WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekagua mradi wa ujenzi wa ofisi na studio za
Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na kuwaagiza wahusika wahakikishe
mradi huo unakamilika kwa wakati.
Ametoa
maagizo hayo leo (Jumapili, Januari 19, 2020) wakati akizungumza na
watumishi wa ZBC na wananchi baada ya kukagua mradi huo uliopo katika
wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba. Mradi huo wenye thamani ya
sh. bilioni 1.4.
Waziri
Mkuu amesema kukamilika kwa ujenzi wa ofisi na studio za ZBC kisiwani
Pemba kutaboresha sekta ya TEHAMA, hivyo kuwawezesha wananchi kupata
taarifa za ndani na nje kwa wakati. “Tunaimarisha ZBC ili kila mtu aweze
kupata habari kwa wakati.”
Pia,
Waziri Mkuu amewaagiza watumishi wa ZBC waongeze ubunifu katika
utayarishaji wa vipindi vyao pamoja na kutenga muda kwa ajili ya
kutembelea mashirika mengine ya utangazaji kwa lengo la kujifunza.
Kabla
ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuifanyia maboresho studio yake ya
kurushia matangazo ya Pemba wananchi wa kisiwa hicho walikuwa wanakaa
hadi wiki moja bila ya kusikia habari zinazohusu kisiwa hicho.
Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi waendelee kuwa na imani na
Serikali kwa sababu imejipanga katika kutoa huduma mbalimbali za kijamii
zikiwemo za maji, afya, elimu kwa Watanzania wote bila ya ubaguzi wa
aina yoyote.
Pia,
Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi waendelee kudumisha amani na utulivu
na wasikubali kushiriki katika matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa
amani kwa kuwa hayana tija.
“Amani,
utulivu na mshikamo tulionao nchini haujaja kwa bahati mbaya bali
umeasisiwa na viongozi wa kwanza wa Taifa letu hayati Mwalimu Julius
Nyerere pamoja na Sheikh Abeid Aman Karume hivyo ni muhimu tukawaenzi
waasisi wetu kwa kuimarisha amani.”
Awali,Waziri
Mkuu alikagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba sita za Askari Polisi
zinazojengwa katika eneo la Mfikiwa wilayani Chakechake. Kati ya nyumba
hizo sita, tano tayari zimekamilika na zinatumika. Nyumba moja ipo
kwenye hatua za kukamilika.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.