Serikali
imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu
kwa kuwajengea uwezo watendaji wake katika matumizi ya mfumo wa kielektroniki
wa ukusanyaji na usimamizi wa taarifa za watu wenye ulemavu (PD-MIS), hatua
inayolenga kupata takwimu sahihi kuanzia ngazi ya kaya hadi mkoa.
Mafunzo
hayo yamehusisha Maafisa Tehama na Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Mikoa ya
Ruvuma, Mtwara, Lindi na Njombe, yakifanyika mkoani Ruvuma kwa lengo la
kuwawezesha washiriki kutambua na kusimamia matumizi ya mfumo huo katika maeneo
yao ya kazi.
Akizungumza
wakati wa mafunzo hayo, Afisa kutoka Kitengo cha Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu,
Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Bw. Jackob
Mwinula, alisema kuwa uwezeshaji huo ni muhimu katika kuhakikisha watendaji
wanakuwa na uelewa wa kutosha wa mfumo huo na kuwafikia wananchi kwa ufanisi
zaidi.
“Baada
ya mafunzo haya, tunatarajia kuona watu wenye ulemavu wakisajiliwa, kupata
namba za utambulisho na hivyo kuwezeshwa kufikia huduma mbalimbali za kijamii
pamoja na kuunganishwa na mifumo mingine ya Serikali,” alisema Bw. Mwinula.
Aliongeza
kuwa zoezi la usajili ni endelevu na litahusisha maafisa kuwafikia walengwa
moja kwa moja katika maeneo wanayoishi ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.
Kwa
upande wake, Bi. Suzana Mayengo, mwezeshaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu,
alisema mafunzo hayo pia yanalenga kuwajengea watendaji uwezo wa kutambua aina
mbalimbali za ulemavu na namna ya kushirikisha kundi hilo katika mipango ya
maendeleo ili kuhakikisha ushirikishwaji jumuishi na unaozingatia mahitaji yao.
Aidha,
upatikanaji wa taarifa sahihi utaiwezesha Serikali kutekeleza kikamilifu
Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2006 unaosisitiza
kauli mbiu ya “Nothing About Us Without Us”, inayolenga ushirikishwaji wa moja
kwa moja wa kundi hilo katika maamuzi yanayowahusu.
Naye
Mchambuzi wa Mifumo kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Bw. Antony
Nchimbi, alieleza kuwa mfumo wa (PD-MIS) umesanifiwa kwa ushirikiano kati ya
e-GA na Ofisi ya Waziri Mkuu, na umeunganishwa na mifumo mingine 11 ya Serikali
ili kurahisisha upatikanaji na ubadilishanaji wa taarifa.
Alibainisha
kuwa mfumo huo una uwezo wa kuwasiliana na mifumo muhimu ikiwemo wa wanafunzi
(SIS) kutoka TAMISEMI, mfumo wa afya (GoTHOMIS), mfumo wa mikopo (Wezesha) na
Mfumo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), hatua itakayosaidia
kuthibitisha na kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu nchini.


EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.