsi na wadau wengine kuwekeza Dodoma. Ninalipongeza sana Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kujenga nyumba 300 za makazi hapa Dodoma ambazo watumishi wanaweza kununua au kupangishwa. Ninatoa wito kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma kuongeza kasi ya upimaji wa viwanja, kuboresha miundombinu na kudhibiti ujenzi holela kwa kushirikiana kwa karibu na Manispaa ya Dodoma na Taasisi nyingine za Serikali.

SIASA


15.      Mheshimiwa Spika, mwaka mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, hali ya kisiasa nchini imeendelea kuwa shwari na ya kuridhisha. Aidha, Chaguzi Ndogo zilifanyika tarehe 22 Januari, 2017 katika Jimbo la Dimani - Zanzibar na Udiwani katika kata 20 Tanzania Bara kwa kushirikisha wagombea kutoka vyama 15 vya siasa. Ninavipongeza vyama vyote vilivyoshiriki katika chaguzi hizo, na kipekee nakipongeza Chama cha Mapinduzi kwa ushindi wa Jimbo la Dimani na viti 19 vya udiwani katika chaguzi hizo.

16.    Mheshimiwa Spika, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, mashauri 53 ya kupinga ushindi wa Ubunge na mashauri 194 ya kupinga ushindi wa Udiwani yalifunguliwa. Mashauri hayo yamekwishasikilizwa na hukumu kutolewa, isipokuwa shauri moja la kupinga matokeo ya Ubunge katika Jimbo la Mbagala. Nizipongeze Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuhakikisha kesi hizo zinaendeshwa kwa kasi na kwa weledi na hivyo kuwezesha wananchi kuendelea kupata uwakilishi.

17.    Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuboresha demokrasia hapa nchini, hatuna budi kujenga jamii inayoheshimu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi pamoja na kuwa na uvumilivu wa kisiasa. Ninatoa rai kwa wadau wa siasa kote nchini kujenga utamaduni wa masikilizano na kuendesha siasa za maendeleo badala ya siasa za malumbano; siasa za kuunganisha watu wetu badala ya kuwagawa; na siasa za uwajibikaji badala ya siasa za mazoea. Serikali itaendelea kulinda na kuheshimu misingi ya siasa zinazolenga kuleta ustawi wa wananchi na zinazotanguliza maslahi ya nchi na wananchi.

MUUNGANO


18.    Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kudumisha muungano wetu ambao ni tunu na mfano wa kuigwa barani Afrika na dunia nzima. Wananchi wanaendelea kunufaika na matunda ya Muungano wetu ambao ni imara na dhabiti. Serikali zote mbili zinafanya mashauriano kupitia Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kushughulikia masuala ya Muungano chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, viongozi na watendaji wa sekta nyingine zisizo za Muungano wamekuwa wakikutana mara kwa mara ili kubadilishana uzoefu na kubaini maeneo ya ushirikiano kwa ustawi wa wananchi wa pande zote mbili. Jumla ya vikao 13 vya sekta ambazo siyo za Muungano vilifanyika kati ya Julai 2016 na Machi 2017.

19.      Mheshimiwa Spika, ninapenda kutumia fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendesha kwa ufanisi mkubwa kikao kilichofanyika tarehe 13 Januari, 2017 ambapo taarifa kuhusu hoja zilizopatiwa ufumbuzi, maagizo na maelekezo ya kufuatilia utekelezaji wa changamoto zilizobaki ilitolewa. Serikali itaendelea kuulinda na kuuenzi Muungano wetu kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

HALI YA UCHUMI


20.           Mheshimiwa Spika, mwenendo wa viashiria vya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kwa mwaka 2016/2017 vinaonesha kuwa uchumi wetu unakua na kuimarika. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, ukuaji halisi wa Pato la Taifa ulifikia asilimia 7.0 mwaka 2016. Sekta zilizochangia kwa kiwango kikubwa kwenye ukuaji huo ni uchimbaji madini na mawe;  usafirishaji na uhifadhi wa mizigo; habari na mawasiliano; pamoja na shughuli za fedha na bima. Mfumuko wa Bei uliendelea kubakia katika wigo wa tarakimu moja na kasi ya upandaji bei ilipungua kutoka wastani wa asimilia 5.6 mwaka 2015 hadi asilimia 5.2 mwaka 2016. Kwa upande mwingine, tathmini ya hali ya Taasisi za Fedha inaonesha kuwa Benki zetu ziko salama na zina mitaji na ukwasi wa kutosha. Aidha, taarifa za Mashirika mbalimbali ya Kimataifa zinaonesha kwamba katika mwaka 2016 uchumi wa Taifa letu ulikua vizuri na hivyo kutufanya kuwa miongoni mwa nchi sita (6) za Bara la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa zaidi.

21.      Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeweka juhudi kubwa katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Kutokana na juhudi hizo, makusanyo ya ndani kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yaliongezeka kutoka wastani wa Shilingi Bilioni 850 kwa mwezi katika mwaka 2015/2016 hadi Shilingi Trilioni 1.2 kwa mwezi katika mwaka 2016/2017. Pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato, juhudi kubwa zimefanyika kudhibiti matumizi ya rasilimali za umma ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya rushwa, ubadhirifu, wizi na upotevu wa fedha za umma. Mwenendo huo umeiwezesha Serikali kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa kwa fedha za ndani na pia utoaji huduma kwa wananchi. Serikali itaendelea kupanua wigo wa vyanzo vya mapato ya ndani na kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kila anayestahili kulipa kodi aweze kuilipa.  

22.           Mheshimiwa Spika, kuimarika kwa viashiria vya uchumi wa nchi yetu katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani ni dalili njema katika kujenga uchumi imara na tulivu utakaotusaidia kuelekea katika Uchumi wa Viwanda na kufikia nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Serikali itaongeza juhudi katika kuchochea ukuaji wa sekta za kipaumbele zenye fursa kubwa ya kukuza uchumi kwa haraka na kuondoa umaskini kama vile Kilimo na Viwanda. Pia, itahakikisha kwamba sekta wezeshi kama vile Nishati, Habari na Mawasiliano, Fedha na ujenzi wa miundombinu muhimu ya barabara, bandari, reli, vivuko na viwanja vya ndege zinaimarishwa. Vilevile, Serikali itaendelea kuhimiza utekelezaji thabiti wa miradi ya maendeleo na kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji.

Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi


23.  Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwezesha Wananchi kupitia Mipango na Programu mbalimbali kwa kuelekeza nguvu zaidi kwa makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu. Serikali imeweka mazingira bora kwa vikundi vya kiuchumi na vijana kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, SACCOS na VICOBA. Aidha, Serikali imeanzisha majukwaa ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi katika mikoa yote na kufanya mapitio ya Mwongozo wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake wa mwaka 2007. Mapitio hayo yana lengo la kuboresha uendeshaji na usimamizi wa Mfuko huo ili kuwezesha wanawake wengi zaidi kukopesheka.
 
24.    Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba asilimia 56 ya nguvu kazi ya Taifa ni vijana. Hivyo, Serikali inatekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi ili kuwawezesha vijana kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda pamoja na kuinua ari ya vijana kupenda kufanya kazi. Katika mwaka 2016/2017, Serikali inatoa mafunzo kwa  vijana 9,120 katika fani mbalimbali zikiwemo stadi za kushona nguo, kutengeneza bidhaa za ngozi, mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana kwa mfumo usio rasmi na mafunzo ya kukuza ujuzi na stadi za kujiajiri katika fani mbalimbali. Jumla ya vijana 1,469 wamehitimu mafunzo hayo na kupata ajira. Vijana 7,651 waliobaki wanaendelea kupata mafunzo kupitia viwanda vya TOOKU GARMENTS, MAZAVA FABRICS, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), VETA na Don Bosco. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itatoa mafunzo ya kukuza ujuzi wa kujiajiri na stadi za kazi kwa vijana 15,350 katika fani mbalimbali.

25.      Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.5 kwa vikundi vya vijana 297 katika Halmashauri mbalimbali nchini. Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia mapato yake ya ndani zimetoa Shilingi bilioni 4.6 ikiwa ni mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi vya vijana 2,356. Hatua hizi zimekwenda sanjari na utengaji wa maeneo maalum yenye jumla ya ekari 85,603 kwa ajili ya shughuli za vijana za kilimo, biashara ndogo ndogo, burudani na michezo. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kusimamia Halmashauri zote nchini kutenga asilimia tano (5) ya mapato yao kwa ajili ya vijana na asilimia tano (5) kwa wanawake.
 

Ajira na Mahusiano Mahali pa Kazi


26.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu utekelezaji wa juhudi za kukuza ajira nchini kama inavyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. Hadi kufikia Machi 2017, jumla ya ajira 418,501 zimezalishwa nchini. Kati ya ajira hizo, ajira 239,017 sawa na asilimia 57 zimezalishwa katika sekta binafsi wakati ajira 179,484 sawa na asilimia 43 zimezalishwa kutokana na shughuli za sekta ya umma ikiwemo miradi ya maendeleo.

27.      Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 58 ya migogoro ya kikazi inatokana na kutozingatiwa kwa taratibu za kuachisha kazi. Sekta zinazoongoza kwa migogoro ya kazi ni usafirishaji, ujenzi, ulinzi binafsi, elimu, huduma za hoteli na viwanda. Katika kupunguza migogoro mahali pa kazi, Serikali imefanya kaguzi na kusimamia uundwaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi. Aidha, Tume  ya Usuluhishi na Uamuzi imeendelea kutimiza wajibu wake wa kusuluhisha migogoro ambapo katika kipindi cha Julai 2016 hadi Februari 2017, Tume imesajili jumla ya migogoro 8,832 kati ya hiyo migogoro 3,319 sawa na asilimia 37.6 ya migogoro yote iliyosajiliwa imesuluhishwa. Kati ya migogoro hiyo iliyosuluhishwa, migogoro 1,957 ilifikia suluhu (mediation) na migogoro 1,362 haikufikia suluhu. Aidha, migogoro 5,513 inaendelea kusuluhishwa katika hatua mbalimbali.  

Ninatoa wito kwa waajiri na waajiriwa wote nchini, kuzingatia Sheria za Kazi na kuimarisha uhusiano mzuri kwenye maeneo ya kazi, ili muda mwingi zaidi utumike kwenye uzalishaji mali badala ya kutatua migogoro. Vilevile, ni muhimu sana kuimarisha kaguzi za kazi na kuendelea kusaini mikataba ya kuunda na kusajili mabaraza ya wafanyakazi ili kuimarisha zaidi mahusiano mahali pa kazi.

MAENDELEO YA KISEKTA


Sekta za Uzalishaji

Viwanda

28.      Mheshimiwa Spika, ili kujenga uchumi wa viwanda, Serikali inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Viwanda vinavyopewa kipaumbele ni vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa nchini, vinavyotoa ajira kwa watu wengi na vinavyozalisha bidhaa zenye soko hapa nchini na nje ya nchi. Katika kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye uchumi wa viwanda, Serikali inahamasisha zaidi sekta binafsi ya hapa nchini pamoja na mashirika ya umma kujenga viwanda. Jitihada hizo zimewezesha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF, PPF, LAPF, GEPF, PSPF na NHIF kuanza kufufua, kuendeleza na kujenga viwanda vipya vipatavyo 27 katika maeneo mbalimbali nchini. Natoa pongezi kwa Bodi na Menejimenti ya Mifuko hiyo, kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika ujenzi wa viwanda nchini. Aidha, ninaendelea kuyasisitiza mashirika ya umma kuhakikisha kwamba mipango yao inaendana na utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ambao dhima yake ni kujenga uchumi wa viwanda. 

Maliasili na Utalii

29.    Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii ni moja kati ya sekta muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu. Kote ulimwenguni, mafanikio ya sekta ya utalii kwa kiasi kikubwa hutegemea miundombinu thabiti ya utalii, huduma bora na ulinzi na usalama. Ili kuendelea kunufaika na sekta hiyo, Serikali inaboresha miundombinu ya utalii, kupanua wigo wa vivutio vipya vya utalii na kuimarisha huduma ya usafiri wa anga. Vilevile, Serikali inafanya juhudi kubwa za kudhibiti ujangili na biashara haramu ya wanyamapori ambapo watuhumiwa 897 walitiwa mbaroni na kati yao watuhumiwa 282 wamefikishwa Mahakamani.

30.    Mheshimiwa Spika, idadi ya watalii imeongezeka kutoka 1,137,182  mwaka 2015 hadi watalii 1,284,279  mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 12 na kuliingizia Taifa Dola za Marekani bilioni 2. Juhudi zilizoanza za kuliimarisha shirika letu la ndege zinalenga pia kutoa mchango mkubwa kwenye sekta ya utalii kwa kusafirisha watalii wa ndani na kutoka nje ya nchi. Shabaha yetu ni kuongeza idadi ya watalii wanaokuja kutembelea nchi yetu na pia mapato yatokanayo na sekta hiyo. Nitumie fursa hii kuisihi sekta binafsi kuwekeza zaidi kwenye miundombinu muhimu ya sekta hii zikiwemo hoteli, kuboresha huduma na kubuni mbinu mpya za kuvutia watalii.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.