WASIFU
WA ALIYEKUWA WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, URATIBU NA WENYE
ULEMAVU MAREHEMU WILLIAM VANGIMEMBE LUKUVI
KUZALIWA
Mheshimiwa
William Vangimembe Lukuvi alizaliwa tarehe 15 Agosti 1955 katika kijiji cha
Mapogoro, Kata ya Idodi - Wilaya ya Iringa Vijijini, Mkoani Iringa.
Marehemu
William Vangimembe Lukuvi alikuwa mwanasiasa mashuhuri alieshika nyadhifa
mbalimbali za uongozi na aliesifika kwa ubunifu, uthubutu, uchapakazi,
uzalendo, mwenye uwezo wa kujitoa na kujituma katika kazi na aliweka maslahi ya
Taifa mbele na wakati wote aliamini katika matokeo chanya katika utekelezaji wa
shughuli mbalimbali za Serikali. Alijulikana kwa mtindo wake wa kazi wa
kutembelea maeneo ya miradi na kusikiliza kero za wananchi moja kwa moja, jambo
lililosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za Serikali.
Katika kudhihirisha uchapakazi wake, siku moja kabla ya umauti kumkuta,
marehemu alihudhuria na kuratibu Serikali katika Vikao vya Kamati za Kudumu za
Bunge pamoja na kutoa maelekezo mbalimbali ya Serikali.
ELIMU
Marehemu
William Vangimembe Lukuvi alipata elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi
Kitanewa kuanzia mwaka 1962 hadi 1970. Alijiunga na Chuo cha Ualimu Tabora
(TTC) kuanzia mwaka 1974 – 1975 ambapo alihitimu na kutunukiwa Cheti cha
Ualimu. Mwaka 1982- 1983 alijiunga na Shule ya Komsomol High School, Moscow
nchini Urusi na kutunukiwa Stashahada ya Juu ya Sayansi ya Siasa (Advanced
Diploma in Political Science). Alipata Shahada ya Masuala ya Kimatiafa na
Diplomasia yaani Bachelor of Arts in International Studies and Diplomacy kutoka
Washington International University kuanzia mwaka 1999 – 2001, na baadaye
alijiendeleza kimasomo katika ngazi ya shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu
Huria Tanzania ambapo alihitimu na kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika Sayansi
ya Siasa mwaka 2008 – 2011.
KAZI
NA SIASA
Marehemu
William Vangimembe Lukuvi alianza safari yake ya kisiasa mwaka 1973 alipojiunga
na Chama cha TANU akiwa mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Tabora (TCC) na
kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama katika chuo hicho mwaka 1974 - 1975.
Mnamo mwaka 1984 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Vikao vya umoja wa Vijana wa CCM
katika Ngazi ya Wilaya hadi Taifa. Alichaguliwa kuwa Katibu wa Mkoa na Wilaya
wa chama cha CCM mwaka 1980 – 1984. Vile vile, aliteuliwa kuwa Naibu Katibu
Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM mwaka 1993 – 1994. Aidha, Alichaguliwa kuwa
Mjumbe wa Halmashuari Kuu ya CCM na Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Chama mwaka
2010 hadi sasa.
Marehemu
William Vangimembe Lukuvi aliajiriwa kama Mwalimu katika Wizara ya Elimu
kuanzia mwaka 1975 hadi 1980.
Aliteuliwa
kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba kuanzia mwaka 1994 – 1995, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
2006 – 2008 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam 2008 - 2010.
Katika
uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya Siasa nchini uliofanyika mwaka 1995,
Marehemu Lukuvi alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Isimani na hivyo kuwa
mbunge wa kwanza wa jimbo hilo alilolitumikia kwa takribani miaka 30 hadi
umauti ulipomkuta. Akiwa mbunge aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuanzia Mwaka 2005 – 2010.
Katika
maisha yake ya siasa, Marehemu Lukuvi aliingia katika Baraza la Mawaziri kwa
mara kwanza alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Vijana na Ajira mwaka 1995 –
2000, na baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu na Mnadhimu Mkuu wa Serikali (Chief
Whip) kati ya mwaka 2000 – 2005, 2010 – 2015 na 2025 - 2026.
Halikadhalika,
Marehemu Lukuvi aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi Nyumba, na Maendeleo ya Makazi
kuanzia Januari, 2015 hadi mwaka 2022.
Aidha,
mnamo Juni 2023, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania alimteua kuwa Mshauri wa Rais kuhusu Mahusiano ya Kisiasa na Kijamii.
MAFANIKIO
KATIKA SEKTA ALIZOONGOZA KIPINDI CHA UTUMISHI WAKE
Akiwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu),
Alikuwa
msimamizi mahiri wa shughuli za Serikali Bungeni na alifanikiwa kuimarisha
mahusiano kati ya Serikali na Bunge, jambo ambalo lilimfanya kuwa mmoja wa
Mawaziri wenye ushawishi mkubwa katika awamu mbalimbali za uongozi, na kujenga
daraja imara kati ya Serikali, Bunge na wananchi.
Alisimamia
utekelezaji wa sera mbalimbali zilizolenga kuboresha ustawi wa wenye ulemavu
akihamasisha ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika fursa za kiuchumi na
ajira na kusisitiza kuwa kundi hili ni sehemu muhimu ya nguvu kazi ya taifa.
Alisimmamia
kikamilifu Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma ambao hadi sasa
umefikia wastani wa asilimia 93 na tayari Wizara 15 zimeshahamia katika mji huo
na zinatoa huduma kwa umma kutoka hapo.
Alisimamia
uimarishaji wa mifumo ya kisera kwa kufanya maboresho katika usimamizi wa maafa
nchini ikiwemo Mfumo wa Taarifa wa kielektroniki wa Usimamizi wa Maafa
(Disaster Management Information System - DMIS), hatua iliyosaidia kupunguza
Athari za maafa nchini.
Alikuwa
mstari wa mbele kwa kuhakikisha Wizara zote zinafanya kazi kwa ushirikiano ili
kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuhakikisha
ahadi za serikali kwa wananchi zinatekelezwa.
Akiwa
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Alifanikiwa
kutatua migogoro ya ardhi nchini kwa kuanzisha mifumo bora ya kutatua migogoro
ya ardhi na kupeleka huduma bora na zilizo karibu na wananchi.
Alisimamia
uanzishwaji wa mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa ardhi iliyolenga kupunguza
urasimu na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi, hatua
iliyosaidia kuongeza mapato ya Serikali.
Alisimamia
utoaji wa hati miliki za ardhi zaidi ya 1,992,245 kwa Watanzania hatua
iliyosaidia kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutumia hati hizo kama dhamana za
mikopo.
Alifanikiwa
kutenga ardhi yenye ukubwa wa ekari 224,439.4 kwa ajili ya uwekezaji kupitia
Mipango Kabambe ya miji, mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya na Vijiji.
Hatua hii ilisaidia kuongeza uwekezaji nchini na kutoa ajira kwa wananchi.
Akiwa
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM
Alianzisha
mfumo wa mbio za mwenge kwa kushindanisha mikoa katika maandalizi, hamasa na
utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mikoa husika. Suala hili lilileta
chachu ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa ufanisi na kuleta matokeo makubwa kwa
wananchi.
Alibuni
na kuanzisha mradi wa mabasi ya wanafunzi katika Mkoa wa Dar es Salaam jambo
ambalo lilipunguza adha kubwa ya usafiri kwa wanafunzi wa Jiji la Dar es
Salaam.
Akiwa
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
Alifufua
na kuimarisha kilimo cha mtama na kuanzisha shamba la ushirika la zabibu
akishirikiana na benki ya CRDB ambapo mradi huo sasa unasimamiwa na Wizara ya
Kilimo ukijulikana kama BBT (Bulding a Better Tommorow).
Alihakikisha
kuwa mipango ya upanuzi wa mji wa Dodoma inazingatia sheria na taratibu za
mipango miji ili kuzuia ujenzi holela, jambo ambalo lilikuwa ni msingi muhimu
wa ukuaji wa Mji mkuu wa kisasa.
Alisimamia
Ujenzi wa Chuo Kikuu cha UDOM, hatua iliyosaidia kuongeza udahili wa Wanafunzi
wa Elimu ya Juu nchini.
FAMILIA
Enzi
za uhai wake, Marehemu Lukuvi alifunga ndoa takatifu tarehe 28 Julai, 1990 na
Bi. Germina Lukuvi katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Jijini Dar es Salaam na
kujaaliwa kupata watoto watatu ambao ni Nobert William Lukuvi, Brown William
Lukuvi na Anifisye Vanessa William Lukuvi.
Marehemu
Lukuvi ameacha mjane, watoto watatu na mjukuu mmoja aitwae Donovan.
UGONJWA
NA KIFO
Marehemu
William V. Lukuvi alifariki dunia tarehe 25 Machi, 2026 saa 1:00 asubuhi katika
Hospital ya Benjamini Mkapa Jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya
kupata ugonjwa wa mshtuko wa Moyo.
Tunamsukuru
mwenyezi Mungu, kwa maisha ya Willian V. Lukuvi ambaye hakika aliitumikia
nafasi yake ya Ubunge na nafasi nyingine alizoaminiwa na serikali kwa bidii,
ufanisi na uadilifu wa hali ya juu. Tunaomba Mungu ampe pumziko la Amani.
RAHA
YA MILELE UMPE EE BWANA NA MWANGA WA MILELE UMWANGAZIE, APUMZIKE KWA AMANI,
AMINA.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.