Katibu
Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim
Yonazi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa inayosimamia na kuratibu
fedha za Global Fund inayojulikana kama Tanzania National Coordinating
Mechanism – (TNCM) ameongoza Kikao cha (TNCM) kilichofanyika katika Ukumbi wa
Serengeti, Jengo la FCC, jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, mambo mbalimbali
yamejadiliwa ikiwemo maandalizi ya awali ya kuandaa andiko la maombi ya
ufadhili wa awamu ya nane ya Mfuko wa Dunia (Global Fund Grant Cycle 8 - GC8).
Aidha, Dkt. Yonazi amesisitiza umuhimu wa kuwa na mipango madhubuti na yenye
tija ili kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na rasilimali hizo katika
mapambano dhidi ya magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu, na Malaria, pamoja na
kuimarisha mifumo ya afya kwa ujumla.
Akifunga
mkutano huo, Dkt. Yonazi amewahimiza wajumbe na wadau wote kuendeleza
ushirikiano na uwazi (Transparency) katika hatua za maandalizi ya GC8, huku
akibainisha kuwa ufanisi wa (TNCM) unategemea sauti ya pamoja ya wadau wote
wanaowakilishwa.
Mkutano
huo uliowahusisha wadau kutoka Serikalini, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia, na
Washirika wa Maendeleo, umelenga kujadili masuala mtambuka ya uendeshaji wa
taasisi hiyo pamoja na kuweka misingi imara ya upatikanaji wa rasilimali katika
sekta ya afya nchini.
Mbali na hayo,
katika mkutano huo, wajumbe walimchagua Bw. Godlisten Moshi kuwa Makamu
Mwenyekiti mpya wa (TNCM) ili kukamilisha safu ya uongozi na kuongeza ufanisi
katika utendaji wa chombo hicho.


EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.