Friday, May 5, 2017

WAZIRI MKUU ANUNUA HISA ZA VODACOM


*Awasihi wananchi wote wanunue hisa kabla muda haujaisha
*Asema wajasiriamali, wakulima, wafugaji na wavuvi wana fursa sawa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amenunua hisa za kampuni ya Vodacom Tanzania Plc zenye thamani ya sh. milioni 10 pamoja na nyingine za sh. milioni 10 kwa ajili ya mke wake, Mary Majaliwa.

Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo leo hii (Ijumaa, Mei 5, 2017) wakati akizungumza na waandishi wa habari mbele ya wakuu wa Masoko ya Hisa na Dhamana; Soko la Hisa la Dar es Salaam, viongozi wa Baraza la Uwezeshaji na kampuni ya Vodacom katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amewasihi Watanzania walioko ndani na nje ya nchi wachangamkie fursa ya kununua hisa hizo ili waweze kuwa wamiliki wa kampuni kupitia hisa zao. “Hii ni fursa kwa Watanzania kumiliki kampuni. Ukinunua hisa, unashiriki kikamilifu kumiliki kampuni na pia unaboresha uchumi wako binafsi. Ninawasihi Watanzania wote tumieni fursa hii kununua hisa hizo kabla muda haujaisha,” alisisitiza.

Alisema watumishi wa umma wamepewa ya kununua hisa hizo kupitia mipango iliyowekwa na Makatibu Wakuu wao lakini pia amewasihi viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi wachangamkie fursa hiyo ili nchi iweze kupata kodi kupitia makampuni hayo.

“Hii ni fursa kwa kila Mtanzania, kwa viongozi kwa taasisi na mashirika ya umma, taasisi binafsi, wajasiriamali wadogo kama akinamama lishe au madereva wa bodaboda. Watanzania walioko nje ya nchi (Diaspora) nao pia wanunue hisa kwani watakuwa wanachangia uchumi wa nchi na wakati huo wanaweka akiba nyumbani,” aliongeza.

Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango uwekezaji kwenye hisa ni njia mojawapo ya kuwawezesha Watanzania kumiliki uchumi wa nchi.

“Huko mtaani ukisema uchumi wa nchi unakua, watu wanabisha wakidai kuwa hawaoni unakua kwa sababu hawana fedha mifukoni. Hii ni fursa nyingine ya kuwawezesha kukua kiuchumi, ninaomba waichangamkie,” alisema.

Alisema sekta ya mawasiliano ni miongoni mwa sekta inayokua kwa kasi hapa nchini kwani katika robo tatu ya mwaka, sekta hiyo imekua kwa asilimia 11.3. “Niwasihi Watanzania wenzangu, tununue hisa za Vodacom ili tuweze kuboresha uchumi wetu,” alisema.

Alisema anatoa ombi maalum kwa wafugaji kukubali kuuza mifugo yao na kununua hisa ili kupunguza idadi ya mifugo yao, jambo ambalo alisema litapunguza migogoro baina yao na wakulima.

“Wakulima wa vitunguu, alizeti, maua au wafugaji wa samaki nao pia wanaweza kununua hisa na kuwa na mitaji kwa ajili ya shughuli zao. Ninawasihi wote watumie fursa hii ili kumiliki kampuni,” alisema.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana, Bi. Nassama Masinda alisema amefurahishwa kuona Waziri Mkuu akinunua hisa za kampuni ya Vodacom katika soko la awali.

Alisema uuzwaji wa hisa hizo ni utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 kwa lengo la kuwawezesha Watanzania kuwa wamiliki wa makampuni ya simu za mikononi hapa nchini. “Marekebisho ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta sura ya 306 yanazitaka kampuni za simu na mawasiliano ya kielektroniki kuuza si chini ya asilimia 25 ya hisa zao kwa umma wa Tanzania kupitia masoko ya mitaji (IPO).”

Alisema baada ya hapo hisa hizo zinapaswa kuorodheshwa kwenye soko la Hisa la Dar es Salaam baada ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, sura ya 79. Kampuni ya Vodacom ilitoa hisa milioni 560 kwa umma kwa bei ya sh. 850 kila moja na hivyo kutarajia kukusanya sh. bilioni 476.

Alisema hivi sasa, wawekezaji kwenye masoko ya mitaji ni watu 500,000 tu ikilinganishwa na Kenya ambayo ina wawekezaji milioni 1.7; Uganda (40,000) na Rwanda (14,000). “Vodacom ina wateja milioni 6.2, iwapo nusu ya wateja wake wote watashiriki ununuzi wa hisa, idadi ya wawekezaji kupitia masoko ya mitaji na dhamana itaongezeka kwa asilimia 1,140. Na haya yatakuwa ni mageuzi makubwa katika sekta ya masoko ya mitaji si hapa nchini tu bali katika Afrika Mashariki,” alisema.

Mtendaji Mkuu wa Dodacom, Bw. Ian Ferrao alisema mauzo ya hisa yanayofanywa na kampuni hiyo ni makubwa mara nne ya mauzo ambayo yamewahi kufanyika hapa nchini.

Alisema kampuni hiyo ambayo imekwishafanya kazi kwa miaka 17 hapa nchini, imewekeza zaidi ya sh. trilioni mbili katika mtandao wa mawasiliano nchini Tanzania.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.