Thursday, May 4, 2017

WAZIRI MKUU AIOMBA ROTARY CLUB ISAIDIE KUKABILIANA NA MALARIA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akivishwa beji ya uanachama wa Rotary Club na Dk. Manoj Desai kwenye mkutano wa 92 wa mwaka unaojumuisha nchi za Uganda na Tanzania (District 9211) katika ukumbi wa AICC jijini Arusha Mei 4, 2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifungua mkutano wa 92 wa mwaka wa Rotary unaojumuisha nchi za Uganda na Tanzania  (District 9211) katika ukumbi wa AICC jijini Arusha Mei 4, 2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Rotary Club kwenye mkutano wa 92 wa mwaka unaojumuisha nchi za Uganda na Tanzania (District 9211) katika ukumbi wa AICC jijini Arusha Mei 4, 2017.
*Awa mwanachama wa 651 kujiunga na klabu hiyo, mkewe pia ajiunga
*Aaahidi kushawishi viongozi wa Serikali na wabunge wajiunge kwa wingi
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Klabu ya Rotary nchini uangalie uwezekano wa kuisaidia Serikali kupambana na ugonjwa wa Malaria. 

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye leo hii (Alhamisi, Mei 4, 2017) amekuwa mwanachana wa 651 kujiunga na klabu hiyo,  ametoa wito huo wakati akifungua mkutano wa 92 wa mwaka wa Rotary unaojumuisha nchi za Uganda na Tanzania (District 9211) katika ukumbi wa AICC jijini Arusha. 

"Ninatambua kazi nzuri inayofanywa na Rotary Club katika kuisaidia jamii kwa vile na mimi mwenyewe nimekuwa nikisaidia jamii. Kwa hiyo mimi na mke wangu Mary Majaliwa tunajiunga tukiwa ni wanachama wa 651 na 652 ili kuongeza nguvu ya Rotary kusaidia jamii," alisema huku akishangiliwa na washiriki zaidi ya 1,000 waliohudhuria mkutano huo kutoka Uganda, Tanzania, India, New Zealand na Australia. 

Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa klabu hiyo uongeze mikakati ya kutangaza kazi wanazozifanya ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa watu wengi kwamba wanaojiunga na klabu hiyo ni watu matajiri na watu maarufu. 

"Kazi mnazozifanya ni kubwa na nzuri mno kwa jamii. Lakini itabidi mjitangaze zaidi ili watu wengi zaidi watambue kazi zenu na waweze kuwaunga mkono," alisema. 

Waziri Mkuu aliahidi kuwashawishi viongozi wengine wa Serikali, taasisi za umma pamoja na Wabunge wajiunge kwa wingi na klabu hiyo. Tanzania ina klabu za Rotary 36 zenye wanachama 650 wakati Uganda ina klabu za Rotary 93 zenye wanachama 2,700. Tanzania na Uganda zinaunda District 9211 katika mfumo wa kimataifa wa rotary.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwapongeza wana-Rotary kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusaidia jamii hasa kwenye sekta za maji, elimu, na afya.

Alisema Rotary inatambulika duniani kwa kampeni yake ya kutokomeza ugonjwa wa polio; na kupitia michango ya wana-Rotary, Tanzania hivi sasa haina mgonjwa yeyote wa polio.

"Licha ya uchache wenu, natambua mchango mkubwa unaotolewa na Rotary Club hapa nchini. Hivi karibuni, Rotary Club saba ziliungana na Benki M na kujenga hospitali kubwa ya watoto pale Muhimbili (MNH) na Kituo cha Ujasiriamali kwa Vijana pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)," alisema. 

"Miradi mingine inayofadhiliwa na Rotary Club ni ujenzi wa hospitali ya akinamama wajawazito mkoani Dodoma, utoaji wa vitabu vya ziada 20,000 kwenye shule za sekondari zaidi ya 40 mkoani Tanga pamoja na miradi ya maji safi kwenye  wilaya za Same na Mwanga mkoani Kilimanjaro. 

Kwa upande wake, District Gavana wa Rotary 9211 ambaye anamaliza muda wake, Bw, Jayesh Asher wana-Rotary duniani wanaamini kwamba Serikali za nchi mbalimbali haziwezi kutekeleza majukumu yote kwa wananchi wake kwa hiyo wanajiunga na kutoa rasilmali zao ili kusaidia jamii zenye uhitaji.

Akizungumzia kuhusu uchahe wa wanachama hapa nchini, Bw. Asher alisema Rotary Club ya Uganda imepata umaarufu kwa sababu viongozi wengi wamejiunga na klabu hiyo wakiwemo Mawaziri, Spika wa Bunge la Uganda, wabunge na mabalozi.

“Hapa Tanzania itabidi tutangaze zaidi kazi zetu ili tuweze kuwavuta viongozi wa kisiasa na wa umma na pia kuongeza wanachama zaidi,” alisema.

Mkutano huo wa siku tatu, utamalizika Juni 6, mwaka huu.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.