*Serikali kugawa salpha bure kwa wakulima wa korosho
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kuhakikisha wanafanya marekebisho ya mizani katika maghala ya kuhifadhia korosho ili kuepuka changamoto ya kutofautiana kwa uzito wa bidhaa hiyo kila inapofikishwa kutoka katika vyama vya msingi.
Amesema kitendo cha mizani za kwenye maghala hayo kupunguza uzito wa korosho zinazopelekwa kutoka kwenye Chama cha Ushirika cha Msingi (AMCOS) hakivumiliki, hivyo Wakala wa Vipimo ipendekeze aina ya mizani zitakazotumika katika upimaji wa korosho.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Mei 13, 2017) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wadau wa Tasnia ya Korosho uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mjini Dodoma.
“Kuna jambo baya sana linaendelea kila korosho inayofikishwa katika ghala kuu lazima kilo ziwe zimepungua kwa zaidi ya kilo mia moja mpaka elfu, kwa nini korosho tani kumi zikiletwa kwenye mizani yenu zinasoma tani nane kwa nini?
“Na huwa haitokei ikasoma tani kumi na mbili, wakati wote huwa inasoma chini tu, watu wa WMA mpo fanyesni marekebisho, haiwezekani tukavumilia wizi huu. Huna mkorosho hata mmoja lakini mwaka huu utasikia umeuza tani zaidi ya elfu tano.
Jambo hili lisijitokeze tena,” amesisitiza.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuimarisha na kuboresha utaratibu wa stakabadhi ghalani na kupambana na biashara ya kangomba, hivyo viongozi wa Mikoa inayolima korosho wahakikishe wanawashughulikia watu wote watakaobainika kushiriki kwenye biashara hiyo bila ya kujali wadhifa wao.
Amesema mwelekeo wa Serikali kwenye sekta ya kilimo ni kuhakikisha kuwa kilimo kinakuwa sehemu muhimu ya kuimarisha uchumi, kuongeza kipato cha mkulima na kuchochea ukuaji wa viwanda ili kuongeza ajira.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba amesema takwimu zilizotolewa na Benku Kuu ya Tanzania (BoT) mwezi Februari mwaka huu, zinaonyesha zao la korosho linaongoza kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni. Zao la korosho limeliingizia Taifa Dola milioni 346.6, likifuatiwa na zao la tumbaku dola 276 na kahawa dola 152.9.
“Zao la korosho linakuwa zao kuu la biashara nchini na tayari mikoa ya Dodoma, Morogoro, Iringa, Njombe na Mbeya imeanza kulima, hivyo kuongeza idadi ya mikoa inayolima zao hilo nchini na kufikia 11 na wilaya 40,” amesema.
Aidha, Dkt. Tizeba ameitaka Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kuhakikisha inakuwa makini na viuatilifu vinavyoingizwa nchini kwa kuvipima kwa kutumia wataalamu wa Serikali ili kujiridhisha ubora wake kabla ya kuwafikishia wakulima.
Pia Dkt. Tizeba amesema katika msimu wa mwaka huu Serikali itagawa salpha bure kwa wakulima wa zao la korosho kwa ajili ya kupuliza kwenye mikorosho yao ili isishambuliwe na wadudu.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.