Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri
wenye dhamana ya Menejimenti ya Maafa
kwa Nchi wanachama wa SADC, wakifuatilia mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020,
Zanzibar.
|
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri
wenye dhamana ya Menejimenti ya Maafa
kwa Nchi wanachama wa SADC, wakifuatilia mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020,
Zanzibar.
|
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri
wenye dhamana ya Menejimenti ya Maafa
kwa Nchi wanachama wa SADC, wakifuatilia mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020,
Zanzibar.
|
Na. OWM, ZANZIBAR
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein amesema
maeneo ya visiwa yapo katika hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na maafa ukilinginisha na
maeneo mengine duniani, hivyo alitoa wito kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC) kuja na mikakati imara itakayoainisha mbinu za kutambua na
kuwahi viashiria vya maafa kabla madhara hayajatokea.
“Tuna jukumu la
kuendelea kushirikiana kati ya Serikali zetu, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na
Kimataifa, Taasisi za Utafiti, Sekta Binafsi, Taasisi za Kidini, Taasisi za
Fedha na Mashirika yasiyo ya Serikali,
Asasi za Kiraia na Vyombo vya Habari katika suala hili. Tukifanya hivyo,
itakuwa tumeitekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya mkutano huu isemayo: “Ushiriki wa kisekta kwenye kupunguza madhara
ya maafa ni njia bora ya kujenga uhimili katika ukanda wa nchi wanachama wa
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.”
Rais
Shein amesema hayo leo tarehe 21, Februari, 2020 Zanzibar alipokuwa anafungua kikao
cha Mawaziri wa nchi za SADC wenye Dhamana ya Menejimenti ya Maafa.
Rais
Shein ameeleza kuwa maafa yana madhara makubwa katika nchi, endapo hakutakuwa
na mipango thabiti ya kukabiliana nayo na kutolea mfano namna vimbunga vya Idai,
Kenneth na vinginevyo vilivyosababisha vifo, uharibifu wa mali na miundombinu katika
nchi za Malawi, Zambia, Zimbawe, Msumbiji na Comoro.
Rais
Shein amefafanua kuwa maafa yanabadilisha agenda za maendeleo ya nchi mbali mbali
duniani kwa sababu fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo
zinabadilishwa matumizi kukidhi dharura za maafa kwa gharama kubwa zaidi.
Akitoa
mfano wa mpango wa Sendai wa kukabiliana na maafa ambao unaonesha kati ya mwaka
2015 hadi 2018 nchi za Afrika zimekubwa na matukio 160 ya maafa ambayo yamesababisha
uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu. Ameeleza kuwa mpango huo unaonesha kuwa
zinahitajika Dola za Marekani bilioni 3700 ili nchi zilizoathirika ziweze kurejesha
hali yake ya kawaida. “Kiasi kikubwa hiki cha fedha kinatumika kujenga upya miundombinu
iliyoharibika badala ya kujenga miundombinu mipya”, Rais Shein alisema.
Rais
wa Zanzibar amewambia wajumbe wa mkutano huo hatua zilizo fanywa na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha uhimili wa kukabiliana na maafa, kwa
kuzingatia kuwa Zanzibar ni miongoni mwa visiwa ambavyo hupata madhara ya
maafa.
Hatua
hizo ni pamoja na kuandaa Sera ya kukabiliana na maafa ya mwaka 2011 na sheria yake
ya mwaka 2015, kuanzisha Kamisheni inayoshughulikia masuala ya maafa na mpango
wa mawasiliano wakati wa maafa.
Aidha, amebainisha hatua nyingine kuwa ni pamoja na mpango wa elimu ya kujikinga
na maafa kwa wanianchi, kuimarisha vyombo vya usafiri wa baharini ikiwemo ununuzi
wa meli mbili kubwa za MV. Mapinduzi II ya abiria na MV. Ukombozi II kwa ajili ya
kubeba mafuta, ujenzi wa vituo vitatu vya uokozi, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya
kufuatilia usafiri wa majini ikwemo ndege zisizokuwa na rubani na boat za uokoaji
na kuzimia moto.
Dkt.
Shein amesema ili kukabiliana na maafa ya mafuriko ambayo huwa yanakikumba kisiwa
hicho kutokana na mvua za mwezi Oktoba hadi Desemba na mwezi Machi hadi Juni,
nchi hiyo kwa msaada wa Serikali ya Falme za Kiarabu (UAE) imejenga kituo cha
kuhifadhi watu wanaoathirika na mafuriko ambacho kina nyumba 30 zenye miundombinu
yote kwa ajili ya maisha ya mwanadamu.
Aidha,
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua mkopo wa Dola za Marekani milioni 93
kwa ajili ya ujenzi wa mitaro inayopeleka maji baharini wakati wa mafuriko.
Ujenzi huo ambao upo katika hatua za mwisho utakapokamilika, Dkt. Shein aliwahakikishia
wajumbe wa mkutano huo kuwa, Zanzibar itaweza kuepuka mafuriko au Kupunguza kwa
kiasi kikubwa.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Jenista Muhagama (Mb)ameeleza kuwa malengo ya kuanzishwa kwa Kamati ya Mawaziri wenye Dhamana ya Maafa likiwemo
lengo la kulishauri Baraza la Mawaziri wa nchi za SADC namna ya kupunguza madhara
ya maafa. Alisema maafa yaliyosababishwa na majanga ya vimbunga vya Idai na Kenneth
katika nchi za SADC, ukame na mafuriko ambayo hayana mipaka yamedhihirisha umuhimu
wa nchi hizo kuwa na mpango wa ushirikiano wa kukabiliana na maafa.
Alieleza
ili kwenda sambamba na juhudi za kikanda na kimataifa, Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Mhe. Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli itaendelea kuimarisha uwezo
wake wa usimamizi wa maafa katika Nyanja zote.
Amebainisha hatua zilizochukuliwa na
zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ni pamoja na kuandaa Mkakati wa Taifa wa
Kupunguza Madhara ya Maafa; kuandaa Wasifu wa Janga la Mafuriko na Ukame;
kuandaa Mpango wa Dhamira ya Taifa wa Utekelezaji wa Makubaliano ya Paris
kuhusu mabadiliko ya tabianchi; kuandaa Mfumo wa Taifa wa Ufuatiliaji wa
Taarifa za Gesi Joto; Kuandaa Mipango ya
Kukabiliana na Dharura za Afya ya Binadamu, Mifugo na Wanyama; kuandaa Mkakati
wa Taifa wa Usimamizi wa Mazao baada ya Kuvuna.
Naye
Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena Tax aliwambia wajumbe wa mkutano huo kuwa
majanga hayataki urasimu yanapotokea, yanahitaji hatua za haraka na zinazoeleweka
ili kuyakabili ipasavyo kabla hayajasababisha madhara makubwa.
Dkt.
Tax alifafanua kuwa mkutano huo kufanyika Zanzibar ni fursa nzuri kwa nchi za
SADC kujua vizuri muungano wa Tanzania na Zanzibar ambao umedumu kwa miaka mingi
sasa. Aidha, alisema itakuwa fursa nzuri kwa nchi hizo kujionea vivutio vya kipekee
vya kisiwa cha Zanzibar ambacho kina umaarufu mkubwa duniani kote.
Serikali ya Tanzania imekuwa mwenyeji wa
Mkutano wa Kwanza wa Kamati ya Mawaziri wanaohusika na Menejimenti ya Maafa kwa
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika baada ya Tanzania
kuchukua rasmi nafasi ya Mwenyekiti wa jumuiya kuanzia mwezi Agosti, 2019 kwa
kipindi cha mwaka mmoja hadi mwezi Agosti, mwaka huu (2020). Hatua hii inatokana na utaratibu wa kawaida
wa mzunguko wa kushika nafasi hiyo kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa
jumuiya hiyo.
MWISHO.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.