Saturday, April 1, 2017

WAZIRI MKUU AAGIZA DC BAGAMOYO AMALIZE MGOGORO WA ARDHI SAADANI

*Asema waliouza eneo la hifadhi wawajibishwe 
 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Majid Mwanga aende kata ya Saadani na kukaa na uongozi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Saadani ili watambue kwa pamoja mipaka iliyowekwa na Serikali.  
 
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vya Saadani na Matipwili wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani ambao walisimamisha msafara wake wakati akitoka Hifadhi ya Taifa ya Saadani kukagua miundombinu.
 
“Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, Afisa Ardhi njoo na ramani yako na Mhifadhi Mkuu naye aje na ramani yake, kaeni na Mwenyekiti wa Kijiji na kamati yake ya ardhi; muende beacon kwa beacon  kwa kutumia kifaa cha GPS ambacho kitawaongoza kubainisha huo mpaka umepitia wapi. Nahitaji kupata taarifa kuhusu jambo hili kuwa limetekelezwa,” alisema.
 
Alisema anazo taarifa kuwa baadhi watu kwenye kijiji hicho wamewauzia ardhi wakazi kutoka Dar es Salaam wakati wakijua kuwa ardhi hiyo ni mali ya hifadhi ya Saadani. “Hao watu wasakwe na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria kwa sababu hakuna mtu anayeruhusiwa kuuza ardhi ya hifadhi,” alisisitiza.
 
Alisema mikoa, wilaya, vijiji kila kimoja kina mipaka yake ambayo inatambulika na ilikwishatolewa kwenye gazeti la Serikali. “Vijiji vyote vina mipaka ambayo inatambulika rasmi na ramani zake ziko ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kikiwemo na hiki kijiji chenu. Lakini baadhi ya vijiji vina maeneo ya hifadhi. Tunataka mtambue kuwa mipaka hiyo ipo rasmi, na kwamba inapaswa iheshimiwe,” aliongeza.
 
Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao kuwa alilazimika kupita Saadani wakati akitokea Wami, ili aweze kufuatilia ni kwa nini hifadhi hiyo haitangazwi vya kutosha wakati iko karibu na Dar es Salaam na watalii wengi wanapita hapo wakati wakirudi makwao.
 
“Serikali imenunua ndege za kuleta watalii wengi zaidi nchini lakini hadi sasa ni mbuga zilezile ambazo zinapata watalii. Tunataka mbuga hii iliyoko karibu na Dar es Salaam itangazwe na ijulikane zaidi ili wale ambao hawana muda wa kwenda mikoa ya mbali waje hapa na kuona rasilmali tulizonazo,” aliongeza.
 
Hifadi ya Saadani ambayo iko umbali wa km. 45 kutoka Bagamoyo na km. 100 kutoka Dar es Salaam, ina mvuto wa kipekee kwani ndiyo hifadhi pekee unayoweza kuona wanyama wakijivinjari katika fukwe za Bahari ya Hindi kwa vile imeunganisha nyika na bahari.
 
Hifadhi hiyo iko kati ya mikoa ya Pwani na Tanga, katika wilaya za Bagamoyo na Pangani, ikiwa na ukubwa wa zaidi ya km. za mraba 1,000, ikijumuisha maeneo ya Mkwaja na misitu ya Zaraninge na Tumbirini.
 
Katika ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu alikuwa amefuatana na Mkuu wa Mkoa wa Mkoa pwani, Eng. Evarist Ndikilo, viongozi wa wilaya ya Bagamoyo na Mbunge wa jimbo hilo, Ridhiwani Kikwete.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.