Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeridhishwa na utekelezaji wa maagizo iliyoyatoa mwezi Oktoba mwaka jana, kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambapo iliitaka Tume hiyo kuhakikisha inasimamia ukamilishwaji wa Mradi wa ujenzi kwa wakati wa ofisi za Tume hiyo jijini, Dodoma kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Akiongea mara baada ya kukagua hatua ya Mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi zilizopo eneo la Njedengwa Jijini Dodoma leo tarehe 15 Februari, 2020, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Mhe. Aeshi Khalfan Hilaly (Mb), amebainisha kuwa Kamati imeridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa ofisi za Tume hiyo kwa Jengo Kuu la Ofisi, Jengo la kutangazia matokeo na ghala la kuhifadhi vifaa.
“Tunaipongeza serikali kwa hatua ilizozichukua kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuhakikisha kuwa ujenzi wa Ofisi hizi unakamilika kwa wakati, kimsingi ni nia njema kamati kutembelea miradi ya serikali lakini tunapoona inafanya vizuri hatunabudi kuipongeza na ni imani yetu kuwa kwa malengo iliyoyaweka mwezi Aprili mwaka huu hatua kubwa ya utekelezaji itakuwa imefikiwa ” Amesisitiza, Mhe. Aeshi
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Mhe. Anthony Mavunde (Mb) amefafanua kuwa tayari wanatekeleza maelekezo ya Mhe.Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ambaye ameitaka tume hiyo kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa Ofisi za Tume hizo kwa wakati ili shughuli za uchaguzi za mwaka huu zinafanyika kwenye majengo hayo.
“Kutokana na mkandarasi mpya wa mradi huu ambaye ni SUMA JKT, Tumewahakikishia wanakamati wa PAC, kuwa ifikapo mwezi Aprili mwaka huu mradi wa ujenzi wa ofisi za Tume utakuwa umefikia hatua kubwa kwa kiwango cha kuruhusu shughuli za Tume kuanza kuendeshwa katika majengo haya, ambapo litakuwa ni jambo kubwa kwa kuwa katika historia tume hiyo haijawahi kuwa na ofisi yake yenyewe”Amesisitiza Mhe. Mavunde.
Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge) Tixon Nzunda, amefafanua kuwa hatua ya ujenzi wa mradi huo imeendelea vizuri baada ya kutekeleza maagizo ya Mhe. Waziri Mkuu ya kuvunja Mkataba wa mkandarasi wa awali wa mradi huo TBA na kusaini mkataba mpya na Kampuni ya Ujenzi ya Jeshi la Kujenga Taifa- SUMA JKT CCL.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelzaji wa Mradi wa Ujenzi wa Ofisi hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Wilson Mahera amebainisha kuwa Tume hiyo kwa kushirikiana na Chuo kikuu- Ardhi na Kampuni ya Ujenzi ya Jeshi la Kujenga Taifa- SUMA JKT CCL wanaouhakika mnamo mwezi Aprili mwaka huu Tume hiyo itaanza kuendesha shughuli zake kwenye majengo hayo.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni idara huru iliyoanzishwa mwaka 1993 kwa mujibu wa Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997, ambapo kwa kipindi chote hicho tangu kuanzishwa kwake Tume hiyo haijawahi kumiliki Jengo lake lenyewe, hivyo mnano mwaka 2016, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alikubali ombi la Tume hiyokujenga jingo lake.
Muonekano wa sehemu ya jengo Mradi wa Mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi za Tume hiyo zilizopo eneo la Njedengwa Jijini Dodoma leo tarehe 15 Februari, 2020.
|
Muonekano wa sehemu ya jengo Mradi wa Mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi za Tume hiyo zilizopo eneo la Njedengwa Jijini Dodoma leo tarehe 15 Februari, 2020
|
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.