Sunday, February 16, 2020

MAWAZIRI WENYE DHAMANA YA MENEJIMENTI YA MAAFA KWA NCHI ZA SADC KUKUTANA ZANZIBAR

Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Zanzibar, Makame Khatibu Makame akitoa Ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa kuhusu  Mkutano wa kwanza wa Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya menejimenti ya Maafa kwa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika tarehe 16 Februari, 2020, Ukumbi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Mnazi mmoja.

 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud Mohamed akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa kwanza wa Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi Wanachama  Jumuiya ya MaendeIeo Kusini mwa Afrika, tarehe 16 Februari, 2020, Ukumbi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Mnazi mmoja.
Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia Mkutano wa Waandishi wa Habari na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud Mohamed (hayupo pichani) wakati wa akifafanua kuhusu Mkutano wa  kwanza wa Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi Wanachama  Jumuiya ya MaendeIeo Kusini mwa Afrika, tarehe 16 Februari 2020, Ukumbi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Mnazi mmoja.

Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia Mkutano wa Waandishi wa Habari na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud Mohamed (hayupo pichani) wakati wa akifafanua kuhusu Mkutano wa  kwanza wa Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi Wanachama  Jumuiya ya MaendeIeo Kusini mwa Afrika, tarehe 16 Februari 2020, Ukumbi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Mnazi mmoja.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu Wananchi,
Kama tunavyoelewa kuwa kufuatia Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika mwezi Agosti 2019 ambapo, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokea rasmi uenyekiti wa jumuiya hiyo, hali hiyo imepelekea mkutano mbalimbali ya  Kisekta kufanyika hapa Tanzania.
Ndugu Wananchi,
Mkutano huu unafanyika kutokana na umuhimu mkubwa wa Mawaziri wa nchi wanachama wa SADC wanaohusika na masuala ya maafa kukutana kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya namna bora ya kukabiliana na matukio ya  maafa yanayoukabili ukanda huu yakiwemo vimbunga, mafuriko, ukame, na hata ajali za baharini ambayo yamekuwa yakisababisha athari kubwa kwa maisha ya watu na mali.

Sote ni mashuhuda athari za Kimbunga Idai na Keneth vilivyotokea katika nchi za Madagascar, Malawi, Msumbiji na Zimbabwe vilipelekea vifo vya maelefu ya watu na wengine kutoonekana kabisa na kupelekea  mahitaji ya kiasi cha dola bilioni 10 za Kimarekani kwa ajili ya kurejesha hali.

Ndugu Wananchi,
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kwanza wa Kamati ya Mawaziri wanaohusika na Menejimenti ya Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika utakaofanyika katika hoteli ya Madinat Al Bahri Mbweni, tarehe 18 – 21 Februari, 2020,  hapa Zanzibar. ambapo Kaulimbiu ya Mkutano huu: “Ushiriki wa Kisekta kwenye Kupunguza madhara ya maafa ni njia bora ya kujenga uhimili katika ukanda wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika” (SADC)

Ndugu Wananchi,
Mkutano huu unakuja kipindi ambacho nchi nyingi wanachama katika ukanda huu zimekuwa zikiathiriwa na majanga ya asili mara kwa mara na kusababisha madhara makubwa. Hali iliyoonesha wazi umuhimu wa mashirikiano ya kikanda katika kukabiliana na maafa  ili kupunguza athari za maafa, kukuza uwezo wa kujiandaa  na kukabiliana kwani mara nyingi athari zinazotokana na majanga ya kimaumbile yakiwemo ukame, mafuriko, maradhi ya mlipuko na mengineyo, hupelekea vifo kuharibu miundombinu muhimu ikiwemo barabara na hudumaza msingi za jamii kama vile afya na elimu na kupelekea gharama kubwa  katika kurejesha hali baada ya maafa kutokea.
Ndugu Wananchi,
Katika hatua ya kujenga mataifa yenye uhimili katika kukabiliana na maafa, SADC imefanikiwa katika kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema inayoendana na majanga ya Hali ya  hewa, kuandaa vikao vya mwaka kwa nchi wananchama  kwa ajili  ya kujikinga, kujiandaa na kukabiliana na maafa pamoja  na kuandaa mipango ya dharura na kutoa mafunzo ya utafutaji na uokozi kwa majanga ya baharini kwa nchi wananchama.
Ndugu Wananchi,
SADC imetekeleza program ya ufanyaji wa tathmini na uchambuzi wa usalama wa chakula kwa nchi wananchama 14 zilizoathiriwa na majanga yanayoendana na hali ya hewa yakiwemo ukame, imeandaa mpango na mkakati wa pamoja kwa ajili ya kujikinga na kukabili maafa. Mikakati yote hiyo ni kwa ajili ya kupunguza athari za maafa katika kanda hii. Mnamo mwaka 2017-2018 takribani watu wapatao milioni 7 waliathiriwa na maafa idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na watu milioni 17 walioathirika katika miaka ya 2015-2016.
Kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekamilisha kuandaa nyaraka zote muhimu katika masuala ya kukabiliana na maafa ikiwemo sheria ya Usimamizi wa Maafa ya Kitaifa Na. 7 ya 2015, Sheria ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar No. 1 ya mwaka 2015, Sera za Kukabiliana na Maafa, Mipango ya Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa na Mkakati wa Mawasiliano Wakati wa Maafa na rasimu ya Mkakati wa Kukabiliana na Maafa pamoja kuanzisha vituo vya mawasiliano na operesheni za dharura na vituo vya uokozi hasa kwa majanga ya baharini.
Mkutano huu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika unalenga katika kushajihisha juhudi zilizopo katika kukabiliana na maafa kwa kuziwezesha nchi wanachama kuandaa mikakati ya uhimili kutokana na athari za maafa, kuandaa mkakati wa kujiandaa na kukabiliana na maafa. Aidha, mikakati hii itaisaidia sana juhudi za ukanda huu katika kupunguza athari za maafa na kuimarisha uwezo wa nchi husika katika kukabiliana na maafa pamoja na kurejesha hali baada ya maafa kutokea.

Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kuwakaribisha waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kufuatilia juu ya Mkutano huu ambao utakuwa ni fursa tosha ya kutangaza utalii wetu na kukuza uchumi wan chi pamoja na kupunguza athari za maafa.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Mhe. Mohamed Aboud Mohamed
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa wa Pili wa  Rais Zanzibar
EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.