Wednesday, May 31, 2017

WAZIRI MKUU AHIMIZA UJENZI WA NYUMBA ZA BEI NAFUU

*Ataka VIGUTA iende kwenye halmashauri, ihamasishe watumishi
*Asema Watanzania wanataka nyumba bora, hawana muda wa kusimamia ujenzi
          
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri za wilaya nchini ziangalie uwezekano wa kuwapatia watumishi wake nyumba za bei nafuu kwa malipo kidogo kidogo.

Amesema Halmashauri za wilaya kupitia mapato ya ndani, japo si makubwa zinaweza kuandaa mazingira yatakayowawezesha watumishi wake kupata nyumba kupitia mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu unaofanywa na Muungano wa Vikundi vya Vicoba Tanzania (VIGUTA).

Ametoa wito huo leo (Jumatano, Mei 31, 2017) mara baada ya kutembelea maonyesho ya Mpango wa Ujenzi wa Nyumba za Waheshimiwa Wabunge (Low Cost Housing) yanayoendelea kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma. 
         
Waziri Mkuu aliwashauri  viongozi wa VIGUTA wafanye mawasiliano na Halmashauri zote na akawataka watenge muda wa kuzitembelea  Halmashauri hizo ili kuonyesha nia na uwezo wao wa kujenga nyumba za gharama nafuu ambazo malipo yake hulipwa kidogo kidogo kwa lengo la kuboresha maisha ya Watanzania.

“Watanzania wengi hivi sasa wanapendelea nyumba ndogo, nzuri na ambazo zimekamilika. “Wengi wao, na hasa wafanyakazi, siku hizi wana shughuli nyingi na hawana muda wa kujenga nyumba na kuzisimamia wenyewe kama zamani. Hivyo, wanahitaji makampuni yanayoweza kuwanjengea nyumba na wao wakalipa kidogo kidogo,” amesisitiza.
         
Aliwaaasa viongozi wa VIGUTA wahakikishe kuwa wanajenga nyumba zenye ubora unaokubalika ili waweze kuaminika hali ambayo itawawezesha kupata wateja wengi zaidi.

“Katika kipindi hiki ambacho Serikali inahamia Dodoma, Muungano wa Vikundi vya VICOBA au VIGUTA unayo nafasi kubwa ya kuwapatia watumishi wanaohamia nyumba za kuishi kupitia mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu,” Waziri Mkuu alisema.

Alisema watumishi wengi wanaoingia gharama kubwa kwa kuishi katika nyumba za kupanga huku wakilipa kodi, sasa wamepata kimbilio kwani  wanaweza kujengewa nyumba kwa muda mfupi na kwa bei nafuu na wakalipa kidogokidogo kwa kipindi cha hadi miaka 15.

Naye, Mwenyekiti wa VIGUTA Taifa, Dkt. Salmin Ibrahim Dauda alimweleza Waziri Mkuu kwamba wana uwezo wa kujenga nyumba kwa gharama ya shilingi milioni 12, milioni 15, milioni 25 na milioni 60 kutegemeana na ukubwa wa nyumba.

Alisema wameweka viwango tofauti ili kuwawezesha Watanzania wenye kipato cha chini kumiliki nyumba zao wenyewe.

(


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.